Tanzania
imekuwa nchi ya kwanza duniani kufanya majaribio ya kupambana na mbu
waenezao magonjwa mbalimbali ikiwemo malaria kwa kutumia kitambaa
kilichowekewa viatilifu ili kudhibiti ugonjwa malaria ambao ni tishio
kwa afya ya wananchi wengi wanaoishi vijijini.
Hatua
hiyo ya utafiti imefikiwa na watafiti wa magonjwa ya binadamu katika
cha taifa cha Magojwa ya Binadamu (NIMR) katika kituo cha Amani mkoani
Tanga ili kuweza kuwadhibiti mbu waenezao ugonjwa malaria ambao
unaathiri watu wa rika zote nchini.
Hayo
yamesemwa na Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR)
cha Amani mkoani Tanga Dkt. William Kisinza alipokuwa akiongea na
waandishi wa habari kutoka Kituo cha Waandishi wa Habari wa Kimataifa
(ICFJ) na Taasisi ya “Malaria No More” kutoka nchini Marekani ambao
walitembelea kituo hicho mwishoni mwa wiki kujionea namna Tanzania
inavyopambana na ugonjwa huo.
Katika
kufanikisha majaribio hayo, Dkt. Kisinza amesema kituo hicho
kinaendelea vizuri na majaribio ambapo wanatarajia mchanganuo wa utafiti
huo utafanyika mwishoni mwa mwaka 2016 na taarifa kamili itatolewa
rasmi mwaka 2017 ili iweze kutumika nchi nzima na duniani kote.
Dkt.
Kisinza amesema kuwa mafanikio ya taasisi yake yanatokana na
ushirikiano mzuri uliopo na taasisi nyingine za kitaaluma ndani na nje
ya nchi.
Miongoni
mwa taasisi hizo ni Chuo Kikuu cha Afya cha Kilimanjaro (KCMC), Kituo
cha Kudhibiti Kuzuia na Magonjwa cha Marekani (CDC), Taasisi ya Tiba,
Dawa na usafi wa mazingira ya London nchini Uingereza (LSHTM) na Chuo
Kikuu cha Brandeis cha nchini Marekani.
Naye
Mtafiti Mkuu anayesimamia zoezi la majaribio hayo ya mradi huo wa
vitambaa vyenye viatilifu hivyo vijulikanavyo kama “insecticide treated
wall liners”, Dkt. Joseph Mugasa amesema kuwa zoezi hilo linahusisha
vijiji 44, kaya zaidi ya 25,000 na idadi ya watu wanaonufaika na
majaribio hayo ni zaidi ya 100,000 katika maeneo mbalimbali ndani ya
wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
Mbali
na kuangalia uwezo wa vitambaa hivyo, mradi huo unaangalia pia uwezo wa
vitambaa hivyo katika kukabiliana na upugufu wa damu kwa watoto chini
ya miaka 11, uwezo wa vitambaa kupambana na mbu sugu kwenye viatilifu
vingine na pia kufanya tathmini ya gharama anazoingia mwananchi katika
kugharamikia tiba za malaria.
Kitambaa
hicho ambacho huwekwa kwenye kuta za nyumba kwandani hutumika sambamba
na chandarua ili kuweza kutoa kinga madhubuti mara mbili kumkinga
binadamu dhidi ya mbu waenezao magonjwa.
Mradi
huo wa majaribio wa kutokomeza ugonjwa wa malaria umeanza kufanyiwa
utafiti nchini miaka mtatu iliyopita kuanzia 2013 na unafadhiliwa na
Shirika la Misaada la Marekani (USAID) chini ya Mpango wa Rais wa
Marekani wa Kukabiliana na Malaria (PMI) ambao hadi kukamilika kwake
utarajiwa kugharibu zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 3.
Kwa
upande wake Meneja wa Mawasiliano Taasisi ya “Malaria No More” ya
nchini Marekani ambaye pia ni Mkuu wa msafara wa waandishi hao Dena
Gudaitis amesema kuwa wamefurahishwa kuona Tanzania ilivyosimama imara
kujali afya za wananchi wake hasa watu wa kipato cha chini ambao wengi
wao wanaishi vijijini.
Katika
kutekeleza wajibu wao wa kiuandishi, waandishi hao kutoka ICFJ
wanaongozwa na kaulimbiu ya taasisi hiyo inayosema “Andaa mazingira bora
ya mwandishi wa habari wa kimataifa ajaye”.
Waandishi
hao wa habari wamefanya ziara ya siku tano nchini kuanzia Mei 8 hadi
13, 2016 katika mikoa ya Dar es salaam, Arusha na Tanga ambapo
wametembelea baadhi ya zahanati katika mikoa hiyo, familia zenye watoto
walio chini ya mpango wa majaribio wa kudhibiti malaria, vituo vya
utafiti vya Korogwe na Amani pamoja na kiwanda cha kutengenezea
vyandarua cha A to Z cha jijini Arusha.
Mkuu
wa Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) cha Amani mkoani
Tanga Dkt. William Kisinza akiongea na waandishi wa habari kutoka Kituo
cha Waandishi wa Habari wa Kimataifa (ICFJ) na Taasisi ya “Malaria No
More” kutoka nchini Marekani ambao walitembelea kituo hicho mwishoni mwa
wiki kujionea namna Tanzania inavyopambana na ugonjwa huo.
Dkt.
Robert Malima akitoa maelezo ya namna watafiti wanavyofanya utafiti na
kuwakusanya mbu katika chumba maalum cha kufanyia utafiti kwa waandishi
wa habari kutoka Kituo cha Waandishi wa Habari wa Kimataifa (ICFJ) na
Taasisi ya “Malaria No More” kutoka nchini Marekani walipotembelea Kituo
cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) cha Amani mkoani Tanga
mwishoni mwa wiki kujionea namna Tanzania inavyopambana na ugonjwa huo.
Mfanyakazi
wa Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) cha Amani mkoani
Tanga, Masha Mfinanga akichambua viluwiluwi vya mbu na kuviweka kwenye
kifaa maalum tayari kwa hatua nyingine za utafiti.
Sungura
wanaofugwa katika Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) cha
Amani mkoani Tanga kwa lengo la kuwalisha mbu wanaofanyiwa utafiti,
sungura mmoja ana uwezo wa kulisha mbu 1500.
Baadhi
ya waandishi wa habari kutoka Kituo cha Waandishi wa Habari wa
Kimataifa (ICFJ) na Taasisi ya “Malaria No More” kutoka nchini Marekani
wakimsikiliza Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR)
cha Amani mkoani Tanga Dkt. William Kisinza (hayupo pichani)
walitembelea kituo hicho mwishoni mwa wiki kujionea namna Tanzania
inavyopambana na ugonjwa huo.
Mkuu
wa Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) cha Amani mkoani
Tanga, Dkt. William Kisinza akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa
habari kutoka Kituo cha Waandishi wa Habari wa Kimataifa (ICFJ) na
Taasisi ya “Malaria No More” kutoka nchini Marekani mara baada ya
kutembelea kituo hicho mwishoni mwa wiki kujionea namna Tanzania
inavyopambana na ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment