Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano Prof. Faustin Kamuzora alifanya
ziara ya kutembelea Shirika la Posta Tanzania ili kufahamu utendaji kazi na
utekelezaji wa majukumu ya Shirika. Katika ziara hiyo Prof. Kamuzora
aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wake Dkt. Maria Sasabo na kufanya mazungumzo
na Menejimenti ya Shirika hilo. Katika ziara hiyo Prof. Kamuzora alimuagiza
Kaimu Posta Masta Kuu wa Shirika la Posta Tanzania Ndugu Fortunatus Kapinga kuhakikisha kuwa ukusanyaji
wa mapato yote ya Shirika la Posta Tanzania (TPC) nchi nzima yanafanyika kwa
kutumia njia ya elektroniki ambapo alisema kuwa, “Shirika liboreshe mifumo yake
ya kielektroniki ili kupunguza mianya ya wizi na upotevu wa fedha za Shirika na
kufanikisha ongezeko la ukusanyaji wa mapato ya Serikali”. Prof. Kamuzora
aliongeza kuwa Shirika la Posta Tanzania liendane na mabadiliko ili liende
kuwahudumia wananchi wa sasa na wa vizazi vijavyo. Shirika ni la kipekee na
lina nafasi nzuri ya kutoa huduma kwa wananchi kama ambavyo Shirika kama hili
linafanya kazi nzuri kwenye nchi ya
China na Brazil.
Aidha, Prof. Kamuzora aliwaagiza
Viongozi wa wasimamizi wa Shirika la Posta Tanzania kutumia Sheria, Kanuni na
taratibu za kuwasimamia wafanyakazi na kuwachukulia hatua kali na za kinidhamu
watumishi wazembe; wasiotimiza majukumu yao; wasio waaminifu na wabadhirifu.
Aliongeza kuwa watendaji wafanye kazi na kusimamia Shirika kwa kuwekeana
malengo kama inavyojulikana kisheria kwa kutumia Mfumo wa wa Wazi wa Upimaji
Utendaji Kazi (OPRAS). Alisisitiza kuwa, “Sheria zilizopo zinatosha
kumsimamisha mtumishi kazi kwa makosa na hatimaye kumfukuza kazi kwa kuwa
watumishi wazembe na wasio waadilifu wanawafanya wananchi wawe na mtazamo hasi
na Serikali yao”. Prof. Kamuzora alisema kuwa wateja wanahitaji huduma nzuri;
ya uhakika na kufikishiwa vifurushi, barua, vipeto na bidhaa nyingine kwa
wakati. Aliwaagiza viongozi wa Shirika kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama
za uendeshaji ili kuendesha Shirika kwa tija na faida. Prof. Kamuzora alisema,
“Uchumi wa nchi hauwezi kukua wala kwenda popote bila kufanya kazi kwa tija.
Alivitaka vyama vya wafanyakazi visiwatetee watumishi wazembe na vishirikiane
na Serikali kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Shirika na watumie mtandao
mpana wa Shirika uliopo nchi nzima na kuangalia fursa zilizopo ili kufikisha
huduma kwa wateja.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
anayeshughulikia Mawasiliano ambaye aliambatana na Katibu Mkuu wake Dkt. Maria
Sasabo aliagiza kuwa, “Shirika lijipange haraka na kuongeza kasi ya utendaji
kazi ya kuwahudumia wateja wake na wananchi ili kuweza kuendana na Serikali ya
Awamu ya Tano ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli”. Dkt. Maria Sasabo aliongeza kuwa Shirika la Posta lipo nchi nyingi
duniani na bado linahitajika hivyo ni muhimu kujipanga kuendana na mahitaji ya
sasa ya wateja na Shirika libadilishe utaratibu wa utendaji kazi na kuondoa
urasimu ili kuweza kuwahudumia wateja. Dkt. Maria Sasabo aliwaagiza viongozi wa
Shirika wafanye tathmini na kuangalia namna bora ya kujiendesha ikiwemo kupitia
upya muundo na majukumu ya Shirika.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
anayeshughulikia Mawasiliano Prof. Kamuzora aliuagiza uongozi wa Shirika la
Posta Tanzania kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa
kuwa na huduma za ziada za kisasa zinazoendana na mahitaji ya wateja kwa
kutumia biashara mtandao kusafirisha na kufanikisha usambazaji wa huduma na
bidhaa za wateja kama vile uagizaji wa magari; vitabu na bidhaa nyingine kwa
kushirikiana na kampuni kubwa duniani kama vile Alibaba, Amazon na eBay.
No comments:
Post a Comment