Zahir Zoro (Kulia) akiwa na mtoto wake Banana Zoro
Dar es Salaam. Zoro anasema kuwa mwaka 1981
walihamia Mafinga na ndiyo chimbuko hasa la kumpata mkewe huyo ambaye
anasimulia kuwa uhusiano wao ulikuwa wa kihistoria.
“Kipindi hicho tukiwa Mafinga rafiki yangu mkubwa
alikuwa ni Emmanuel Mpangala ambaye alikuwa akifanya kazi RTC, sasa
nilipokuwa nakwenda kumtembelea ndiyo nikamwona binti mrembo wa kutoka
kandokando ya Ziwa Nyasa Angela Mahinya ambaye kwa sasa ni marehemu,”
anaanza kusimulia Zahir kwa masikitiko yaliyochanganyika na huba.
Anasema akiwa anakwenda hapo mara kwa mara
wafanyakazi wengi walikuwa na shauku ya kumwona na kuongea naye kwa kuwa
alikuwa ni mwanamuziki anayefahamika, hivyo siku moja Mpangala
akamwambia kuwa Angela anataka kumwona, wakati huo alikuwa hamfahamu
zaidi ya kumwona juu juu akiwa katika kazi zake.
Anaendelea kueleza kuwa cha kushangaza siku
walipokutana na kuongea akiwa ofisini kwake alipoteza ujasiri wa kiume
aliokuwa nao, kwani aliona anasisimka hadi nywele na kuona kuwa huyu
anaweza kuwa ni mwanamke anayestahili kuwa mpenzi wake.
“Nilipoteza ujasiri mbele ya Angela kwa mara ya
kwanza tu nilipomwona na kujikuta akiniuliza jambo badala ya kujibu
nabaki namwangalia, nikajikaza na kurudi katika hali ya kawaida ingawa
bado mara nyingi nilikuwa sielewi,” anasema Zoro.
Anafafanua kuwa baada ya kukaa kwa muda ofisini
kwake wakapanga siku ambayo walitoka wote kwenda sehemu kuzungumza na
kuanzia hapo akawa anakwenda nyumbani kwake kama rafiki, huku akiogopa
kumwambia hisia zake akiamini anaweza kuvunja hata urafiki wao.
Anasimulia kuwa ilimchukua muda kumwingiza katika 18 zake licha ya kupewa msaada na Mpangala.
Zoro anasema baadaye Angela aligeuka kuwa mpenzi
wake bila kujua kutokana na kuwa na mazoea ya kuwa pamoja kila wakati
ikiwamo kwenda muziki pamoja usiku.
Anaendelea kusimulia kuwa wakiwa katika uhusiano
siku moja akaambiwa na Angela kitu kilichomshtua kuwa mtu mmoja
amewaambia kuwa yeye ana mke jijini Dar es Salaam ambaye ni Brigedia wa
Jeshi hivyo wakati wowote ataingia matatani.
Angela alianza kuomuogopa hali iliyomfanya wasikutane tena mara kwa mara.
”Hali ilikuwa mbaya upande wangu, mwanamke
unayempenda na uliyemsotea kwa muda mrefu anakuja mtu anamwambia maneno
ambayo yanatishia uhusiano wenu we acha tu”
Zoro anasema ili kumthibitishia kuwa hakuwa na mke
alichukua Angela akasafiri naye hadi kwa mama yake jijini Dar es Salaam
ili athibitishiwe kuwa yeye hakuwa na mke. Anasema alimueleza mama yake
uamuzi wake wa kuoa Angela na mama yake akakubali.
“Kama watu wanaoa basi mimi namuoa Angela bila kujali dini wala kabila na mama hakuwa na hiyana,”anasema Zahir huku akitabasamu.
Anasema baada ya utambulisho huo wa ghafla ikabidi
arudi Mafinga kazini na kumuacha Angela na mama yake yaani mama Zahir,
na akapewa zawadi nyingi kwa kuwa wakati huo mama yake alikuwa
mfanyabiashara mkubwa.
Anaongeza kuwa mama yake alimkubali Angela kwa asilimia mia na alikuwa ni kama rafiki yake akimshirikisha katika kila jambo.
Sekeseke la ujio wa Banana Zoro
Anasema baada ya likizo ya Angela kuisha alirudi
Mafinga na maisha yakaendelea ambapo alipata ujauzito ulimlazimu kwenda
kwao kujitambulisha kwa kuwa ilikuwa ngumu kujifungua kabla ya kwenda
kwao nakufuata taratibu.
Hata hivyo, kikwazo kilikuwa baba yake Angela,
Mzee Mahinya ambaye alikuwa mkali mno asiyependa mzaha kwa binti zake.
Alijiuliza itakuwaje akifika nyumbani kwao Angela eneo la Nyasa?
Pamoja na kupata taarifa hiyo, aliamua kwenda.
Alipofika Mbambabey, ikabidi aende kuomba msaada kituo cha Polisi
kilichokuwa eneo hilo kuomba msaada kwa kuwa yeye ni askari mwezao ili
wamsindikize.
Hata hivyo, askari polisi walikubali kumsindikiza
baada ya kuwaleza ujauzito aliompa Angela na hofu yake ya kukutana na
Mzee Mahinya.
Askari hao kwa kutumia gari la kituo hicho
walimsindikiza na kueleza Zoro alichokifanya kwa Angela na wakaomba
msamaha kwa nia yake na baadaye wakaeleza nia yake ya kutaka kumuoa.
Zahir anaongeza kuwa alikaa mwezi mzima kwa Mzee
Mahinya kwa wakati taratibu za ndoa zikifanyika. Baada ya muda mfupi
walifunga ndoa na Angela Mahinya.
Anasema akiwa kijijini hapo watu wengi kutoka
vijiji vya jirani vya Lumulo, Nkili,na Luwili walipata taarifa zake
hivyo walifika na kumuona na wengine kumpa zawadi kutokana na umaarufu
wake aliokuwa nao wa mwanamuziki nguli nchini.
Zahir anasema baada ya kusihi na Angela kwa miaka
15, walitengana baada ya mkewe kuondoka bila kumuaga, ingawa walikuja
kurudiana baadaye.
Itaendelea wiki ijayo ambapo Zahir ataelezea kilichomfanya aache Jeshi na kilichomsukuma kuimba wimbo wa ‘Mashujaa’.
Itaendelea wiki ijayo ambapo Zahir ataelezea kilichomfanya aache Jeshi na kilichomsukuma kuimba wimbo wa ‘Mashujaa’.
No comments:
Post a Comment