TTCL

EQUITY

Thursday, April 2, 2015

UZAZI WA MPANGO UNASAIDIA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO


Wazazi wakiwa wodini mara baada ya kujifungua katika zahanati ya Kambarage  manispaa  ya Shinyanga.  huku wengine wakilazimika kuweka magodoro chini kutokana na ufinyu wa  wodi uliopo na kulala wawili wawili kitanda kimoja.
Wazazi wakiwa wodini mara baada ya kujifungua katika zahanati ya Kambarage manispaa ya Shinyanga. huku wengine wakilazimika kuweka magodoro chini kutokana na ufinyu wa wodi uliopo na kulala wawili wawili kitanda kimoja.
UKOSEFU wa elimu ya uzazi wa mpango bado ni changamoto kubwa kwa wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, hali ambayo imekuwa ni chanzo cha wanawake kutotumia njia za uzazi wa mpango na kusababisha vifo vitokanavyo na uzazi.
Mbali na vifo pia idadi ya wasichana wanaobeba mimba katika umri mdogo imekuwa ikiongezeka , licha ya kwamba mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa ambayo iko mstari wa mbele kuhamasisha kampeni ya wanawake kujiunga na uzazi wa mpango, lakini bado juhudi hizo hazijaleta mabadiliko makubwa.
Pamoja na kuwahamasisha wakina mama kuzingatia uzazi wa mpango ili kusaidia kupunguza tatizo hilo pia kuwashirikisha wanaume katika masuala ya uzazi wa mpango, hata hivyo tatizo linaonekana kuendelea kuwepo huku nchi ya Tanzania ikiwa ni moja ya nchi ambazo zina viwango vya juu vya vifo vya wanawake vitokanavyo na matatizo ya uzazi.
Elimu ya uzazi pia inahitajika kutolewa kwa jamii kwa kushirikisha makundi ya vijana ambao ndiyo wako katika kipindi ambacho wanaweza kujiingiza katika mahusiano, matokeo yake wanabeba mimba katika umri mdogo na maisha yao yakawa katika hatari ya kupoteza maisha wakati wakujifungua.

Wataalamu wa afya.
Mtaalamu wa masuala ya uzazi wa mpango mkoani Shinyanga Anna Mwalongo, anasema wasichana wanaobeba mimba chini ya miaka 20 ni tatizo kubwa kwani anaweza kupoteza maisha yeye na mtoto, kutokana na viungo vyake vya mwili havijakomaa kuweza kuhimili mzigo atakao kuwa nao.
Anasema kama watu watabadilika na kuanza kutumia uzazi wa mpango vifo vya watoto wachanga vitapungua kwa asilimia 20, pia vifo vya wakinamama vitokanavyo na matatizo ya uzazi vitapungua kwa asilimia 44,hivyo ni vema wakaelimishwa pia madhara ya kubeba mimba katika umri mkubwa kuanzia miaka 35.
Anabainisha kuwa uzazi wa mpango ni njia nzuri ambayo itasaidia kupunguza vifo vya wakinamama wakati wa kujifungua ,sanjari na kuwawezesha wanawake ambao wanakuwa hawajaamua kupata watoto kujipanga vizuri, pamoja na kuzuia mimba zisizotarajiwa hususani kwa wasichana ambao hawajatimiza miaka 20.
Mwalongo anasema, kila mwaka takwimu zinaonyesha wanawake 454 kati ya 100,000 hufariki , ambapo kati ya watoto 1000 watoto 51 wanafariki kiwango ambacho bado ni kikubwa kinahitaji juhudi zaidi kukabiliana na changamoto hiyo .
Anaeleza kuwa, pamoja na kuhamasisha matumizi ya njia za uzazi wa mpango pia jamii inahitaji kupatiwa elimu juu ya umuhimu wa wakinamama wajawazito kuwahi kwenye vituo vya afya, hatua itakayosaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto na kuchangia kukuza uchumi wa wananchi na taifa.
Naye mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt. Ntuli Kapologwe anasema asilimia 80 ya vifo vinatokana na matatizo ya uzazi, kutokana na wakinamama wajawazito kuchelewa kufika kwenye vituo vya afya pamoja na wasichana kuzaa katika umri mdogo kuanzia miaka 14.
Anasema uzazi wa mpango unasaidia kupunguza vifo vya wajawazito iwapo wanawake watahamasika na jamii kwa ujumla kutumia njia hizo, ambazo zitasaidia kuimarisha afya ya mama na mtoto na kupanga uzazi uliosalama kwa kuwa na afya bora.
Mganga mkuu Dkt Kapologwe anabainisha kuwa, mwaka jana 2014 wakinamama wajawazito 64 walipoteza maisha kutokana na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutojifungulia hospitali, huku wengine wakida wanaona aibu kuzalishwa na wauguzi wenye umri mdogo.

Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga dkt. Ntuli Kapologwe akizungumzia juu ya huduma za uzazi wa mpango katika mkoa huo pamoja mwamko mdogo wa matumizi ya njia hizo.
Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga dkt. Ntuli Kapologwe akizungumzia juu ya huduma za uzazi wa mpango katika mkoa huo pamoja mwamko mdogo wa matumizi ya njia hizo.
Dkt Kapologwe anasema katika uchunguzi waliofanya walibaini kuwa mila na desturi zilizopitwa na wakati zinachangia kuendelea kutokea vifo vya wakinamama wajawazito, kwani takwimu zinaonyesha nusu yao ndiyo wanajifungulia hospitali ama kwenye vituo vya huduma na wengine majumbani au kwa wakunga wajadi.
“Kama wakitumia vizuri njia ya uzazi wa mpango wanaweza kupunguza na kuzuia vifo vya akina mama na watoto kwa asilimia 25,mikakati iliyopo ni kushirikiana na halmashauri zote wakiwemo wadau mbalimbali na kuwa na idadi kubwa ya watumiaji wa uzazi wa mpango ” anasema Kapologwe
Anasema kuwa, asilimia 24 tu ya wanawake wote hutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango, huku asilimia 27 ni kwa wanawake walioolewa na wengine wanatumia njia za asili za uzazi ,ambapo bado changamoto ni kubwa.
Mkoa wa Shinyanga unakadiriwa kuwa na vijana 625,000 ambao wanahitaji kupatiwa elimu ya uzazi wa mpango, wanaoanzia umri wa miaka 15 hadi 19 ni 161963 huku waliowengi wamekwisha olewa na asilimia 33 tayari wana mimba katika umri mdogo.
Mratibu msaidizi wa huduma za afya ya uzazi na mtoto wa wilaya ya kishapu Suzana Kulindwa anabainisha kuwa , idadi kubwa ya wasichana wanabeba mimba kuanzia miaka 14 hadi 19 umri ambao ni mdogo kuweza kuhimili.
Anasema mwaka 2013 wanawake 13,373 walihudhuria kliniki na kati yao 2,562 walikuwa na umri wa chini ya miaka 20 ikiwa ni sawa na asilimia 19.1, ambapo kipindi cha Januari na Juni mwaka jana wanawake 1,370 wenye umri wa chini ya miaka 20 walihudhuria Kliniki sawa na asilimia19.9 wakiwa wajawazito.
Anabainisha kuwa, kuanzia Januari hadi Juni mwaka 2014, kati ya wanawake 6,871 waliohudhuria 1,370 walikuwa na umri wa chini ya miaka 20, hali inayoweza kusababisha kutokea vifo vitokanavyo na uzazi ambapo watu wangetumia njia za uzazi wa mpango changamoto isingekuwepo.
Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa mwaka 2010 na Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) karibu wanawake 20 hufariki kila siku kutokana na matatizo ya uzazi,huku mkoa wa Shinyanga wanawake 64 walipoteza maisha mwaka jana. Kutokana na hali hiyo nchi imejiwekea malengo ya kupunguza kiwango cha vifo kutoka 454 kwa kila wanawake 100,000 hadi 193 ifikapo mwaka 2015.

Wanawake
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya kata ya Bubiki na Itilima ulibaini changamoto kubwa iliyopo ni umbali wa vituo vya kutolea huduma,jambo ambalo linasababisha wanawake wajawazito kujifungulia njiani wakati wakifuata huduma.
Anjelina Yohana (30) mkazi wa kata ya Bubiki anasema wakati wa ujauzito wa mtoto wake wa tatu, alianza kuumwa uchungu na kulazimika kusafiri umbali wa saa moja mpaka kufika huduma ilipo huku akiwa amepakizwa kwenye baiskeli.
“Tulifika kwenye huduma ya afya nikajifungua ila kwa bahati mbaya mtoto alifariki muda mfupi ,wataalamu walisema ni kutokana na kuchelewa kufika kwenye huduma kwa kuwa kituo kilikuwa mbali kisha walirudi nyumbani waliporuhusiwa na daktari”anaeleza.
Anasema kutokana na mkasa huo alioupata anaiomba serikali kuboresha huduma zake kwa kusogeza karibu na jamii zikiwemo njia za uzazi wa mpango,kutokana na wanawake wengi kushindwa kutumia kwa kukosa ushauri, yeye akiwa ni miongoni mwa wanawake ambao hawatumii njia yoyote.
Sara Marco (27) na Paulina Herman (39) kutoka kijiji cha Ikoma kata ya Itilima wanasema umbali wa huduma ni changamoto kubwa, ambayo imekuwa inasababisha na hofu ya maisha yao pindi wanaposhika ujauzito na kuamua kuendelea kutumia njia za uzazi wa mpango ili kuzuia mimba.
Wanasema wanatumia njia za uzazi wa mpango ambazo zimewasaidia kwa kiwango kikubwa katika kuimarisha afya zao, huku tatizo kubwa likiwa ni umbali wa huduma za afya na kusababisha wanawake kujifungulia njiani wakati wakieleka hospitali jambo ambalo ni hatari.
Umefika sasa wakati kwa serikali kuchukua hatua za dharura kukabiliana na changamoto zilizoko vijijini kwa kuboresha huduma za afya na kuwahamasisha wanawake kutumia njia za uzazi wampango,hatua itakayosaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.

No comments:

Post a Comment