Urafiki kati ya Bob Marley, Peter Tosh na Bunny
Wailers ulipelekea kuzaliwa kundi la muziki wa Reggae-The Wailers la
Jamaica. Kiini cha kuzaliwa Wailers ni Hubert Winston McIntosh au Peter
Tosh kama alivyojulikana na wengi.
Tosh alikuwa mwalimu wa muziki, ambaye baada ya
kukutana na Neville Livingston (Bunny Wailer), na Robert Nesta Marley
(Bob Marley) mwaka 1963, aliwafundisha kutumia vyombo vya muziki kama
magita, kinanda na vyombo vingine.
Mwishoni mwa 1963, Junior Braithwaite, Beverley
Kelso na Cherry Smith walijiunga na Wailers. Tosh na Wailer walijiondoa
Wailers mwaka 1974 na kumwacha Marley.
Tosh na Livingston walijiondoa kwenye kundi baada
ya kususa ziara za muziki nje ya nchi na kumlazimu Marley kutafuta
wanamuziki wengine. Marley aliunda kundi lingine kwa jina la ‘Bob Marley
and The Wailers’, yeye akiwa kiongozi, mwimbaji mkuu na mpiga gitaa.
Kwenye kundi hilo walikuwepo ndugu wawili, ‘Barrett brothers’, Aston
Barrett, maarufu Family Man au kwa ufupi Fams, akipiga gitaa la besi na
mdogo wake Carlton Barrett au kwa kifupi Carly akipiga dram na
waimbaji wa safu ya mbele, akiwemo mke Marley, Rita Marley, Judy Mowatt
na Marcia Griffiths.
Kifo cha Marley aliyezaliwa Februari 6, 1945,
kilisababisha pia makundi kadhaa ya muziki huo nchini Jamaica kuvunjika.
Carlton Barrett na Tosh walifariki dunia mwaka 1987, wengine
waliofariki dunia ni Braithwaite mwaka 1999 na Smith mwaka 2008.
Bob Marley alizikwa kitaifa siku 10 baada ya kifo
chake. Maneno yake ya mwisho kwa mtoto wake wa kiume, Ziggy Marley
yalikuwa: “Money can’t buy life.” Kwa maana fedha haiwezi kununua uhai.
Wailer na Beverley Kelso ndiyo pekee waliobaki hai kwenye kundi hilo miongoni mwa wale wa kwanza kabisa miaka ya 1960.
Desemba 3, 1976, siku mbili kabla ya tamasha huru
la muziki wa reggae “Smile Jamaica” lililoandaliwa na Waziri Mkuu wa
Jamaica, Michael Manley, Bob Marley, mke wake na meneja, Don Taylor
walijeruhiwa kwa risasi zilizofyatuliwa ovyo dhidi yao na mtu
asiyejulikana.
Ingawa dhamira ya shambulizi hilo haikujulikana
haraka, lakini wengi walihusisha tukio hilo na mambo ya kisiasa hasa
kutokana na mtafaruku wa kisiasa nchini humo.
Taylor na mke wa Marley walijeruhiwa vibaya, huku
Bob akipata majeraha madogo kifuani na mkononi. Pamoja na mashambulizi
hayo, tamasha hilo lilifanyika kama kawaida na Bob Marley alipanda
jukwaani.
Wengi walitegemea Bob Marley kutokuonekana siku
hiyo kutokana na hofu pengine angeweza kuuawa jukwaani, lakini
alijiamini na kupanda jukwaani akiwa na majeraha. Akiwa jukwaani,
alisema: “Watu wanaojaribu kuifanya dunia hii kuwa mbaya hawapumziki.
Sasa kwa nini mimi nipumzike. Bob Marley aliwakosa wasanii wake kadhaa
walioshindwa kupanda jukwaani kwa hofu.
Kutokana na hali hiyo, ilimlazimu kuwaazima
waimbaji wa kundi lisilofungamana na mambo ya kidini au kisiasa kuimba
pamoja naye mbele ya mashabiki 80,000.
Kifo:
Julai 1977, Marley aligundulika kuwa na kidonda
chini ya kucha kwenye kidole gumba cha mguuni. Tatizo hilo ambalo
kitaalamu (Malignant melanoma), lilikuja kusababisha kansa. Baada ya
uchunguzi, madaktari walibaini kuwa ugonjwa huo umeshaanza kusambaa
kutoka kwenye kidole, hivyo njia pekee ilikuwa ni kukatwa kidole, uamuzi
uliopingwa na Bob Marley.
Bob Marley alipuuza hata ushauri wa madaktari
waliomtaka kupunguza shughuli za muziki na badala yake aliendelea
kufanya ziara za muziki, ambapo mwaka 1980 alifanya ziara ya dunia.
Tamasha kubwa alilifanya Ulaya kwenye Mji wa
Milan, Italia, ambapo mashabiki 100,000 walishiriki. Baada ya kumaliza
ziara ya Ulaya, alikwenda Marekani na kufanya onyesho kwenye Ukumbi wa
Madison Square Garden.
Onyesho lake la mwisho nje ya nchi lilikuwa
Septemba 1980 kwenye Ukumbi wa Stanley Theater, Pittsburgh,
Pennsylvania, ambapo baada ya hapo afya yake iliporomoka zaidi kutokana
na kansa kuenea mwilini.
Kutokana na hali hiyo, maonyesho yake mengi
yalifutwa kabla ya kwenda kutibiwa kwenye Kliniki ya Josef Issels,
Ujerumani ambako baada ya miezi minane ya kutokupata nafuu, aliamua
kukodi ndege na kurudi nyumbani Jamaica.
Hata hivyo akiwa njiani, hali yake ilizidi kuwa
mbaya na kulazimika kutua kwenye Mji wa Miami, Florida alikopelekwa
Hospitali ya Chuo Kikuu cha Miami, ambapo alifariki dunia Mei 11, 1981
akiwa na umri wa miaka 36.
No comments:
Post a Comment