TTCL

EQUITY

Friday, December 18, 2015

Umekwama na ndoto zako zinafifia? Makala hii inakuhusu!

o-BAD-MOODS-facebook
Mpenzi msomaji wangu, maisha yana changamoto nyingi sana ambazo kamwe huwezi kuzikwepa. Ukikubali changamoto hizo zikuzuie kufikia malengo yako uliyojiwekea, hujipendi na huna tamaa ya kufanikiwa!
Leo nataka kuzungumza na wale ndugu zangu ambao wamejikuta wakikwama katika mambo yao, kufilisika na hatimaye ndoto zao za mafanikio kuyeyuka.
Pia nataka kuzungumza na wale waliokuwa na ndoto zao lakini wameshindwa kuzikamilisha kwa wakati baada ya kupoteza vitu muhimu kama kazi au kufiwa na watu ambao waliwategemea kuwafikisha kwenye vilele vyao vya mafanikio.

barbara-palvin-sad-mood-wallpaper
Mpenzi msomaji wangu, hebu elekeza akili na mawazo yako yote hapa. Naamini leo hutaondoka kama ulivyokuwa kabla ya kuchukua gazeti hili. Tiba ya matatizo ya namna gani unaweza kuanza upya na kufikia tena kilele cha mafanikio, inapatikana kupitia makala haya.
Katika maisha, kuna wakati unapitia hatua mbalimbali za mafanikio. Lakini pia, unaweza ukajikuta umepoteza vitu hivyo vyote na kurudi kama zamani au zaidi. Hayo ndiyo maisha. Hata kama umepoteza kila kitu, kama umebaki na afya yako ikiwa imara, shukuru sana kwani huo ndiyo mtaji na ushindi mkubwa uliobakiza.
Inawezekana kuanza upya. Kuanguka kibiashara siyo mwisho wa maisha. Kupoteza ulichokuwa nacho siyo mwisho wa kila kitu. Tayari imeshatokea, huwezi kubadili. Sawa, umepata hasara, unadhani huo ndiyo mwisho wa maisha yako? Hapana!
Maisha lazima yaendelee na cha msingi hapo ni kukubaliana na matokeo huku ukikaa chini na kutuliza akili. Kama kuna mahali umejikwaa na kuanguka, nyanyuka haraka uendelee na safari.
Kamwe usiendelee kupaangalia mahali ulipojikwaa. Hapakuhusu, achana napo.
Songa mbele na mapambano ya maisha. Kuwa tayari kuanza upya. Ikifika mahali huoni njia, basi itengeneze mwenyewe.
Pia nikukumbushe wewe msomaji wangu  kuwa usiifikirie historia yako ya nyuma. Mafanikio yako hayako nyuma, bali mbele unakoelekea. Achana na historia mbaya ya huko nyuma. Hicho ulichokipoteza, unaweza kukirejesha zaidi ya hicho!
Hayo ndiyo maisha. Kama njia ya kwanza imeshindwa kukufikisha unapotaka kwenda, ni wajibu wako sasa kutengeneza njia nyingine.
Mwanasaikolojia mmoja aliwahi kusema kwamba, kwenye kutafuta mafanikio unapokosa njia, basi tengeneza njia.
Usiruhusu maisha yakuongoze, bali maisha yaongoze wewe. Mwandishi mmoja wa vitabu aitwaye Michael Gian aliwahi kupata ajali mbaya ya ndege. Akapoteza miguu yote na kupooza kuanzia shingoni hadi kiunoni!
Akafilisika baada ya kuingia madeni makubwa wakati wa kutibu majeraha na afya kwa ujumla. Lakini jamaa huyo alianza upya kwa kuwatia watu moyo. Akawa anazungumza akiwa kwenye kiti cha kusukuma cha matairi.
Akihamasisha watu kujikomboa na umaskini. Leo hii ni bilionea na anamiliki viwanda na ndege kadhaa kama usafiri wake binafsi! Hayo ndiyo maisha na mtu huyu akufanye wewe uamini kwamba, ukianguka bado unaweza kusimama na ukafanya mambo makubwa zaidi.
Yaani siyo kusimama tu, unaweza kujikusanyia mali zaidi ya ulizokuwa nazo huko nyuma.
Wakati mwingine Mungu humfilisi mtu kwa makusudi. Pengine ajifunze kuishi maisha ya kuanzia chini kwenda juu.
Hivyo nihitimishe kwa kusema kwamba, huna sababu ya kujiona mnyonge na kuhisi safari yako ya kuelekea kwenye mafanikio imeishia hapo, huo uwe mwanzo wa kupambana na niamini mimi, hakuna linaloshindikana ukiamua kupambana.

No comments:

Post a Comment