TTCL

EQUITY

Thursday, October 1, 2015

NDOA ZA UTOTONI HADILINI TANZANIA YA LEO?

Katikati ni waziri wa wanawake na watoto serikali ya awamu ya nne Bi. Sophia Simba wakati alipokuwa akitiliana saini ya makubaliano ya upambanaji wa haki za watoto wa kike.
 TANZANIA ina matatizo mengi, namna nyingi ya kuyapitia na kutafuta njia za kuyatatua, lakini pia yanazidiana kutegemeana na nani mwathirika. Wakati wote mtu anayetendewa jambo na kuumizwa huku akiwa hana uwezo wa kuzuia walitendalo, huwa katika wakati mgumu zaidi.
Ni katika msingi huu napenda kuzungumzia suala la ndoa za utotoni. Nchi yetu inakabiliwa na tatizo hili kama zilivyo nyingine, lakini kwa kuwa wema huanzia nyumbani, nasi hatuna budi kuanzia nyumbani kwetu – Tanzania.

Tumeona kwa muda mrefu jitihada za Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kilivyovalia njuga suala la utafiti, kupata matokeo na hata kutafuta suluhu ya tatizo hili.
Kuna maeneo yaliyokithiri kwa tatizo hilo na inasikitisha kwamba katika karne ya sayansi na teknolojia, wapo watu wanaotaka kuharibu maisha ya watoto wao, na si ajabu kizazi chote, maana ule mzunguko wa matatizo ya umasikini, maradhi na ujinga hujisokota.

Watoto wanatakiwa wawe shuleni kwa ajili ya kujipatia elimu na si kuwa nyumbani wakitunza watoto wenzao. Katika zama hizi mpya ambapo elimu ya msingi ni bure, kuna kila sababu kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao, hasa wa kike, wanakuwa madarasani na kupewa fursa za kusoma kwa bidii.
Watoto wa kike wameanza kuonesha mwamko mkubwa wa kutaka kusoma, lakini inasikitisha kwamba wanawekewa vikwazo na wazazi au walezi wao, au kwa upande mwingine wanaume katili wanaotokea na kuwaoa.

Tamwa wanahitaji pongezi kwa kazi kubwa waliyofanya ya tafiti kwa kitambo sasa na katika kudhihirisha hilo, tuliona jinsi walivyopewa tuzo ya CEFM kutokana na uongozi wake imara kuwa na mchango mkubwa katika kupiga vita ndoa za utotoni.
Watoto wa kike wamevumilia machungu ya ndoa za utotoni na za kulazimishwa hivyo wanahitaji mtu wa kuwasemea, mtu ambaye ataelezea taarifa zao zinakazosaidia kuwaweka watu pamoja na kuleta mabadiliko yenye tija.

Nionavyo mimi ni kwamba huu ni wakati mwafaka kutumia majukwaa yote, ya nyumba za ibada, siasa, elimu na kwenye mikusanyiko ya kijamii kukemea tatizo hili kwa nguvu zote.
Takwimu zinaonesha kwamba watoto wa kike milioni 14 duniani huozeshwa kila siku katika umri mdogo chini ya 18, jambo ambalo ni kinyume cha haki za mtoto na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa ndoa za utotoni na mikoa husika ni Shinyanga, Tabora, Mara, Lindi, Mbeya na Morogoro. Ndoa za utotoni huelezwa na wataalamu wa afya kuwa si tu huathiri afya kutokana na miili ya watoto hao kutokuwa tayari, bali pia huleta athari za muda mrefu za kisaikolojia.

Nchini Tanzania wadau wa afya ya uzazi wakiongozwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) wanaelimisha na kuchukua hatua stahiki dhidi ya kitendo hicho. UNFPA walifanya kazi kubwa pia nchini ambapo kwa kushirikiana na Mfuko wa Graca Machel walizindua kampeni ya kupinga ndoa za utotoni nchini Tanzania, kampeni iliyokwenda sambamba na msukumo kwa serikali kubadilisha sheria kandamizi ya ndoa.

Kampeni hiyo ilianzia mkoani Mara, mkoa ulioelezwa kwamba umekithiri kwa ndoa za utotoni, ambapo viongozi wa dini na mila wamekuwa wakihusishwa ili kufanikisha lengo. Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 41 duniani zenye idadi kubwa ya watoto wa kike wanaoozwa katika umri mdogo, ambapo kwa wastani wasichana wawili kati ya watano wameolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18.

Ajabu ni kwamba vitu vinavyotumika kuchochea ndoa hizi haviingii akilini; maana kuna ushuhuda kwamba baadhi ya wazazi walipelekewa majani ya chai na sukari nusu au kilo moja na kukubali kumuoza mtoto.

Wasamaria walitoa taarifa juu ya tatizo hilo na polisi wakaingilia kati, lakini bado tatizo linaendelea, kwa sababu za kisiasa, ambapo sasa inaelezwa kwamba wagombea tangu wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa na sasa uchaguzi mkuu, wanakwepa kushughulikia tatizo wakiogopa kunyimwa kura na jamii zinazounga mkono ndoa za utotoni.

Je, mtoto amefikia ngazi ya kudhalilishwa kwa kuozwa kwa kilo ya sukari; kukatizwa ndoto za kupata maisha mazuri baada ya elimu na kupelekwa kuozeshwa? Naona kwamba hili ni kosa kubwa, sasa baada ya utafiti na kampeni, tuone kwa wingi wote waliohusika wakifikishwa mahakamani na kupewa adhabu kali kwa mujibu wa sheria.

Wadau wanatakiwa kuunga mkono jitihada na misingi iliyowekwa na Tamwa na UNFPA kuhakikisha sasa Tanzania mpya inakwenda kivingine kwenye eneo la huduma kwa watoto, elimu kwa watoto na hili halina shida kwa upande wa watoto.

No comments:

Post a Comment