MBUNGE
wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) amesema sasa yuko tayari kufunga ndoa na
Mbunge mteule wa chama hicho wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua
Nassari.
“Nafurahi
kwamba Nassari hatimaye ameshinda ubunge katika uchaguzi mdogo,”
alisema Mdee wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa Arusha na Meru juzi
katika viwanja vya Leganga kusherehekea ushindi wa chama chake katika
uchaguzi huo.
Mdee
alifafanua, kwamba yeye na chama chake walikuwa wamebanwa na kampeni za
kuhakikisha Chadema inatwaa jimbo la Arumeru Mashariki na ndiyo sababu
hakujibu mara moja maombi ya Nassari ya kumwoa aliyoyatoa katika moja ya
mikutano yake ya kampeni.
“Naondoka
kwenda Dar es Salaam kujiandaa kwa Mkutano ujao wa Bunge, kisha
nitakwenda Dodoma ambako nitamsubiri Nassari na kwa pamoja tutafanya
maandalizi,” alisema Mdee huku akishangiliwa na hadhira hiyo huku
wakiimba na kucheza katikati ya mvua iliyokuwa ikinyesha.
Mdee alisema ndoa kati ya wabunge hao wawili wa Chadema ni wazo zuri na itatangazwa sana na kuandika historia.
Alipoona
anashambuliwa sana na wapinzani wake juu ya useja wake katika kampeni
hizo, Nassari hatimaye alitangaza kumwoa Mdee ambaye pia hajaolewa.
Na katika moja ya mikutano ya hadhara, alisimama naye jukwaani kukampeni.
“Kuna
viongozi wengi wa kidini Dodoma, ikiwa ni pamoja na ndani ya Bunge
ambao watatushauri jinsi ya kulitimiza hili,” alisema Mdee na kuongeza
kwamba baba yake Joshua, Mchungaji Samuel Nassari alipata kusema,
‘mwanamke mzuri ni zawadi kutoka kwa Mungu’.
Chadema
ina idadi kubwa ya wabunge vijana ambao hawajaoa, ikiwa ni pamoja na
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Mr Sugu’; wa Ubungo, John
Mnyika; wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na sasa Nassari.
Wakati
huo huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ametaka wananchi kutoa
maoni ya Katiba mpya ili walete mabadiliko mwaka 2015.
Aidha, amewasihi kuacha kutopiga kura, kwa kuwa katika uchaguzi wa Arumeru Mashariki waliojitokeza walikuwa wachache.
Aliwasihi
vijana kujitokeza Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litakapotolewa kwa
ajili ya kuboresha taarifa zao na wengine kujiandikisha upya.
Alisema
hayo katika mkutano huo na kumsifu Nassari ambaye alidai ni kijana
atakayeleta mabadiliko ndani ya jimbo hilo ingawa baadhi ya watu
walihoji umri na mambo mengine. Mbowe alisema chama hicho kitatumia njia
ya miguu, magari hata helikopta nchi nzima, kufikia wananchi ili watoe
maoni yao juu ya mchakato wa Katiba mpya.
Alitoa
rai kwa Polisi kuacha kupiga mabomu, kutumia risasi na nguvu zaidi,
nyakati za uchaguzi kwani vijana wanaoumia ndio watakaokuwa viongozi wa
baadaye.
"Nawashukuru
kwa kunipa kijana mjanja, yaani Nassari namkabidhi Lema (Godbless) ili
aje naye mjengoni (bungeni) na sisi wabunge wa Chadema tutampokea na
wananchi.
“Lakini
nawapasha ninyi vijana, kunapotokea suala la uamuzi wenu kwa ajili ya
maendeleo, pigeni kura na natoa rai, tumieni marekebisho ya Daftari
mjiandikishe na kulinda kadi zenu, ili tulete maendeleo, kwani ushindi
wa Chadema ndiyo safari ya CCM mwaka 2015 na kila wanapotupiga mabomu
tunashinda," alidai Mbowe.
Mbunge
wa Arusha Mjini, Lema alishukuru wananchi hao na kusema watuhumiwa wa
rushwa wakae chonjo, kwani baada ya Chadema kushinda Arusha Mjini na
Arumeru Mashariki maendeleo yatapatikana.
Aliomba
wananchi kuondoa itikadi zao za vyama na kumpa ushirikiano Nassari kwa
kuwa yeye ndiye mbunge atakayewaletea maendeleo. Katibu Mkuu Dk.
Willibrod Slaa, alisema ushindi huo ni wa kishindo, kwani walimtanguliza
Mungu na kutoa angalizo kuwa jimbo la Monduli nalo wanakaribia
kulichukua.
Mbunge
wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo alisema yeye si mtu wa ahadi hewa,
hivyo atashirikiana na Nassari kuchimba visima viwili na kuongeza kuwa
mfadhili wa chama hicho, Mustapha Sabodo, amejitolea kuchimba vinne ili
kuondoa kero ya maji jimboni humo.
Wabunge majeruhi Hali za wabunge wawili wa Chadema walioshambuliwa mwishoni mwa wiki Mwanza na kujeruhiwa wanaendelea vizuri.
Wabunge
hao wa Ilemela, Highness Kiwia na wa Ukerewe, Salvatory Machemli,
wamelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wakiendelea na
matibabu baada ya kupata rufaa kutoka Hospitali ya Bugando, Mwanza.
Akizungumza
na gazeti hili kwa njia ya simu, Machemli alisema bado wanaendelea na
matibabu hospitalini hapo na hali zao zinaendelea kuimarika. Alisema
Kiwia bado hajafanyiwa kipimo cha MRI ili kuangalia usalama wa kichwa,
kutokana na majeraha kichwani.
Habari kwa hisani ya Habari Leo
No comments:
Post a Comment