TEMBO 60 wameuawa na majangili kwenye hifadhi mbalimbali nchini katika mwezi mmoja tangu operesheni tokomeza isitishwe.
Mauaji hayo yametajwa kufanyika katika Hifadhi za Selous, Rungwa, Burigi, Katavi na Ngorongoro.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema jana kwamba idadi hiyo ni sawa na wastani wa tembo wawili kila siku, inakwenda sanjari na kuuawa, kujeruhiwa kwa watumishi kadhaa wanaofanya kazi kwenye hifadhi.
Alisema hayo Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu namna serikali ilivyojipanga kuhakikisha inatokomeza vitendo vya ujangili.
Alitaja askari wa wanyamapori, Ramadhani Magengere (40) aliuawa na majangili na wakati huo huo, Yahya Ramadhani (34) alijeruhiwa na wafugaji walioingiza mifugo ndani ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Jumuiyan(WMA) Ukutu iliyoko Morogoro Vijijini. Matukio hayo ni ya Desemba 6 mwaka huu.
Aidha alisema Novemba 14, mtumishi wa wanyamapori, Sajid Majidi alijeruhiwa kwa kuchomwa mkuki kichwani na kuvunjwa mkono na wafugaji walioingiza ng’ombe katika eneo la Ramsar, Kilombero.
Alisema wapo watumishi wa pori la akiba Mkungunero wilayani Kondoa, Dodoma, waliokuwa doria walivamiwa na kundi la watu zaidi ya 80 waliokuwa na mikuki na silaha nyingine za jadi na kujeruhiwa.
“Kutokana na kusitishwa kwa operesheni tokomeza, matukio ya uvunjaji wa sheria za hifadhi kama vile uingizaji holela wa mifugo katika maeneo ya hifadhi, ujangili wa wanyama wakiwemo tembo pamoja na uvunaji wa miti katika hifadhi za misitu, bado yanaendelea,” alisema.
Nyalandu ambaye kwa mujibu wake, vitendo vya ujangili vimeongezeka baada ya operesheni hiyo ikilinganishwa na kipindi cha opeseheni, alisema wakati wote wa operesheni tokomeza iliyodumu kwa mwezi mmoja, ni tembo wawili waliokuwa wameuawa.
Aliendelea kusema, “Majangili wameua tembo 60 katika hifadhi na mapori ya Selous, Rungwa, Burigi, Katavi na Ngorongoro…..hawa ni takribani tembo wawili kwa siku na ikumbukwe wakati wote wa operesheni tokomeza iliyodumu mwezi mmoja ni tembo wawili tu waliokuwa wameuawa,” alisema Nyalandu.
Naibu Waziri alisema serikali imegundua kambi ya majangili iliyoanzishwa katika pori la akiba la Burigi ambako vitendo vya ujangili vinaendeshwa na baada ya kukurupushwa na askari wa wanyamapori walikimbia na kuacha nyama ya nyani 30 waliokuwa wamewaua.
Aidha alisema hivi karibuni, wilayani Simanjiro, lilikamatwa gari likiwa limejaa mizoga 20 ya swala. Alisema lipo ongezeko la wimbi la uvamizi na ufugaji wa mifugo ndani ya mapori ya akiba, hifadhi za misitu iliyoko Magharibi mwa nchi hususani Burigi, Biharamulo, Kimisi, Moyowosi, Katavi na Ugalla.
“Serikali inawakumbusha wananchi kuwa kwa mujibu wa sheria ya wanyamapori namba 5 mwaka 2009 pamoja na sheria zinazosimamia maeneo ya hifadhi za taifa na misitu kuwa hawaruhusiwi kuingiza mifugo wala kuingia kuua, kuwinda, kukamata wanyama bila kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori,” alisisitiza.
Wakati operesheni tokomeza imegeuka kuwa mwiba baada ya wabunge kuibua kashfa ya unyanyasaji na utesaji uliofanywa na wananchi hivyo kusababisha mawaziri kadhaa kujiuzulu, Nyalandu alisema matukio hayo ya bungeni Dodoma, hayajatengua sheria yoyote ya Wanyamapori au Misitu.
Aliwaagiza watumishi wa Wizara hiyo kuendelea kutekeleza majukumu yao ya ulinzi wa maeneo ya hifadhi za taifa, mapori ya akiba na misitu ya hifadhi bila kutetereka.
Alitaka wachukue hatua stahiki dhidi ya mhalifu yeyote ilimradi wanazingatia sheria. “Ikumbukwe kuwa matukio yaliyotokea bungeni Dodoma, hayajatengua sheria yoyote…hamna maamuzi yoyote ya Bunge yaliyohalalisha ukiukwaji wa Sheria za Uhifadhi,” alisema Nyalandu.Alisisitiza kwamba wananchi wanatakiwa kutii na kufuata sheria hizo kama zilivyo.
“Tahadhari inatolewa kuwa Serikali haitasita kumchukulia hatua kali yeyote atakayekiuka Sheria ya Wanyamapori kwa makusudi. Tunawaomba wananchi wasikubali kudanganywa na mtu yeyote kuvunja sheria za nchi,” alisema. “Serikali inasisitiza kuwa kwa kutumia vyombo vyake itaendelea kutimiza majukumu yake ya kusimamia ipasavyo sheria, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayeshiriki moja kwa moja au kusaidia vitendo vya ujangili ili kunusuru rasilimali za taifa,” alisisitiza.
Katika mkutano huo wa jana, Naibu Waziri asisitiza serikali ina maadili na miiko ya utendaji kazi kwa watumishi wake wakiwemo askari wa wanyamapori.
Alisema serikali itaendelea kuwakumbusha watumishi maadili na miiko kila wakati kupitia mafunzo na mbinu nyingine.
Kujiuzulu mawaziri Operesheni Tokomeza ilisitishwa Novemba mosi kabla ya wabunge kuibua kashfa ya unyanyasaji na utesaji unaodaiwa kufanywa na waliokuwa wakiiendesha na hivyo kusababisha mawaziri wanne kuachia nyadhifa zao.
Ripoti ya kamati ndogo ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyoundwa kuchunguza operesheni hiyo, ilieleza kuwa athari zilizotokana na operesheni hiyo zilisababishwa na wizara nne zilizokuwa zikiongozwa na mawaziri hao.
Mawaziri walioachia nyadhifa zao ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki aliyejiuzulu na wengine wanne ambao kwa pamoja, Rais Jakaya Kikwete alitengua nafasi zao.
Wengine ambao uteuzi wao ulitenguliwa ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
No comments:
Post a Comment