Moshi. Watu wasiojulikana
wamevamia nyumba ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa (TCB), Adolf
Kumburu iliyopo Shanty Town, mjini Moshi na kuiba vitu mbalimbali vyenye
thamani ya mamilioni ya shilingi likiwamo gari.
Wezi hao walifanikisha dhamira yao baada kumteka
mfanyakazi wa ndani na kisha kumfunga kamba mikononi na vitambaa usoni.
Gari lililoibwa ni Toyota Raum namba T643 CDZ rangi ya Bluu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz
alithibitisha jana kutokea kwa tukio lililofanywa kati ya saa 6.00 na
saa 7.00 mchana.
“Ni kweli, tukio limetokea na miongoni mwa vitu
vilivyoibwa ni gari. Mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa na
tunaendelea na uchunguzi,” alisema Kamanda Boaz.
Kamanda Boaz ametoa wito kwa wananchi wenye
taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao pamoja na vitu
vilivyoibwa waziwasilishe kwa siri kwake ama kwa maofisa wake na majina
yatahifadhiwa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kumburu alisema wezi hao walifanikiwa kuiba vitu mbalimbali na kuvipakia katika gari lake.
Mbali na gari hilo, pia televisheni aina ya
Samsung Flat Screen, Deck aina ya Phillips, Micro-Wave, kompyuta mpakato
aina ya Apple Mac Book, Samsung Min-Tablet na Digital kamera mbili pia
viliibwa.
Kwa mujibu wa Kumburu, wezi hao huenda walitumia
mazingira ya ukimya katika eneo hilo la Shanty Town kutekeleza uhalifu
wao bila majirani kufahamu.
No comments:
Post a Comment