TTCL

EQUITY

Thursday, December 24, 2015

Uswisi yaahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania

Uswisi imeahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo huku mkazo mkubwa ukiuelekeza katika kuendeleza elimu ya mafunzo ya ufundi stadi.
Balozi wa Uswis nchini Tanzania Mhe. Florence Tinguely Mattl akisaini kitabu.
Balozi wa Uswisi hapa Nchini Mhe.Florence Tinguelly Mattli, amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es salaam.
Balozi Florence amemueleza Rais Magufuli kuwa pamoja na kuwepo kwa miradi mingine ambayo nchi hiyo inaendelea kuitekeleza kwa kushirikiana na Tanzania, katika awamu hii Uswisi itatilia mkazo katika elimu ya ufundi stadi ili kuwawezesha vijana wanaosoma kuwa na ujuzi unaowawezesha kuzalisha bidhaa na kujipatia kipato kama ambavyo nchi ya Uswisi inafanya.
Maeneo mengine ambayo viongozi hao wamezungumzia ni kuimarisha ushirikiano katika uwekezaji, ambapo Rais Magufuli amewaalika wawekezaji kutoka Uswisi kufanya biashara na Tanzania, kuimarisha huduma za bandari na pia kuongeza uwezo katika kukabiliana na vitendo vya Rushwa.
Kuhusu Sekta ya afya, Rais Magufuli ameipongeza Uswisi kwa kushirikiana na Tanzania kupitia Taasisi ya Afya Ifakara katika kukabiliana na changamoto mbali mbali za kiafya ikiwemo kukabiliana na ugonjwa wa Malaria na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuitumia taasisi hiyo ili kusaidia juhudi za kukabiliana na magonjwa.
Wakati Huo Huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Kuwait hapa Nchini Mheshimiwa Jasem Al Najem Ikulu, Jijini Dar es salaam.
Katika Mazungumzo hayo, Balozi Al Najem amewasilisha salamu za mfalme wa Kuwait Mheshimiwa Sabah Al Ahamad Al Jaber al Sabah kwa Rais Magufuli, ambaye amempongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa awamu ya tano na amemhakikishia kuwa Kuwait itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo ikiwemo kufadhili utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta za ujenzi, Maji na Kilimo.
Miongoni mwa miradi hiyo ni mradi wa ujenzi wa barabara ya Chaya - Nyahua yenye urefu wa kilometa 85 kwa kiwango cha lami ambapo Tanzania imeomba ufadhili wa dola milioni 85, Mradi wa Maji wa Same - Mwanga - Korogwe ambapo Tanzania imeomba ufadhili wa dola milioni 20 na Mradi mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji katika bonde la Mhongo na Luhiche Mkoani Kigoma ambapo Kuwait imeonesha nia ya kuufadhili.
Aidha, Rais Magufuli amemshukuru Mfalme wa Kuwait kwa salamu zake za pongezi na amewaalika wafanyabiashara wa Kuwait kushirikiana na Tanzania katika biashara na uwekezaji.
Katika Hatua nyingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Mhe. Louise Mushikiwabo aliyetumwa kuleta ujumbe maalum wa Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Katika Ujumbe huo, Mheshimiwa Kagame amemuhakikishia Rais Magufuli kuwa Rwanda itaendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kijamii hasa ikizingatiwa kuwa licha ya kuwa ni nchi jirani ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rwanda ni marafiki na ndugu wa Tanzania.
Rais Kagame pia amempongeza Rais Magufuli kwa uongozi mzuri aliounesha katika siku za mwanzo za uongozi wake wa awamu ya tano ambao amesema anauunga mkono.
Pamoja na kupokea salamu za Rais Kagame, Rais Magufuli na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda wamezungumzia mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini Burundi na wote kwa pamoja wameona ni muhimu kupata suluhisho kwa njia ya mazungumzo ili wananchi waweze kuishi kwa amani na kuendelea na shughuli zao maendeleo

No comments:

Post a Comment