
Hata hivyo, mapumziko haya yataendelea keshokutwa Jumapili kama ilivyozoeleka.
Tunapenda kuwatakia kila la heri Watanzania wanaposherehekea siku hizi na mapumziko haya.
Kwani ni wakati mzuri wa kutafakari maisha yao ya kila siku na yanayowazunguka.
Tunaomba washerehekee siku hizi kwa utulivu na bila uvunjifu wa amani kwani tangu zilipoanza kusherehekewa sikukuu hizi miaka mingi iliyopita, amani hutawala.
Ni jambo ambalo Watanzania wanapaswa kujifunza kuwa amani siyo ya kuchezea na ndiyo maana utulivu unahitajika wakati wa sikukuu hizi.
Sikukuu hizi za Maulid na Krismasi zinasherehekewa wakati nchi kama Burundi, Iraq, Syria, Afrika ya Kati, Libya na nyinginezo, zikikabiliwa na vita.
Tunaomba viongozi wa dini zote katika kipindi hiki kuhimiza waumini na wafuasi kudumisha amani na udugu.
Pia ni bahati nzuri Jeshi la Polisi limetoa tahadhari kwa wananchi kusherehekea sikukuu hizi kwa utulivu.
Jeshi la Polisi limewaomba wananchi kutoa taarifa moja inapotokea kuwa kuna viashiria vya kuwapo kwa uhalifu.
Yapo mambo mengi hutokea katika kipindi cha sikukuu kama unywaji wa pombe wa kupitiliza.
Wananchi wanapaswa kujihadhari na hali hii kwani kutokana hatari nyingi hutokea zinazosababishwa na ulevi wa kupindukia.
Pia madhara mengi hutokea kutokana na kuwapo kwa mrundikano kwenye kumbi za starehe.
Wananchi pia wanatakiwa kulinda watoto kutokana na ukweli kuwa siku hizo wengi wao hupenda kutoka na kwenda sehemu mbalimbali, mathalani kwenye fukwe za bahari.
Watanzania watumiao magari, pia wanatakiwa kuchukua tahadhari kwa kuendesha wakizingatia sheria za usalama barabarani.
Kutokana na ukweli kwamba kumekuwa na tatizo kwa miaka mingi la kuwapo kwa ajali za barabarani.
Husababishwa na mambo mengi ikiwamo ulevi, lakini pia uendeshaji wa ovyo wa magari ya kubeba abiria.
Tatizo haliko kwa magari tu, hata kwa madereva wa pikipiki maarufu `bodaboda’, ambao baadhi yao huendesha kwa fujo.
Uendeshaji huu wa hatari katika siku za sikukuu, huhusisha kupakia abiria wengi kwa wakati mmoja, mtindo, ambao ni maarufu kwa jina la `mishikaki’.
Tunapongeza pia hatua ya polisi ya kuongeza ulinzi katika kipindi hiki cha sikukuu.
Polisi wamesema wameweka ulinzi mkali katika sehemu za makanisa na misikiti ili kuhakikisha watu wanasali bila matatizo.
Tunaomba wananchi kuwapa ushirikiano polisi katika kipindi cha sikukuu kwa kutoa taarifa pale inapotokea watu wanataka kuleta vurugu.
Hata hivyo, pia sikukuu hizi zitumiwe na Watanzania kutafakari mustakabali wa taifa letu baada ya Uchaguzi Mkuu.
Taifa letu linakabiliwa na changamoto kubwa na hasa katika vita vyake ya kupambana na maadui watatu ujinga, umaskini na maradhi.
Watanzania bila kujali itikadi za kisiasa na kidini, imefika wakati lazima tuunganishe nguvu zetu ili kuhakiksha taifa letu linapiga hatua kubwa kimaendeleo.
Ndiyo maana wakati Watanzania wakisherehekea sikukuu hizi, lakini pia wakumbuke wana dhamana kubwa ya ujenzi wa taifa letu.
Tunapenda kuwatakia kila heri na furaha tele Watanzania wote katika kipindi hiki cha sikukuu.
No comments:
Post a Comment