DIWANI wa kata ya Turwa katika
Halmashauri ya mji wa Tarime wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Charles Ndessi Mbusiro, amesema kuwa Chama cha Mapinduzi
(CCM), wilayani Tarime, kimepora uwanja wa michezo bila ridhaa ya
wananchi.
Diwani huyo alitoa tuhuma hizo juzi
wakati alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi wa Tarime waliohudhuria
maadhimisho ya miaka mitano ya kifo cha aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo
hilo, marehemu Chacha Zakayo Wangwe.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika
kwenye uwanja wa michezo wa Serengeti, diwani huyo alisema kuwa uwanja
huo ni mali ya wananchi wote wa Tarime lakini CCM kwa hila zake
wameupora.
“Baada ya
kuona uwanja huo ukitumiwa mara kwa mara na CHADEMA katika mikutano
yake, wamefanya ujanja na kupata hati ambapo sasa wanadai kuwa ni mali
yao.
“Ndugu zangu
wananchi wa Tarime napenda kuwafahamisha kuwa uwanja huu sasa ni wa CCM,
wamefanya njama na wameuchukuwa na wanadai kuwa ni wa kwao na tayari
wanataka kujenga vibanda na wameshagawana vibanda kila kiongozi ana
milango yake sijui kama wananchi mnalijua hilo?’’ alisema na kuhoji diwani huyo.
Diwani huyo alidai kuwa uwanja huo
ulijengwa na wananchi wote kipindi cha mfumo wa chama kimoja na kwamba
CCM haina hati miliki wala haina mamlaka ya kuupora.
Aliwabana viongozi wa CCM wawaambie
wananchi kama chama chao ni cha biashara au ni chama cha siasa kwani
viongozi wa chama hicho ndio waliojipanga kufanya biashara katika uwanja
huo.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati
tofauti, baadhi ya wananchi wa mji wa Tarime wamedai kusikitishwa na
kitendo hicho ambacho walisema ni cha kifisadi na kwamba jambo hilo si
la kufumbia macho.
“Unajua
hawa watu wa ‘magamba’ wamezoea sana dhuluma na ufisadi; hiki kiwanja
ni cha wananchi wote na wala si cha CCM sasa leo nimeshangaa kusikia
kuwa wamekichukua kwa nguvu ili kiwe mali yao kwa kweli halitawezekana,
tumechoka kuonewa liwalo na liwe lazima wakirudishe" alisema mwananchi mmoja Mwita Mseti mkazi wa mtaa wa Rebu.
Read more: http://talkbongo.blogspot.com/2013/08/diwani-chadema-afichua-njama-za-ccm.html#ixzz2b4UTvepj
No comments:
Post a Comment