MFANYA biashara
wa madirisha ya alluminium jijini Arusha, Japhet Minja (30), amelazwa
katika Hospitali ya Selian jijini hapa, baada ya kumwagiwa kimiminika
kinachodaiwa kuwa ni tindikali usoni na watu wasiojulikana. Tukio
hilo la kusikitisha limetokea jana saa 12:15 alfajiri katika eneo la
Shamsi, wakati mfanyabiashara huyo akitoka nyumbani kwake kwenda kazini.
Akisimulia
tukio hilo, mmoja wa
ndugu zake ambaye hakutaja jina lake, alisema kuwa
Minja alikumbwa na mkasa huo wakati akienda kwenye shughuli zake za
kila siku.
Alisema
baada ya kufika eneo la Shamsi, Minja alikutana na vijana wanne wakiwa
wamesimama barabarani kisha walimsimamisha kama vile walikuwa wakitaka
kumuomba msaada.
“Baada ya ndugu yangu kusimama, alishusha kioo cha gari upande wake na
hapo wale vijana wakafungua mlango kwa nguvu na kumchomoa ndani ya gari
na kumtoa nje, kisha kumshambulia kwa kumpiga na baadaye kumwagia
tindikali usoni,” alisema.
Alisema kuwa baada ya kumwagia tindikali wakati watu waliokuwa karibu
na eneo hilo wakikusanyika vijana hao walikimbia na kutokomea
kusikojulikana.
Alisema watu hao walimchukua Minja na kumkimbiza hospitalini hapo kwa
matibabu waandishi wa habari walipofika hospitalini hapo kufuatilia
tukio hilo, walizuiwa na uongozi kutokana na majeruhi huyo kulazwa
chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU)Mganga wa
Hospitali hiyo, Dk. Godbless Massawe, aliyempokea Minja hospitalini hapo
kwa matibabu, alithibitisha kuwa alimwagiwa kitu ambacho mpaka sasa
hawajaweza kukibaini kwa kuwa vipimo vya kubaini tindikali kwa nchini,
vinapatikana Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Dk. Massawe alisema kitu alichomwagiwa Minja kilikuwa kinamsababishia
macho yake kukosa nguvu ya kuona, kadri muda ulivyokuwa ukienda huku
kikimsababishia apate maumivu makali kwenye ngozi ya uso.
Alisema wakati akiendelea kupatia huduma ya kwanza, alilalamika kuwa
anapata shida kuhema, wakamwekea hewa ya oksijeni na baada yamuda
alishindwa kuzungumza, lakini alianza kupata nafuu baada ya kuendelea
kumhudumia.
Dk. Massawe alisema baada ya kupata nafuu aliweza kusema kuna wateja
walikwenda nyumbani kwake na kumuomba awauzie madirisha kwa Sh. milioni
4, lakini walimpatia Sh. milioni 3.
Alisema baada ya kumapatia fedha hizo waliongozana hadi barabarani na
wakiwa njiani kuna watu wakazuia gari la wateja wake na alipoamua
kushuka, ndipo alipovamiwa na baadhi yao wakaingia kwenye gari lake na
kuchukua fedha zake kisha kummwagia ‘spray’ kwenye macho.
Alisema Minja aliendesha gari mwenyewe hadi duka moja la dawa nao
wakamshauri anawe uso na aliponawa aliambiwa aende hospitalini.
Alisema alikwenda zahanati moja ambayo hakuitaja na kushauriwa kwenda
hospitali kubwa na alipofika Selian, akaanza kujisikia vibaya na
kupoteza fahamu.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kusisitiza kwamba wanaendelea kufanya uchunguzi ili
kubaini kitu alichomwagiwa mfanyabiashara huyo.
“Kitu kinachotupa mashaka ni kimoja kuwa yule mtu aliendesha gari
mwenyewe, sasa kama tindikali utaweza kuendesha gari kweli, hivyo
vitakuwa visa tu,” alisema Sabas.
Matukio ya watu kumwagiwa tindikali yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka nchini.
Masoud Mohamed Shambi, mkazi wa kisiwa cha Pemba, alikumbwa na mkasa huo mwaka 2000.
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Zanzibar, Rashid Ali Juma
(45) naye, alimwagiwa tindikali Februari 18, 2011, saa 2:30 usiku, nje
ya msikiti wa Amaan.
Novemba
5, 2012, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga, alimwagiwa
tindikali na mtu asiyefahamika wakati akifanya mazoezi ya viungo kwenye
Uwanja wa Mwanakwerekwe.
Mwaka 2012 mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia mjini Zanzibar, Chandurali Chunilai Asawala alimwagiwa tindikali.
Mei 23, 2013, Sheha wa Shehia ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Mkoa Mjini
Magharibi, Mohamed Said Omar maarufu kwa jina la Kidevu, pia alimwagiwa
tindikali.
Agosti 7, 2013, saa 1:15 usiku, watu wawili waliokuwa katika pikipiki
kwenye eneo la Mji Mkongwe, Mtaa wa Shangani, waliwamwagia tindikali
mabinti wawili, raia wa Uingereza, Katie Gee (18) na Kirstie Trup (18)
waliokuwa Zanzibar wakifanya kazi ya ualimu kwa kujitolea.
Septemba 14, 2013, Padri Ancelmo Mwang'amba wa Kanisa Katoliki, Parokia
ya Cheju, alimwagiwa tindikali na mtu asiyejulikana katika maeneo ya
Mlandege.
Mwaka 1995, aliyewahi kuwa Mbunge wa Mwanza Mjini, Said Shomari
alimwagiwa tindikali na kujeruhiwa vibaya mwilini, hasa sehemu za
shingoni.
Usiku wa kuamkia Julai 13, Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Said Juma
Makamba alimwagiwa tindikali wakati akiwa nyumbani kwake eneo la
Kwamrombo, Arusha.
Mwingine ni mmiliki wa maduka ya Home Shopping Centre, Said Mohamed Saad
aliyemwagiwa tindikali Julai 19, 2013, usiku wakati akiwa kwenye jengo
kubwa la biashara la Msasani City Mall.
Mwingine ni Saeed Kubenea, Mkurugenzi wa Hali Halisi Publishers ambao
huchapisha gazeti lililofungiwa la Mwanahalisi aliyepatwa na mkasa huo
Januari 7, 2008.
No comments:
Post a Comment