Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu maafa
Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali, Mbazi Msuya ameahidi kuwa
serikali itakamilisha kwa haraka ukarabati wa Kituo cha Afya cha Chipole
wilayani Songea Vijijini, ambacho kinashindwa kuhudumia wananchi elfu
7000 wa kata ya Magagura baada ya kupata majanga ya kuungua na moto
mwaka 2013.
Akiongea mara baada ya kukagua shughuli za ukarabati na kujionea
hali halisi ya Kituo hicho Mkurugenzi wa Uratibu Maafa, Brigedia
Jenerali, Mbazi Msuya amesema kuwa ameridhika na matumizi ya fedha za
ukarabati shilingi milioni 35 ambazo zilitolewa na Ofisi hiyo na kuahidi
kutoa fedha nyingine mapema mwezi huu za kukamilisha ukarabati wa kituo
hicho cha Afya.
Kwa upande wake Afisa tabibu wa Kituo hicho,Ismail Mzimya amesema
kukamilika kwa kituo hicho kutaboresha na kuimarisha huduma za Afya
katika kata hiyo hasa za watoto na mama wajawazito huku mmoja wa wakazi
wa kata hiyo akisema kukamilika kwa kituo hicho kutawasidia wakazi hao
ambao wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za Afya na
kuiomba serikali kuharakisha ukarabati wa kituo hicho cha Afya.
Kituo cha Afya cha Chipole kilichopo Kata ya Magagura wilayani
Songea vijijini kinamilikiwa na Shirika la watawa wa Mtakatifu Agnesi
Chipole na kinahudumia takribani wakazi 7,434 wa kata hiyo yenye
vijiji 3, hivyo kukamilika kwa ukarabati wa kituo hicho kutawezesha
wakazi wa kata hiyo kuipata karibu huduma ya Afya.
No comments:
Post a Comment