TTCL

EQUITY

Friday, June 28, 2013

Billioni 161/-Kutumika ziara ya Obama

  Ni kwa siku tano atakazokuwa barani Afrika

Rais wa Marekani, Barack Obama
Ziara ya Rais wa Marekani, Barack Obama ya siku nane katika nchi tatu za Afrika ikiwamo Tanzania, itaigharimu hazina ya Marekani kiasi cha Dola za nchi hiyo kati ya milioni 60 na 100 (Sh. bilioni 97 na Sh. bilioni 161) hadi kukamilika kwake.

Aidha, ziara hiyo imesababisha kuahirishwa kwa uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata nne za Jiji la Arusha uliopangwa kufanyika Juni 30 mwaka huu na sasa utafanyika Julai 14.


Fedha hizo zinatosha kuendesha wizara tatu za Tanzania kwa mwaka mmoja kwa mujibu wa bajeti ya mwaka 2013/14 iliyopitishwa juzi bungeni.


Wizara hizo ni Ofisi ya Makamu wa Rais Sh. bilioni 55.6; Wizara ya Maliasili na Utalii Sh. bilioni 75.6 na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Sh. bilioni 30.3.


Mbali na Tanzania, ambako ziara hiyo ya Rais Obama itafanyika kuanzia Julai Mosi, nchi nyingine ambazo atazitembelea ni Senegal na Afrika Kusini.


Ziara hiyo ya Rais Obama inaanza rasmi leo katika Jiji la Dakar, nchini Senegal, kisha Johannesburg na Cape Town, nchini Afrika Kusini na hatimaye jijini Dar es Salaam na inatarajiwa kumalizika Julai 3, mwaka huu.


Kwa mujibu wa habari iliyoandikwa na gazeti la The Washington Post la Marekani, kiasi hicho cha fedha kitatumiwa na idara za usalama za Marekani kuhakikisha usalama wa Rais Obama na familia yake.

Gazeti hilo lilisema mamia ya mashushushu wametumwa katika nchi za Senegal, Afrika Kusini na Tanzania kuandaa mazingira ya usalama.


Lilisema manowari ya kijeshi inayobeba ndege, iliyo na kituo cha matibabu, itawekwa katika Pwani ya Afrika, tayari kukabili dharura yoyote.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, ndege za kijeshi za mizigo zitabeba magari 56 ya msaada, magari 14 aina ya ‘Limousines’ na malori matatu yaliyo na vioo maalum vya kuzuia risasi, vitakavyowekwa kwenye madirisha ya hoteli itakakoishi familia ya Rais Obama.


Pia lilisema ndege za kijeshi zitakuwa na zamu za kuruka, zikitoa ulinzi wa saa 24 katika anga, ambayo Rais Obama atapita na kukaa ili kuingilia pindi itakapotokea ndege isiyo rafiki kumkaribia.


Gazeti hilo lilieleza kuwa ufafanuzi wa masharti ya usalama utakaoligharimu taifa hilo mamilioni ya dola, uko kwenye nyaraka ya siri, ambayo liliipata, japokuwa maandalizi yakionekana kuwa ya kawaida, kama yaliyofanyika siku za nyuma kwa marais wa nchi hiyo.


Lilisema safari yoyote ya rais kama ile aliyoifanya Ireland ya Kaskazini na Ujerumani ni za gharama na changamoto kubwa, lakini ziara ya Afrika zinaongezwa ugumu kutokana na mazingira yake ya kiusalama.


Gazeti hilo lilisema sababu hizo zinazoweza kuifanya ziara katika bara hilo kuwa ya gharama zaidi katika kipindi chake cha uongozi wa taifa hilo.


Lilisema familia hiyo inafanya ziara hiyo, huku maofisa wa serikali ya Marekani wakitoa karibu rasilimali zote zinazohitajika, bila ya kutegemea zaidi vyombo vya ulinzi vya ndani ya nchi hizo, kama vile polisi, mamlaka za kijeshi au huduma za hospitali kwa matibabu.

Gazeti hilo lilisema Rais Obama na mkewe walipanga kutembelea pia mbuga za wanyama, kama sehemu ya ziara, ambayo ingehitaji timu ya ulinzi, kubeba bunduki maalum za kukabiliana na duma, simba au wanyama wengine, ambao wangeleta rabsha kwa mujibu wa nyaraka ya ziara hiyo.


Hata hivyo, gazeti hilo lilisema ziara ya Rais Obama kwenye mbuga za wanyama nchini imefutwa na badala yake atafanya ziara katika kisiwa cha Robben nje ya Pwani ya Cape Town, nchini Afrika Kusini alipokuwa amefungwa Rais mstaafu wa nchi hiyo, Nelson Mandela.


Lilieleza kuwa kila Rais wa Marekani anapokuwa na safari nje ya bara la Amerika, huwa kuna matumizi makubwa ya fedha kwa ajili ya ulinzi.


Kwa mfano, gazeti hilo lilieleza kuwa ziara ya Rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton, aliyoifanya barani Afrika, mwaka 1998, iligharimu Dola za Marekani milioni 42 (Sh. bilioni 68).


HALI ILIVYO SENEGAL


Kwa mujibu wa Radio ya Vatican, wananchi wa Senegal wana shauku kubwa ya kumwona Rais Obama kwa kuwa wanaamini atakuwa mkombozi wao wa maendeleo.


Poirier, mtangazaji wa radio hiyo alisema wananchi wa Segegal wanataka kumwonyesha Rais Obama kuwa kuna watu maskini nchini humo na kwamba, nchi inahitaji msaada wa uwekezaji wa kimaendeleo.


Alisema wananchi hao kwa sasa wamepanga kumwonyesha Rais Obama kuwa Senegal haina huduma bora za afya na elimu.


Alieleza kuwa hadi sasa hali ya ulinzi nchini humo imeimarishwa, hususan mipakani na viwanja vya ndege kwa kuwapo upekuzi wa hali ya juu kwa raia wanaotaka kuingia.


 ZUMA AMZUNGUMZIA OBAMA


Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, akizungumza na wahariri wa habari, alisema Rais Obama anatarajiwa kuwasili Afrika Kusini keshokutwa.


“Marekani ni moja ya wawekezaji wakubwa katika biashara, utalii na teknolojia hapa Afrika Kusini. Kuna kampuni 600 za Marekani zilizowekeza hapa nchini,” alisema Rais Zuma.


Alisema ujio wa Rais Obama utaongeza misaada kutoka Marekani nchini Afrika Kusini pamoja na kuimarisha huduma za afya, elimu, kilimo, utungwaji wa sheria, biashara, uwekezaji, nishati pamoja na uimarishwaji wa ulinzi nchini humo.


Taarifa kutoka Ikulu ya Afrika Kusini inaeleza kuwa, Rais Obama akiwa nchini humo hataweza kuonana na Mandela, bali atakwenda katika kisiwa cha Robben alichofungwa.


Ilieleza kuwa baada ya kutoka katika kisiwa hicho atatembelea sehemu mbalimbali za Cape Town na mwishoni kuhutubia katika Chuo kikuu cha Cape.


UCHAGUZI ARUSHA WAAHIRISHWA


Tume Taifa ya Uchaguzi (Nec) imeahirisha uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata nne uliopangwa kufanyika Juni 30 hadi Julai 14, mwaka huu.


Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, alitaja sababu za kuahirisha uchaguzi huo kuwa ni pamoja na tume kutaka kujiridhisha kuhusiana na hali ya usalama jijini Arusha, ambako uchaguzi huo ulitarajiwa kufanyika.


“Ni kweli hali ya usalama imeanza kurudi taratibu baada ya matukio ya kulipuliwa kwa mabomu na kusababisha baadhi ya watu kuumia na wengine kupoteza maisha,” alisema Jaji Lubuva na kuongeza:


“Lakini ili uwapo utulivu kamili; yaani hali iwe nzuri zaidi, tume kutokana na hali ilivyo hadi sasa baada ya tukio la kulipuliwa kwa bomu la machozi, wimbi la amani halijatulia bado. Hivyo, muda unatakiwa kuongezwa zaidi hadi pale hali ya usalama itakapokuwa kamilifu.”


“Kutokana na hiyo, tume imeamua kuahirisha tena uchaguzi huo kwa kusogeza mbele wiki mbili zaidi na hivyo badala ya kufanyika Jumapili wiki hii mwisho wa mwezi huu, utafanyika Julai 14, mwaka huu.”


Alisema Juni 15, mwaka huu, ilikuwa siku ya mwisho kukamilisha kampeni kwa ajili ya chaguzi katika kata 26, lakini siku hiyo hiyo walisikia tukio hilo la kwanza la kulipuliwa kwa mabomu na kusababisha madhara hayo katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendelo (Chadema) jijini Arusha.


Jaji Lubuva alisema kutokana na tukio hilo, Nec walifanya kikao mjini Pemba na kufikia maamuzi ya kuuahirisha uchaguzi huo wa udiwani katika kata nne, eneo la Arusha mjini hadi Juni 30, mwaka huu, kwa ajili ya kusubiri kurejea kwa hali ya usalama.


Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, tume ingeamua kufanya uchaguzi huu mwishoni mwa mwezi huu kama ilivyopanga ingekuwa si kwa manufaa ya umma kwa kuwa bado hali ya utulivu haijatengemaa vizuri mbali na kuanza kurejea taratibu.


Hata hivyo, wachambuzi wa mambo ya siasa wanasema huenda Nec imechukua hatua hiyo kutokana na ujio wa Obama.


Kata hizo ni Themi, Kimondolu, Elerai na Kaloleni zote za Arusha mjini.


MACHINGA WALIZWA DAR


Katika kile kilichotafasiriwa na baadhi ya wafanyabiashara ndogo ndogo jijini Dar es Salaam kuwa ni shinikizo la ziara ya Rais Obama, jana Manispaa ya Kinondoni iliendelea na zoezi la safishasafisha, kwa kuvunja na kusomba mali zilizokutwa katika barabara ya Morogoro.


NIPASHE jana ilishuhudia baadhi ya maofisa wa manispaa waliombatana na mgambo wa jiji pamoja na askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa katika magari matatu katika eneo la Ubungo wakikusanya mali mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara.


Wakati FFU wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser maofisa wa manispaa na baadhi ya mgambo wa jiji walikuwa kwenye gari kubwa aina ya TATA likitumika kubebea mali na vifaa vyote vilivyokamatwa, vikiwamo viti na meza.


Akizungumza na NIPASHE, mmoja wa waathirika wa kadhia hiyo, Alex Mariaga, aliyekuwa na kiosk kilichokuwa kikiuza bidhaa ndogondogo, zikiwamo biskuti, maji, juisi, soda, pipi na vitambaa vya kufutia jasho karibu na kilipo kituo cha mafuta Ubungo, alisema safishasafisha hiyo imemgharimu sana.


“Yote hii ni sababu ya ziara ya Obama. Nilikuwa na biashara yenye thamani ya Sh. 150,000, ambayo ilikuwa ikinisaidia sana. Sasa naanza upya na sijui nitafanya nini,” alisema.


Hata hivyo, mwananchi mwingine, Mariamu Abdallah, anayefanya biashara ya kuuza magazeti katika eneo hilo, alisema magazeti yao hayakuchukuliwi.


“Waliochukua ni meza na kiti nilichokuwa ninauzia, lakini magazeti wameyaacha. Ninashukuru kwa hilo kwa sababu kama wangechukua ingekuwa ni hasara kwa upande wangu kwa kuwa nisingeweza kupata fedha za kulipia hasara hiyo kwa bosi,” alisema.


Msemaji wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhowera, alipinga madai yaliyotolewa na wafanyabiashara hao kuwa safishasafisha inayofanywa na manispaa inatokana na ujio wa Rais Obama.



Imeandikwa na Isaya Kisimbilu, Raphael Kibiriti na Gwamaka Alipipi.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment