TTCL

EQUITY

Monday, February 6, 2017

Ukiyataka mafanikio yoyote makubwa na ya muda mrefu kuwa kiziwi msikivu!

Successful businesspeople raising hands upward.Ni muda mwingine tulivu kabisa tunakutana kupitia safu hii nikiamini kwamba umzima na unaendelea kupambana kuhakikisha maisha yako yanakuwa mazuri.

Mimi namshukuru Mungu kwa kuwa amenipa afya njema na maarifa ambayo nayatumia katika kuyaboresha maisha yangu lakini pia kuboresha maisha yako kwa kukuandikia makala ambazo naamini zinaweza kuyabadili maisha yako endapo utazifanyia kazi.
Mpenzi msomaji wangu, katika kipindi chote ambacho nimekuwa nikizungumzia kuhusu masuala ya mafanikio, nimekuwa nikisema kwamba unaowaona leo wana mafanikio, walipambana na hawakukata tamaa pale walipokumbana na changamoto mbalimbali.
Hawa ni wale ambao walijua fika kwamba kukata tamaa ni adui mkubwa wa mafanikio. Unapojaribu jambo mara moja ukashindwa kisha ukakata tamaa, ni dhahiri hukuwa umedhamiria kusaka mafanikio.
Wenye dhamira ya dhati huwa hawakati tamaa, watajaribu tena na tena na tena mpaka pale ambapo wataona ndoto zao zimetimia. Na wewe unayesoma makala haya unatakiwa kuwa hivyo.
Lakini, tambua wapo baadhi ya watu wanaokuzunguka ambao watafurahi kukuona unaendelea kuishi maisha duni. Wanakuwa na ile dhana kwamba ukifanikiwa utaringa, hutawaheshimu lakini pia utaonekana uko juu yao.
Kutokana na hilo usishangae watu hao wakakupiga vita na wakati mwingine kukukatisha tamaa kwenye yale unayoyafanya. Watakuambia huwezi kufanikiwa kwa sababu elimu yako ni ndogo au watakuambia huwezi kupata mafanikio kwa kuwa uko kijijini.
Watakuaminisha kwamba bila kuwa na elimu kubwa, bila kwenda mjini huwezi kufanikiwa. Ukiwa na akili ndogo zisizojua kuchambua mambo, unaweza kuona wanachokisema ni kweli na ukajikuta unapunguza kama siyo kuacha kabisa jitihada za kupambana kutafuta mafanikio.
Ndiyo maana nikasema kwamba, wewe kama wewe unatakiwa kujiaminisha kwamba unaweza kuwa kama hao unaowaona wana mafanikio makubwa. Jiambie kabisa kwamba kukata tamaa kwako ni mwiko.
Ukiwa na mawazo hayo, wale waliojikatia tamaa ya maisha hawawezi  kukushawishi muwe kwenye mkumbo mmoja. Lazima utakaa mbali nao na kutafuta wale ambao unaamini wanaweza kuwa na mawazo kama yako.
Nilishawahi kusema kwamba, ukiwa ni mtu wa kutaka mafanikio, marafiki zako wawe na mawazo hayo. Kaa mbali na watu wanaokuambia maneno ya kukukatisha tamaa, fahamu hao ni adui wengine katika kufanikiwa kwako.
Kwa maana hiyo usikubali wale waliokata tamaa wakukatishe tamaa, pambana huku ukijua kwamba hakuna wa kuyabadilisha maisha yako isipokuwa wewe mwenyewe.
Ukikubali ndani ya nafsi yako kwamba umeshindwa na huwezi kufanikiwa, hakuna muujiza utakaojitokeza. Utaendelea kuogelea kwenye dimbwi la umasikini mpaka pale utakapoamua kubadili fikra zako.
Hivyo basi, dawa ya wale wasiopenda mafanikio yako ni kukaa nao mbali na kukubali uwezo ulionao bila kufikiria watu wanasema nini juu yako. Amini unaweza, kubali changamoto na uzifanyie kazi kisha muombe Mungu akuongoze katika kila unalolitenda.
Kwa leo naomba niishie hapo ila nikuambie tu kwamba kama una lolote ambalo linakukosesha amani, usikae nalo likazidi kukuumiza, unaweza kuwasiliana na mimi kupitia namba za simu zilizopo hapo juu ili niweze kukushauri.

No comments:

Post a Comment