Wataalam
wa Uhifadhi wakiongozwa na Dk. Alfred Kikoti (wa kwanza kulia)
wakiendelea na zoezi la uwekaji kola maalum kwa tembo zinazosaidia
kudhibiti mienendo ya tembo ndani nan je ya hifadhi ya Mfumo wa Ikolojia
wa Ruaha Rungwa.
Zoezi la uvalishaji wa kola maalum kwa tembo katika hifadhi ya Ruaha likiendelea.
Helikopta
maalum inayotumiwa na madaktari kwa ajili ya kutambua na kupiga dawa ya
usingizi kwa tembo kabla ya uvalishaji wa kola maalum.
Mkurugenzi
Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi (mwenye kofia) akishuhudia zoezi la
uvalishaji kola maalum kwa tembo katika Hifadhi ya Ruaha.
Daktari
wa Wanyamapori kutoka Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori (TAWIRI)
akijiandaa kumdunga sindano ya kumzindua tembo baada ya kukamilika kwa
zoezi la kumvalisha kola maalum.
Picha
ya pamoja ya wahifadhi walioshiriki zoezi la uzinduzi wa program maalum
ya uvalishaji kola kwa tembo katika Hifadhi ya Ruaha.
Mkurugenzi
Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi (kulia) akiongea na Mwenyekiti wa Klabu ya
Waandishi wa Habari mkoani Iringa wakati wa zoezi la uvalishaji kola kwa
tembo katika Hifadhi ya Ruaha.
(Na Jovina Bujulu-MAELEZO)
Utalii
ni miongoni mwa sekta muhimu zinazoliingizia Taifa pato hasa fedha za
kigeni zinazotolewa na watalii wanaofika nchini kwa shughuli mbali mbali
ikiwemo kuangalia wanyama na vivutio vilivyopo katika hifadhi za taifa.
Sekta
hii ya utalii inakumbana na tatizo kubwa la ujangili ambalo linaripotiwa
kuiingizia taifa hasara kubwa kutokana na idadi kubwa ya wanyama pori
hasa tembo kuuawa kila mwaka.
Hivi
karibuni Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) limezindua programu maalam
ya kuwavalisha tembo kifaa maalumu kijulikanacho kama “kola” au
king’amuzi maalum shingoni mwa tembo hao kinachong’amua na kurekodi
mienendo yao kwa kutumia mawasiliano ya satelaiti.
Program
hiyo inatekelezwa katika mfumo wa ikolojia wa Ruaha Rungwa ambapo tembo
30 wanaoongoza makundi 30 wamevalishwa kola hizo.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa program hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Bwana
Allan Kijazi alisema kuwa inalenga kuimarisha ulinzi wa tembo nchini.
“Lengo kuu la program hii ni kupata taarifa za kina juu ya mienendo ya
tembo katika mfumo wa ikolojia wa Ruaha Rungwe zitakazosaidia kubainisha
maeneo shorobo (njia za wanyama) na mitawanyiko yao kwa ajili ya ulinzi
wa tembo” alisema Bwana Kijazi.
Aliendelea
kusema kuwa teknolojia hiyo inawawezesha kujua mwenendo wa tembo ndani
na nje ya hifadhi, kujua walipo, wanapopita, kasi yao, sehemu
wanazojificha, wanapokunywa maji, ikiwa wamejeruhiwa, wanapopumzika,
maeneo wanayokaa muda mrefu, kama wamekufa, kama wamehama hifadhi moja
hadi nyingine na taarifa nyingine nyingi, hivyo itakuwa rahisi kwa
askari wa wanyamapori kufuatilia usalama wa tembo hao.
Akizungumzia
uanzishwaji wa program hiyo, Bwana Kijazi alisema kuwa inafadhiliwa na
taasisi ya Global Government Facility pamoja na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Maendeleo (UNDP); ambapo UNDP kwa kushirikiana na TANAPA na
SPANET wametoa kandarasi ya kufanya kazi hiyo ya kufunga “kola” kwenye
tembo kwa kituo cha kimataifa cha utafiti wa Tembo “WORLD ELEPHANT
CENTRE “ kilichopo mkoani Arusha.
Bwana
Kijazi aliendelea kusema kuwa, pamoja na shughuli ya kuweka “kola”
kwenye tembo, pia kituo hicho kina jukumu la kuongeza hali ya usalama wa
tembo katika hifadhi za Taifa.
Kwa
upande Mkurugenzi wa Kituo cha World Elephant Centre Dkt. Alfred Kikoti
ambaye pia ni mtafiti wa tembo aliyebobea kwenye sayansi za wanyama hao
alisema kuwa kituo hicho kilianza kazi ya kufunga “kola” kwenye tembo
kuanzia mwaka 2005 ambapo hadi sasa wamekwisha fanya kazi hiyo maeneo ya
ukanda wa kaskazini kuanzia Serengeti, Loliondo, Manyara, na Tarangire.
Maeneo
mengine ni Wami Mbiki mkoani Morogoro, Mashariki mwa Serengeti, Ziwa
Natron, Kilimanjaro Magharibi na Amboseli upande wa Kenya.
Dkt.
Kikoti alisema kuwa sehemu zote walizofanya kazi ya kufunga kola kwenye
tembo, kifaa hicho kinafanya kazi vizuri ya kufuatilia mienendo ya
tembo kwa tija na ufanisi mkubwa.
Akizungumzia
jinsi kifaa hicho kinavyofanya kazi, Dkt Kikoti alisema kuwa, kifaa
hicho kina uzito wa kilogramu 5 ambacho huvalishwa kwenye shingo ya
tembo na kinarekodi mwenendo wa tembo kwa njia ya satelaiti.
“Kituo
kinafuatilia mienendo ya tembo kwa kutumia kompyuta maalum ambazo
zimeunganishwa na kifaa hicho, hivyo tembo wanaonekana kwenye kompyuta
hizo, na kila wanapokwenda na wanachofanya kinarekodiwa.” Alisema Dkt
Kikoti.
Aidha,
Dkt. Kikoti alisema kuwa kifaa hicho kinatumia betri maalum ambayo ina
uwezo wa kukaa kwa miaka 3 hadi 5, kabla ya kuweka betri nyingine.
Alipoulizwa
jinsi namna wanavyowavalisha tembo kola hiyo, Dkt Kikoti alisema kuwa
wanatumia helikopta ambayo inakuwa umbali wa mita 30 hadi 40 kutoka
ardhini kulingana na ukubwa wa pori walipo tembo hao, na kuongeza kuwa
wanachagua tembo mmoja kutoka kwenye kundi la tembo wanayeona anafaa
kufungwa kola hiyo.
“Tembo
anayechaguliwa ni yule ambaye anaonekana ni kijana mwenye umri wa miaka
20 hadi 35, na asiye na mtoto,wala majukumu, hapo daktari wa wanyama
anamchoma sindano kutoka kwenye helikopta ambayo inamfanya alale
usingizi na tembo wengine kwenye kundi wanakimbia kutokana na mlio na
kelele za helikopta na baada ya hapo wanateremka kwenye helikopta na
kumvalisha kola hiyo” alisema Dkt Kikoti.
Aliendelea
kusema tembo huyo baada ya kuzinduka huwafuata tembo wenzake na
waliokuwa naye kwenye kundi na hapo kifaa hicho huanza kuratibu na
kufuatilia mwenendo wa kundi hilo la tembo.
Akizungumzia
kupungua kwa idadi ya tembo katika hifadhi za taifa, Dkt. Kikoti
alisema kuwa kwa sasa hali si nzuri kwani kwa kawaida makundi ya tembo
huwa na tembo 150 hadi 300 lakini kwa sasa makundi yaliyofungwa kola ni
yenye tembo 15 kwa kundi dogo na 300 kwa kundi kubwa.
Katika
kuendeleza jitihada za kulinda tembo, Dkt. Kikoti alisema kuwa kwa sasa
kituo cha World Elephant Centre kinaandaa ujenzi wa kituo kikubwa zaidi
cha kimataifa kitakachoonesha taarifa za tembo dunia nzima ikiwa ni
kumuenzi hayati Mwalimu Nyerere.
Naye
Meneja Mawasiliano wa TANAPA Bwana Paschal Shelulete alisema kuwa zoezi
la kuwafunga kola tembo litasaidia kudhibiti mienendo ya tembo na hivyo
kujua walipo ili kuimarisha ulinzi dhidi ya majangili.
Dkt.
Kikoti alizungumzia mafanikio ya program hiyo kuwa ni pamoja na kutoa
elimu kwa maaskari wa wanyamapori kwani wanaelewa wanyama walipo na
kuimarisha doria sehemu hizo.
Mafanikio
mengine ni idara ya wanyamapori kufahamu mienendo ya tembo na hivyo
kuwaelekeza watalii sehemu ambazo tembo wanakuwepo kwa wakati huo.
Aidha
matumizi ya ardhi yameboreshwa kwani kutokana na satelaiti kola kutoa
taarifa tembo walipo, watu wamefahamu sehemu zinazofaaa kwa wao kuishi
na kuendesha shughuli za kilimo. Pia kutokana na kuwepo kwa ufuatiliaji
wa taarifa za mienendo ya tembo, migongano isiyo ya lazima kati ya tembo
na binadamu imepunguzwa.
Pamoja
na jitihada za serikali za kulinda tembo, wadau mbalimbali wa
wanyamapori wameunga mkono suala hilo kwa kuanzisha kampeni ya “OKOA
TEMBO WA TANZANIA.” ambayo ina lengo la kuhamasisha watanzania kuhifadhi
tembo.
Akizungumzia
sababu za kuanzisha kampeni hiyo, Mratibu wa kampeni hiyo Bwana Shubeti
Mwarabu alisema kuwa walihamasika kutokana na takwimu za sensa ya tembo
zilizotolewa na Taasisi ya Wanyamapori (TAWIRI) inayoonesha kuwa tembo
wamepungua kwa asilimia 60% kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
“Mwaka
2009 idadi ya tembo ilikuwa 109,000 na ilipofika 2014 takwimu hizo
zilionesha tembo wamebaki 43,000 kwa nchi nzima” alisema Bwana Shubeti.
Bwana
Shubeti aliendelea kusema kuwa kampeni hiyo imefanikiwa kutoa elimu
iliyotolewa kwa Umma kwa njia mbalimbali kama vile ushiriki wa maonesho
mbalimbali na matamasha ambapo husambaza vipeperushi vinavyoonesha
madhara ya kuua tembo, kufanya matamasha mbalimbali yenye lengo la
kuzuia kuua tembo.
Programu
ya kufunga kola tembo itaendeshwa kwa miaka mitatu, na inawashirikisha
wadau mbali mbali wakiwemo, World Elephant Centre, TANAPA, Taasisi ya
utafiti wa wanyamapori (TAWIRI), Wizara ya Maliasili na Utalii, Idara ya
wanyamapori, na askari wa hifadhi ya taifa.
No comments:
Post a Comment