TTCL

EQUITY

Wednesday, December 16, 2015

Mfalme wa Afrika Kusini kufungwa jela

Mfalme Buyelekhaya Dalindyebo 
 
Mfalme mmoja wa kabila la Nelson Mandela la Thembu amejipata pabaya baada ya mahakama ya kikatiba nchini kukataa katakata kusikiza ombi la rufaa kufuatia kauli ya mahakama ya juu ya kumhukumu kutumikia kifungo cha miaka 12 gerezani.
Mfalme Buyelekhaya Dalindyebo alipatikana na hatia ya kuteka nyara kuvamia na kuchoma moto makao ya watu.
Ameamrishwa kujiwasilisha kwa kituo chochote cha polisi kilichoko karibu naye katika kipindi cha saa 48.
Chanzo chenye ukaribu na mfalme huyo kimeiambia BBC.
Dalindyebo ndiye mfalme wa kwanza kuhukumiwa jela tangu Afrika Kusini ijipatie uhuru mwaka wa 1994.
Kesi hii inatokana na tukio lililotokea yapata mwongo mmoja uliopita ambapo mfalme Dalindyebo anadaiwa kuwa alimteka nyara mwanamke mmoja na wanawe 6 kisha wakachoma moto nyumba walimokuwa wakiishi.
Yamkini kosa lao lilitokana na mmoja wa jamaa wa mwanamke huyo kukaidi amri ya kufika mbele ya mfalme huyo kujibu mashtaka dhidi yake.
Mahakama ya kikatiba imekataa kusikiza rufaa yake.
Mwandishi wa BBC Pumza Fihlani ambaye yuko Johannesburg anasema kuwa ''Utawala wa mfalme huyo unasemekana kuwa ulikuwa wa kiimla na unalaumiwa kwa mateso mengi yaliyowapata raia maskini katika maeno ya mashambani.''
Utawala wake uliwaudhi wenyeji wengi na huenda asiwe na wafuasi wanaompenda.
Aidha mwanamfalme Azenethi Dalindyebo ameratibiwa kutawazwa kuwa mfalme endapo babake atafungwa jela.
Msemaji wa ikulu Daludumo Mtirara anasema kuwa kauli ya mahakama ya kikatiba kukatalia mbali ombi la kusikizwa kwa rufaa ya kesi hiyo imemnyima uwezo wa kikatiba wa kukata rufaa.

No comments:

Post a Comment