DINA MARIOS ATAKA WATOTO WAWILI
Dina Marioa kushoto na BIN ZUBEIRY,swahiba wake wa siku nyingi. Picha na mwandishi wetu. |
KATIKA sauti ambazo hurindima na kusikilizwa sana kwenye anga za miji mikubwa ya Tanzania majira ya mchana ni ya Dina Marios, mtangazaji wa kituo cha redio cha Clouds FM.
Ni mwendeshaji wa kipindi cha Leo Tena. Amefanikiwa kujikusanyia mashabiki wengi kutokana na ubunifu na mbwembwe zake.
Gazeti la Mwanaspoti leo limeandika leo kwamba Dina hayupo peke yake katika safari ya kipindi hicho cha saa tatu kinachorushwa kuanzia Jumatatu mpaka Ijumaa, huwa na watangazaji wengine wawili, Gea Habibu na Zamaradi Mketema wakisaidiwa na Bi Ponza.
Yafuatayo ni mahojiano ya Dina na Mwanaspoti yaliyofanyika wiki hii.
Linapokuja suala la mahusiano ya kimapenzi, wewe unajiweka katika nafasi ipi?
"Unajua katika ulimwengu tuliopo hivi sasa, vijana wengi hawana subira, hawana uvumilivu wala upendo wa dhati.
"Kabla suala hilo halijaanza, kwanza kabisa mnakutana watu wawili mliotoka katika malezi tofauti hivyo kila mmoja ana tabia zake ila kinachowakutanisha pale ni mapenzi.
"Wengi wanashindwa kuvumiliana katika kipindi kigumu, hapa inaweza kuwa ni ugonjwa, kipato, mabadiliko, maana unaweza ukamwona mwenzako amebadilika kwa wakati fulani, watu hawapo tayari kwa nyakati kama hizi.
"Kuna idadi kubwa ya wanawake ambao wameamua kuzaa na kuishi bila waume, ni kwa sababu wameshaumizwa sana, na hawa ni wale wenye kipato chao na wanaojiweza kimaisha.
"Lakini wapo wanaosema kuwa siwezi kuishi bila ya mwanaume inatakiwa tujiamini, ukijiamini na kujipenda mwenyewe utapendwa."
Katika suala la mahusiano, una malengo gani katika maisha hayo?
"Huwa sipendi sana kuzungumzia mahusiano yangu. Lakini niliwahi kuwa katika mahusiano ambayo yalidumu kwa takribani miaka minne, kwa bahati mbaya hayakuendelea kutokana na yale niliyoyasema mwanzo.
"Nina malengo makubwa katika maisha yangu ya mahusiano, mimi ni mwanamke na ninategemea siku moja nitakuja kuwa na mume na ninamwomba Mungu anijalie watoto wawili."
Miaka ya hivi karibuni ulikuwa unaonekana mnene lakini sasa umepungua kwa kiasi kikubwa, imekuwaje?
"Hakuna mtu mnene ambaye hapendi kupungua, unajua ukiwa mwembamba unatamani unenepe kwa kuwa unakuwa bado hujaujua unene na kero zake.
"Lakini kwangu ilikuwa kero, nilikuwa nikivaa naona sipendezi na kuna wakati niliahirisha kwenda kwenye hafla kadhaa kutokana na kunenepa kupita kiasi hata nguo niliona hazinipendezi tena.
"Siri ya mafanikio ni mazoezi, japokuwa awali nilishameza dawa nyingi na ikafikia hatua nikanywa hata dawa za kuhara ili nipungue, lakini niligonga mwamba.
"Nashkuru kwani mara nilipoanza kufanya mazoezi ya sarakasi katika kituo cha THT, pamoja na kupunguza kula nikajikuta nikipungua mwili.
"Ikiwa mtu anahitaji kupungua afikirie hivyo kwa hitaji lake atafanikiwa."
Miaka minne ya nyuma uliwahi kueleza kuwa una mpango wa kuanzisha kipindi maalum cha Talk Show, mpango ambao unazidi kupata wawekezaji hapa Tanzania vipi mpango huo bado unao?
"Maisha yangu ninayapanga, mawazo nilikuwa nayo na nikiwa na wazo mara nyingi nilikuwa nikiwashirikisha watu na ndiyo maana wengi hutumia mawazo yangu kusonga mbele.
"Lakini si kwamba sitafanya tena kwa kuwa Talk Show zipo nyingi Tanzania kwa sasa, ila natafuta kitu cha utofauti na najua nini Watanzania wataka kutoka kwangu."
Kuhusu Leo Tena, kipindi kinawalenga akina nani hasa, na kwanini kilipunguzwa muda kutoka urefu wa saa nne mpaka saa tatu?
Kipindi chetu kinawalenga wanawake kwa wanaume na hata watoto, lakini walengwa wakubwa zaidi walikuwa wanawake.
"Kuhusu muda tulikuwa tuna nafasi kubwa sana na hivyo tunajikuta tunapiga zaidi muziki, na kipindi cha asubuhi Power Breakfast wao wakawa na muda mchache lakini kipindi chao kimemezwa na matangazo mengi, hivyo katika kulinganisha ikabidi muda ubadilishwe."
Siku hizi kuna vipindi vya redio tofauti vinavyofanana, hata staili ya utangazaji nayo vilevile huku wengine wakiongea mpaka kupitiliza, unalizungumziaje hilo?
"Hilo lipo tena haswaa! Nadhani inatokana na uvivu wa kufikiri, watu wanashindwa kujituma, hawana ubunifu kwa wasikilizaji au watazamaji wao.
"Si kwamba nawaponda watangazaji wenzangu, la hasha! Lakini tabia ya kukopi na kupeleka matangazo kama yalivyo si busara na wasikilizaji hawataki hivyo wanataka kusikia vitu tofauti.
"Mtu anapochukua ubunifu wangu si kwamba ninachukia hapana, ila najiona kuwa nina mawazo ya kuwafanya na wengine waige kwa hiyo najikubali. Wapo ambao waliweka wazi kuhusu nini nafanya na wakasema kuwa wananikubali."
Inakuwaje linapokuja suala la kuzungumza maneno yasiyofaa mpaka wasikilizaji wanazima redio au kubadilisha stesheni?
"Tatizo hilo lipo na ni sugu hapa nchini, ninachoweza kusema mimi ni ushauri kwa hawa watangazaji, kuwepo na mipaka kwani tatizo hilo lilikuwepo kwetu awali.
"Lakini baada ya kufuatwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) tulikaa chini na kupanga, kweli mwanzoni tulikuwa tukijiachia mno na kuzungumza lolote.
"Redio za sasa zinafuata nyayo za nini tunafanya na wao wanaiga, lakini ni vema kuiga kile ambacho una uwezo wa kukikarabati na si kuiga kila kitu.
"Wapo walioiga kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa Leo Tena."
Dina kabla ya kuwa mtangazaji uliwahi kufikiria kuja kufanya kazi gani?
"Siku zote nilikuwa nikipanga kuwa Mwanasheria, hilo ndilo lilikuwa wazo langu kubwa kabla sijaingia katika tasnia ya habari na utangazaji."
Unakumbana na changamoto zipi katika kazi yako?
"Changamoto ni nyingi, lakini kubwa zaidi ni katika kujipanga. Mimi naumiza sana kichwa nikifikiria nimpe nini msikilizaji wangu aridhike na kumwondoa mawazo ambayo alikuwa nayo kabla ya kipindi.
"Nataka baada ya kipindi nimwache anacheka au amefurahi na kubadilishwa kimtazamo. Kwa kifupi silali muda mwingi nautumia nikiwa na timu yangu tukijipanga nini tunafanya."
No comments:
Post a Comment