TTCL

EQUITY

Wednesday, January 13, 2016

Mgogoro mzito waibuka ADC.


Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC) Kumeibuka mgogoro mzito ndani ya Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), baada ya Bodi ya Wadhamini kuisimamisha kamati tendaji ya chama hicho.
Kamati hiyo inajumuisha viongozi wote wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Said Miraaj, huku viongozi hao wakisema hawatambuiuamuzi huo wa bodi. Akizungumza na Nipashe, jijini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya ADC, Kimangale Ayubu Mussa, alisema imeamua kunyang`anya maamlaka ya viongozi hao kwa sababu Katiba ya chama kifungu cha 72 na 73 kinawaruhusu kufanya hivyo baada ya kuona wameshindwa kuwajibika ipasavyo. Alisema moja ya sababu ya kuisimamisha kamati hiyo ni kushindwa kuwajibika katika uchaguzi mkuu uliopita na kusababisha chama kupata matokeo mabaya na kuambulia patupu hata katika viti vya udiwani.
Mussa alisema sababu nyingine ni kamati hiyo ikiongozwa na mwenyekiti wa chama iliandika barua kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ya kutosimamisha mawakala katika uchaguzi huo bila ya kuishirikisha bodi hiyo, jambo ambalo hawakuridhishwa nalo kwa sababu viongozi hao walipaswa kufanya hivyo kutokana na kusimamisha mgombe urais.
Alisema wakati wowote watatangaza uongozi wa muda ambao utafanya kazi mpaka uchunguzi wa kuchagua viongozi wengine utakapofanyika. Alisema Katiba ya chama hicho inaruhuru bodi kuteua viongozi wa muda iwapo waliokuwa wakishikilia nafasi hizo wataondolewa na kwamba uteuzi unatakiwa kufanyika ndani ya kipindi kisichozidi mwezi mmoja. Hata hivyo, alisema uchunguzi juu ya tuhuma zinazowakabili viongozi hao utakapokamilika, kama kuna atakayekutwa hana hatia ataendelea na nafasi yake na watakaokutwa na hatia watawajibishwa.
 
Alitaja nafasi ambazo ziko wazi baada ya viongozi hao kusimamishwa kuwa ni, mwenyekiti wa chama taifa, makamu mwenyekiti, katibu mkuu, naibu katibu mkuu na nafasi zote za wakurugenzi.
Akizungumzia uamuzi huo wa bodi, Miraaj alisema hawatambui uamuzi huo na wao  bado ni viongozi halali kwa sababu haina mamlaka ya kufanya hivyo. 
Alisema juzi walipeleka malalamiko yao kwa msajili wa vyama vya siasa ya kupinga uamuzi huo wa bodi.

No comments:

Post a Comment