Na Nathaniel Limu, Singida
Mhasibu  wa Halmashauri ya wilaya ya Singida na mkazi wa Utemini mjini hapa, Imani Abdul Nyamangaro (44), amepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi akikabiliwa na makosa 57 ya wizi wa mishahara hewa yenye jumla ya thamani ya shilingi 29,418,642.
Mapema mwendesha mashitaka wakili wa serikali Michael Lucas Ng’hoboko, alidai mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Joyce Minde, kuwa kati ya Aprili,29 mwaka 2013 na Machi, 27 mwaka 2014, mshitakiwa Nyamangaro  kwa makusudi aliiba mishahara hewa ya zaidi ya shilingi 29.4 milioni huku akijua wazi kitendo hicho ni kinyume na sheria.
Ng’hoboko alisema kuwa mshitakiwa alikuwa akijipatia mishahara hiyo ambayo wahusika waliisha staahafu kazi muda mrefu,kupitia akaunti yake no.50802503513 ya tawi la NMB mjini Singida.
Mshitakiwa Nyamangaro alikana kutenda makosa hayo 57 na kesi yake imeahirishwa hadi Aprili, 27 mwaka huu itakapotajwa tena.
Hakimu wa mahakama hiyo, Minde alisema dhamana ya mshitakiwa ipo wazi na kwamba atapashwa kutoa shilingi 14,709,321. taslimu mahakamani au awe na mali isiyohamishika yenye thamani inayolingana na kiasi hicho cha fedha.
Hadi mwandishi wa habari hizi anaondoka mahakamani hapo, mshitakiwa alikuwa bado hajatekeleza masharti ya dhamana.