TTCL

EQUITY

Monday, October 27, 2014

VIGODORO, MUZIKI, MAHUBIRI VYAWATESA WATANZANIA

Vigodoro, muziki, mahubiri vyawatesa Watanzania (hasa jijini Dar)!

- Magari ya matangazo yanapita mitaani huku yakipiga muziki mzito bila kujali athari wapatayo raia
- Madhehebu ya kidini yanafanya mikutano yao ya injili & mihadhara katika maeneo ya wazi na kupiga muziki kwa sauti ya juu

Endelea kusoma zaidi ==> http://goo.gl/PhygH2Kwa ufupi

Kelele ni moja ya mambo yanayosababisha uchafuzi wa mazingira.
Wakati mwingine kelele husababisha mitetemo ambayo huleta bugudha kwa watu waishio au walio jirani na eneo husika.

Nchi nyingi duniani zimekuwa zikifanya jitihada kukabiliana na changamoto mbalimbali za uchafuzi wa mazingira. Mikataba na itifaki mbalimbali imesainiwa ili kuunganisha nguvu katika kukabiliana na changamoto hizo.

Kelele ni moja ya mambo yanayosababisha uchafuzi wa mazingira. Wakati mwingine kelele husababisha mitetemo ambayo huleta bugudha kwa watu waishio au walio jirani na eneo husika.

Jiji la Dar es Salaam linakumbwa na kadhia hii kutokana na shughuli mbalimbali zinazofanyika. Magari ya matangazo yanapita mitaani huku yakipiga muziki mzito bila kujali athari zake. Mengine husimama katika maeneno yenye mkusanyiko mkubwa wa watu na kufanya burudani wakati wakitangaza bidhaa zao.

Baadhi ya viwanda vimejengwa kwenye makazi ya watu. Mbali na kutoa moshi na kutiririsha maji machafu, viwanda hivi vinatoa sauti na muungurumo mkubwa ambao unasababisha adha kwa wakazi wa sehemu hiyo.
Madhehebu ya kidini yanafanya mikutano yao ya injili na mihadhara katika maeneo ya wazi na kupiga muziki kwa sauti ya juu. Nyumba nyingi za ibada zimejengwa katikati ya makazi ya watu, jambo linalosababisha kero kwa watu kwa kuwa baadhi yao hufanya shughuli zao kwa zaidi ya siku tatu za wiki.

Mipango miji mibaya inaelezwa kuwa chanzo cha kelele. Katika nchi nyingi zinazoendelea watu wengi wanaishi kwenye nyumba ndogo na nyumba hizo pia zimejengwa kiholela bila ya kuachiana nafasi. Hii inasababisha maeneo hayo kuwa na mizozo na migogoro ya mara kwa mara.

Pia, watu wengi sasa wanamiliki magari. Magari huongeza kiwango cha kelele ambacho hakitakiwi. Makazi mengine yamejengwa karibu na viwanja vya ndege, jambo linalowafanya wawe karibu na kelele kubwa za ndege wakati zinapotua au kupaa.

Mkurugenzi wa kampuni ya maendeleo ya makazi ya Space and Development, Renny Chiwa anasema ujenzi holela hautakiwi kisheria na kuongeza kuwa Sheria ya Mipangomiji ya mwaka 1956, na maboresho yake ya 1997 imepanga madaraja ya matumizi ya ardhi ambayo kwa mfano, kuanzia A na B ni eneo la makazi, K shule, N na M maeno ya viwanda ambayo hayachangamani na makazi.

“Makanisa, misikiti, klabu za pombe ni taasisi ambazo hazitakiwi kuwa mbali sana na makazi wala kuwa katikati ya makazi, bali zifikike kirahisi. Lakini kwa sasa tunaona baadhi ya makanisa na klabu za pombe zikikimbilia katika maeneo ya makazi na yasiyopimwa,” anasema Chiwa.
Mtaalamu huyo anasema yapo maeneo ya biashara pekee na yale yenye mchanganyiko na makazi. Lile lenye mchanganyiko wa makazi na biashara huwa na hoteli zisizopiga muziki kwa sauti kubwa wakati eneo la biashara huwekwa pembezoni mwa mtaa kwa ajili ya huduma na hapa ndipo masoko na vilabu vya pombe hupatikana.

Sanjari na kuongezeka kwa idadi ya taasisi zinazopiga muziki kwa kiasi kikubwa na katikati ya maeneo ya makazi ya watu, mengine yakijengwa kinyume na sheria, ipo pia burudani mpya maarufu kama vigodoro.

Vigodoro vinazidi kuongezeka kila uchwao katika maeneo mengi ya ‘uswahilini’ ambapo wakazi wake hujikuta wakivumilia shida zitokanazo na furaha za wengine ambao hukesha wakicheza ngoma na muziki usiku kucha.

Tayari jeshi la polisi lilishapiga marufuku, lakini bado vinaendelea kwa mitindo tofauti tofauti kutokana na hadhi ya eneo husika.

Kama hiyo haitoshi, baadhi ya wakazi wa jiji hili wenye sherehe zao huzunguka mitaani na kuonyesha mbwembe za kuning’inia juu ya magari yenye muziki mkubwa huku wakikata viuno.

Katika utafiti wa kelele katika hoteli na migahawa mkoani Morogoro uliochapishwa Desemba, 2009 katika jarida la Sayansi na Usimamizi wa Mazingira (Jasem), Dafrozah Samagwa na wenzake wa Chuo Kikuu cha Sokoine, walibaini kuwa asilimia kubwa ya hoteli zilikuwa zinapiga muziki kwa kiwango kikubwa kati ya 61 dBA hadi 64dBA. dBA ni kipimo cha kisayansi cha ukubwa wa sauti.
Kwa mujibu wa utafiti huo ulioitwa Uchunguzi wa Upigaji Kelele katika Migahawa ya Manispaa ya Morogoro, sauti zilizopimwa kutoka ndani ya migahawa hiyo zilizidi kiwango kinachotakiwa na Shirika la Viwango nchini (TBS) cha sauti isiyozidi 55dBA katika eneo lenye mchanganyiko na makazi.

Pamoja na vurugu zote hizo za kelele, bado mamlaka husika zinatajwa na baadhi ya wadau kuwa hazijachukua hatua yoyote. Halmashauri ambazo hutoa leseni za shughuli mbalimbali zinatuhumiwa kulegalega kiasi cha kuacha tatizo liendelee.
“Hapa tumezungukwa na makanisa matatu; moja kubwa na mengine madogo… yote haya hupiga muziki kiasi cha kufanya mazingira haya kuwa magumu sana kuishi,” anasema Dotto Magoma, mkazi wa Tabata Segerea.
“Wenzetu mitaa ya Kisukuru tumesikia waliokuwa wanapiga kelele wametimuliwa, lakini kwetu hali bado ngumu.”

Anasema kuwa baada ya hali hiyo kuzidi na taasisi hizo kupiga muziki na mapambio usiku kucha kuanzia Ijumaa hadi Jumapili, ilibidi wakazi wa mtaa waombe kufanya kikao na balozi wao ili wajadili namna ya kuzungumza na viongozi wa makanisa husika.

Athari za kelele kwa binadamu
Jarida la Oxford la Uingereza linaeleza kuwa kuishi kwa muda mrefu katika eneo lenye kelele kufikia kiwango cha 85 – 90 dBA kunaweza kumfanya mtu kuwa na usikivu hafifu au kuwa kiziwi kabisa.

Oxford limefafanua kuwa kiwango hicho cha kelele kinaweza kusababisha magonjwa mbalimbali ya moyo (cadiovascular) kama vile shinikizo la damu, mfadhaiko wa moyo (hypertension) na msongo wa mawazo.

Pia, imebainika kuwa kiwango kikubwa cha kelele kinasababisha kutopata usingizi usiku. Inaelezwa kuwa kulala katika eneo lenye kelele kunamfanya mtu asilale kwa muda mrefu, kuwa na hasira muda mwingi na kuathiri ukuaji wa watoto.

Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa katika miji ya London na Los Angeles, kuna uhusiano mkubwa kati ya sauti kubwa zinazosababishwa na milio ya ndege na matatizo ya kisaikolojia na akili.

Jarida hili linafafanua kuwa baadhi ya watu wanakuwa na hasira, wengine kujawa na hofu kulingana na aina ya kelele inayozalishwa. Linaeleza kuwa matatizo yote haya ya kisaikoljia yanajitokeza kama mtu atakaa kwa muda mrefu eneo lenye sauti zilizopitiliza kipimo.


Mamlaka zafafanua
Ofisa uhusiano wa manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhowela anasema sheria za kudhibiti kelele zipo katika ngazi ya halmashauri za manispaa, lakini utekelezaji wake unabaki kuwa katika ngazi ya serikali ya mtaa husika.

Anasema serikali ya mtaa au kijiji ina jukumu la kusimamia udhibiti wa kelele ambazo zitaonekana kuwa kero miongoni mwa wanajamii.
Anafafanua kuwa, kama mtu hajafurahishwa na kelele hizo anatakiwa kupeleka taarifa serikali ya mtaa huo ili ichukue hatua stahiki.
“Hili ni jambo dogo, tumekasimu madaraka kwa serikali za mitaa ili ziweze kusimamia utekelezaji wake. Viongozi wa mitaa walione hili kama tatizo na kuchukua hatua linapojitokeza,” alisema.

Hata hivyo, Mhowela anabainisha adhabu kwa kuvunja sheria hiyo ni faini ya Sh50,000.

Ofisa huyo anasisitiza wananchi kutambua haki na wajibu wao kwa kuzifahamu sheria ndogondogo zinazosimamiwa na halmashauri zao. Hatua hii inaweza kuchukuliwa endapo mwananchi atashiriki kwa kutoa taarifa.
“Tatizo hili tumelizungumzia sana, nadhani sasa wananchi watakuwa na utashi wa kuchukua hatua. Si jambo la kutoa matangazo tu, pia yapo madhehebu yanayoendesha mikutano yao katikati ya makazi ya watu kwa sauti ya juu sana. Nao wanadhibitiwa kwa sheria hiyo hiyo,”

Anabainisha kuwa manispaa pekee ndiyo hutoa vibali vya kufanya matangazo na katika vibali hivyo wanapewa masharti ya kupiga kwa sauti ya kawaida.
Naye ofisa habari wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu anasema ofisi yake hufanya ukaguzi mara kwa mara na kwamba wale ambao hubainika, huchukuliwa hatua za kisheria.

“Wakati wa kuomba na kupatiwa leseni kuna masharti kabisa mmliki wa klabu ya pombe au hoteli hutakiwa kuyafuata. Baadhi ya masharti hayo ni muda wa kufungua na kufunga pamoja na kiwango cha sauti ya muziki unaotakiwa,” anabainisha Shaibu.

Mwishoni mwa juma lililopita, mkurugenzi wa utekelezaji na uzingatiaji wa Nemc, Dk Robert Ntakamulenga alinukuliwa na The Citizen, gazeti dada la Mwananchi, akikiri kuwa ofisi yake inakosa sheria za kuwadhibiti wapiga kelele licha ya kuwepo malalamiko lukuki.
“Tunapokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya hili na baadaye hutembelea eneo husika na kuamuru kusitisha upigaji kelele uliopitiliza, hata hivyo mbinu hii haijaweza kutokomeza tatizo,” anasema Dk Ntakamulenga.
Hivyo, udhibiti wa kelele katika maeneo ya makazi ni jukumu la wananchi kwa kushirikiana na Serikali za mitaa. Wananchi washiriki kwa kutoa taarifa pale wanapokumbana na adha hizo na Serikali za mitaa zisimamie sheria zilizopo.

No comments:

Post a Comment