Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk
Makongoro Mahanga amembeza Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa kwa
hatua yake ya kumshambulia kupitia vyombo vya habari akibainisha kuwa
busara yake ni ndogo kama umri wake.
Dk Mahanga alimbeza Silaa juzi, wakati akizungumza
na gazeti hili kwa njia ya simu baada ya kuhojiwa ambapo alibainisha
zaidi kuwa, busara na umri alionao vinamwongoza asilumbane na viongozi
wenzake kwenye vyombo vya habari.
“Mimi nina miaka 58 yeye ana miaka 31, busara zetu
ni tofauti sana hata kwenye malumbano, ingawa mimi nina cheo kidogo
kwenye chama ukilinganisha na yeye, mimi ni mbunge tu CCM, mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Dar es Salaam na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa
chama, wakati yeye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM,” alisema Dk Mahanga.
Alisisitiza kuwa busara aliyonayo meya huyo ndiyo
iliyomfanya amfananishe na Punda ndani ya Baraza la Madiwani waliokuwapo
kwenye kikao hicho na waandishi wa habari waliohudhuria.
Kwa upande wake, Meya Silaa alibainisha kuwa
tuhuma dhidi ya Dk Mahanga zilitolewa ndani ya Kikao cha Baraza la
Madiwani Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, ambapo kwa mujibu wa tangazo
la Serikali namba 11 la Aprili 16, mwaka 2004, kanuni za kudumu za
halmashauri hiyo sehemu ya (iii) 24 inakataza suala lililojadiliwa
kwenye kikao hicho kuhojiwa nje ya hapo na chombo chochote ikiwamo
mahakama.
“Kanuni hiyo inaeleza kutakuwa na uhuru wa kutoa
mawazo wakati wa majadiliano katika mikutano ya halmashauri na uhuru huo
hautaweza kuhojiwa katika mahakama yoyote au popote nje ya mkutano wa
halmashauri,” Silaa alinukuu kanuni hiyo.
Oktoba 3, mwaka huu Meya Silaa, alikaririwa na
vyombo vya habari akiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya
Ilala,Dar es Salaam, akilaani vikali migogoro ya kisiasa isiyo na tija
kwa wananchi ukiwamo uliosababishwa na barua iliyoandikwa na Mbunge wa
Segerea ambaye ni Dk Mahanga.
Alidai kuwa barua hiyo ilisababisha aliyekuwa
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Gabriel Fuime kusimamishwa kazi bila
kufuatwa taratibu za utumishi hivyo kutia doa utumishi wake wa muda
mrefu.
Silaa alisisitiza kuwa, Dk Mahanga hakujali msaada
wa Fuime ambaye aliutoa jimboni kwake wakati wa Uchaguzi Mkuu 2010,
badala yake kuna barua ya siri iliyoandikwa kwenda Tamisemi ikimtuhumu
Fuime na Silaa wakidaiwa kuhusika na tuhuma mbalimbali za ubadhirifu.
Ilidaiwa kuwa kutokana na tuhuma hizo, Fuime
alisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yake ambapo miongoni mwa
tuhuma hizo ni pamoja na kushindwa kusimamia mapato ya halmashauri hiyo
na ukodishaji unaotia shaka katika Soko la Samaki Feri.
No comments:
Post a Comment