TTCL

EQUITY

Tuesday, May 17, 2016

Dk. Mengi atoa darasa kwa washiriki wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa


IMELEZWA  jukumu la ulinzi na usalama kwa dunia ya sasa halimo kwenye mikono ya polisi na wanajeshi pekee bali ni la kila mtu katika nafasi aliyopo kama amani na demokrasia inatakiwa kuendelea kuwapo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa, Meja Jenerali Yacoub Mohamed wakati akizungumza na Modewjiblog ofisini kwake baada ya mhadhahara ulioshirikisha wataalamu wa masuala ya habari kutoka sekta binafsi na umma ambao wanachukua kozi ya mbinu za usalama chuoni hapo.
 “Zamani mambo ya usalama yalikuwa ya wanajeshi na Polisi lakini kwasasa mambo ni tofauti, kila mmoja anatakiwa kuhakikisha anakuwa mlinzi ili uwepo usalama wa kutosha kwahiyo tunaamini washiriki wakirudi vituoni kwao watazingatia usalama.
“Wote wanaokuja hapa wanakuwa ni viongozi au viongozi watarajiwa na kama sasa tuna wanafunzi 38, 12 sio Watanzania ni kutoka Kenya, Rwanda, Burundi, Malawi, Namibia, Botswana, Afrika Kusini, Zambia, Nigeria na China,” aliongeza Meja Jenerali Mohamed.
Wataalamu walioendesha mihadhara hiyo ni Mwenyekiti Mtendaji  wa  IPP Ltd, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi ambaye amepata nafasi ya kutoa elimu kuhusu habari kwa sekta binafsi na Mkuu wa Shirika la Utangazaji nchini (TBC) na mwanazuoni Dk. Ayoub Rioba ambaye aliwasilisha sekta ya umma.

Dk. Reginald Mengi saini
Mwenyekiti Mtendaji  wa  IPP Ltd, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi akisaini kitabu cha wageni alipowasili kwenye Chuo cha Ulinzi cha Taifa kilichopo Kunduchi, jijini Dar es Salaam Mei 16, 2016 kwa ajili ya kutoa muhadhara kwa washiriki wa kozi ya mbinu za kiusalama katika chuo hicho.

Akielezea ujio wa Dk. Mengi chuoni hapo, alisema wamekuwa na taratibu wa kukaribisha watu mbalimbali ambao wanawaona wana uwezo wa kuelezea uzoefu wao katika mambo mbalimbali ambayo yanaweza kuwa na faida kwa washirika.
Alisema chuo chao kimekuwa hakina walimu wa kudumu hivyo pamoja na kutumia watu mbalimbali kama walivyofanya kwa Dk. Mengi pia wamekuwa wakiwatumia walimu wa vyuo vikuu ili kutoa elimu ambayo itawasaidia washiriki katika masomo yao ambayo wanayapata chuoni hapo.
“Chuo chetu hakina walimu wa moja kwa moja kwahiyo huwa tunatumia walimu kutoka vyuo vikuu vya hapa nchini lakini pia huwa tunakaribisha watu maarufu wanakuja ku’share’ uwezo wao kwa washiriki ambao wanakuwa wapo masomoni.
“Dk. Mengi ameshafika hapa chuoni mara tatu na sio mtu wa kwanza kuja alishakuja Pius Msekwa, Mawaziri, Katibu Mkuu kiongozi na hata jana tulikuwa na (Dkt. Ayoub) Rioba,” alisema Meja Jenerali Mohamed.

Dk Mengi na Meja Jenerali Yacoub Mohamed
Mwenyekiti  Mtendaji wa  IPP Ltd, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi akisalimiana Mkuu wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa, Meja Jenerali Yacoub Mohamed (kulia) mara baada ya kuwasili chuoni hapo kutoa muhadhara kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika kuhakikisha usalama wa taifa kwa washiriki wa kozi ya mbinu za kiusalama Mei 16, 2016 jijini Dar es Salaam.

Alisema chuo hicho hupokea washiriki ambao ni viongozi katika ofisi wanazofanyia kazi na hupokea washiriki kutoka nchi mbalimbali ambapo hupatiwa elimu kuhusu usalama ili wanapotoka chuoni hapo wakafanye kazi kwa umakini ili wasiweze kuwa sababu ya kupoteza usalama katika maeneo yanayowazunguka.
Katika mada yake iliyozungumza kuhusu wajibu wa vyombo vya habari binafsi katika usalama wa Taifa, Dk. Mengi alisema vyombo visipokuwa makini vikawajibika kitaaluma vinaweza kusababisha migogoro itakayohatarisha usalama wa taifa.
Akielezea uzoefu wake kama mmiliki wa vyombo vya habari binafsi alisema usalama ni jambo la muhimu kwa kila mtu bila kujali ana nafasi gani katika nchi hivyo ni wajibu wa kila mtu kushiriki katika kuimarisha usalama.
Alisema vyombo vya habari wanahakikisha habari zinazotolewa zinakuwa hazina madhara ambayo yanaweza kusababisha upotevu wa amani lakini kusimamia misingi na maadili ya uandishi wa habari.

Brigadia Jenerali Yohana Mabongo
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Ltd, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi (kushoto) akisalimiana na Katibu wa  Chuo cha Ulinzi cha Taifa, Brigadia Jenerali Yohano Mabongo mara baada ya kuwasili chuoni hapo.

 “Kama kuna utulivu, mshikamano na usalama wa taifa kuna faida kwa taifa na hilo linaweza kusaidia kukuza kwa uchumi wa nchi ambao pia utakuwa na faida kwa kila mwananchi,
“Vyombo vya habari vinatakiwa kufuata maadili ya kazi yake kuupasha umma habari na kutoa elimu bila kuathiri hali ya amani na utulivu kwa sababu tunaelewa kuwa pamoja na kutoa habari lakini pia ni wajibu wetu kuhakikisha kuna usalama nchini,” alisema Dk. Mengi.

Yacoub Mohamed NDC
Mkuu wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa, Meja Jenerali Yacoub Mohamed akizungumza machache kabla ya kumkaribisha  Mwenyekiti Mtendaji wa  IPP Ltd ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi (hayupo pichani) kutoa muhadhara kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika kuhakikisha usalama wa taifa kwa washiriki wa kozi ya mbinu za kiusalama chuoni hapo.

Dk. Reginald Mengi 1
Mwenyekiti Mtendaji wa Makapuni ya  IPP Ltd, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi akitoa muhadhara kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika kuhakikisha usalama wa taifa kwa washiriki wa kozi ya mbinu za kiusalama (hawapo pichani) katika Chuo cha Ulinzi cha Taifa kilichopo Kunduchi, jijini Dar es Salaam Mei 16, 2016.



Meja Jenerali Yacoub Mohamed
Mkuu wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa, Meja Jenerali Yacoub Mohamed akitoa historia fupi ya chuo hicho kwa waandishi wa habari (hawapo pichani).

Dk. Reginald Mengi akiaga
Mwenyekiti Mtendaji wa  makampuni ya IPP Ltd, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi akiagana na Mkuu wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa, Meja Jenerali Yacoub Mohamed (kulia) mara baada ya kutoa muhadhara kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika kuhakikisha usalama wa taifa kwa washiriki wa kozi ya mbinu za kiusalama (hawapo pichani) katika chuo hicho kilichopo Kunduchi, jijini Dar es Salaam.
National Defence College
Muonekano wa mbele wa Jengo la Chuo cha Ulinzi cha Taifa  kilichopo Kunduchi, jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment