TTCL

EQUITY

Thursday, November 6, 2014

Hili la kupigwa Warioba ni ishara mbaya nchini



Kwa aina hii ya siasa inayoendelea nchini, ni wazi kwamba tunaiharibu demokrasia yetu.
Hakuna ubishi kwamba Tanzania inaelekea kubaya tena pabaya sana. Hali iliyojitokeza Jumapili kwenye Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Dar- es – Salaam na yaliyomkuta kiongozi mahiri katika historia ya nchi hii, Jaji Joseph Warioba ina viashiria vya siasa za ufedhuli na unduli huko tunakoelekea.

Ilikuwa katika mdahalo wa kujadili Katiba Inayopendekezwa ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, ulivunjika baada ya kutokea vurugu. Habari zinadai kuwa mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, pamoja na mambo mengine, alipigwa.

Tukio hili bila shaka limetia aibu kubwa mfumo mzima wa demokrasia nchini kwa sababu mbalimbali, watu wakubali au wakatae jambo kutokana na ubora wa hoja na siyo mabavu. Huo ndiyo msingi mkuu wa demokrasia ya kweli popote duniani.

Baada ya tukio hilo la aibu sana, Watanzania tujiulize kama tunajenga demokrasia ya kweli au tunajenga domokrasia, ufedhuli na uduli ili uje kutudhuru huko tuendako?

Katiba mpya au ya zamani iliyokarabatiwa siyo hoja kama misingi ya demokrasia iliyomo au itakayokuwamo katika Katiba hiyo haitaheshimiwa.

Maana katiba hiyo lazima isimame kwenye misingi ya demokrasia hiyo hiyo, la sivyo siku za kuishi Katiba hiyo si nyingi, itaporomoka tu!

Mtindo wa kuruhusu mabavu kutumika kuua hoja ni hatari sana katika ujenzi wa demokrasia. Kama huelewi hilo, waulize ndugu zetu Wajerumani. Hizo ndizo mbinu zilizotumiwa na Adolf Hitler na chama chake cha Nationalist (maarufu zaidi katika historia kwa jina la Nazi) kushinda uchaguzi wa Ujerumani 1939.

Maafa na mateso yaliyofuata kwa dunia na hasa Ujerumani wenyewe baada ya ‘ushindi’ wa Hitler. Hili siyo siri kwa yeyote aliyekwenda shule.

Mengi yamesemwa na mengi zaida yatasemwa kuhusu mambo ya aibu yaliyotokea Hoteli ya Blue Pearl, lakini jambo moja ni dhahiri palitokea ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ambayo lazima yachukuliwe hatua na vyombo husika.

Picha za kamera/video zinaoyesha na mashahidi waliokuwapo wanadai kada wa CCM, Paul Makonda alihusika kwa njia moja au nyinbgine kwenye vurugu hizo dhidi ya Jaji Joseph Warioba, mtu mwenye utumishi wa kutukuka kwa Taifa, mwenye umri mkubwa.

Wapenda haki tunauliza; Je? Hili nalo lenye ushahidi wa wazi litawekewa mizengwe na vyombo husika kama lile la kutekwa na kuteswa vibaya kwa aliyekuwa kiongozi wa chama cha madaktari nchini, Dk Stephen Ulimboka?

Kuna msemo wa wahenga usemao, ukilea mtoto wa chui siku moja atakua chui kweli na mwingine usemao hata mbuyu ulianza kama mchicha!
Ninachotaka kusisitiza ni kwamba tunahitaji kuona nchi yetu ikiendelea kuwa na amani milele. Kwa maana hiyo kila aina ya fujo inapoanzishwa inapaswa kuchukuliwa hatua thabiti.

Kama hili ambalo limetokea Ubungo halipaswi kamwe kuachwa likapita hivi hivi, badala yake vyombo vya sheria vifanye kazi zake.

Ingawa Makonda mwenyewe anasema kwamba hajampiga Warioba, nashauri kwamba ni vizuri kuwepo ufuatiliaji na hatua thabiti kuchukuliwa ili kuwajengea Watanzania tamaa ya kuipenda haki badala ya kutumia nguvu.

Tunapokuwa na utulivu wa kisiasa ndipo maendeleo mengine yakiwamo ya kiuchumi yanavyoweza kupatikana kwa haraka. Ndio nasema kwamba tunapaswa kutoichezea amani yetu, wala hatupaswi kuacha vizazi vyetu kutulaumu kwamba tumechangia kuliingiza taifa katika shida ya ukosefu wa amani.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya kijamii.

No comments:

Post a Comment