TTCL

EQUITY

Sunday, September 29, 2013

Salma Moshi: Mtanzania mchakarikaji Marekani

UNAMKUMBUKA Salma Moshi? Yule mwanamama aliyevuma DDC Kibisa akiwa na kikundi chake cha maonyesho ya sanaa cha Ujamaa Theatre Troupe?  Ni kweli amepotea nchini lakini anafanya mengi Marekani sasa akiwa kada wa CCM na Mtanzania. Raia Tanzania ilimtafuta na kufanya mahojiano naye kwa njia ya simu akiwa huko na yafuatayo ndiyo yaliyojiri: 

Paparazi:  Uliondoka nchini lini na kwa madhumuni gani?
Salma: Niliondoka nchini mwaka 2003 kwa mwaliko wa kushiriki kwenye tamasha. Wakati huo  nilipata mialiko miwili. Wa Ufaransa na Marekani. 

Paparazi:  Ehee, baada ya tamasha nini kiliendelea? 
Salma: Baada ya tamasha ambalo lilifanyika Miami Florida hapo tukaweza connection (kuunganisha) nyingine mbazo ziko Washington DC, kwa hivyo tukaja Washington DC. 

Paparazi: Safi, sasa unaishije huko?
Salma: Naishi kama kawaida sasa. Mwanzoni inakupa shida hasa kuhusu kwenda nyumbani na kurudi na kuhusu kazi lakini ukishakamilisha inakuwa vizuri zaidi duniani kote ndiyo maana nataraji kuja nyumbani hivi karibuni. 

Paparazi:  Hivi sasa unajishughulisha na nini?  Ni sanaa au…..?
Salma: Naipenda sana siasa.  Napenda kuwa mwanasiasa kuwatumikia watu, kazi ya utumishi. Nipo katika Chama cha Mapinduzi ni katibu mwenezi na pia huwa nafanya sanaa ingawa mara nyingine inakuwa taabu.  Wengi huku wanakwambia wanaona haya kucheza sanaa, nawashawishi nawapata lakini inakuwa sio mara zote, ni tofauti na nyumbani. Pia nafanya kazi za kawaida kujikimu katika maisha ya kila siku. 

Raia Tanzania:  Sanaa za maoyesho Tanzania ni kama zinakufa.  Hakuna tena vikundi kama vya DDC Kibisa ulichowaji kukiongoza wala Ujamaa Theatre Troup ulichowahi kukimiliki.  Muda si mrefu tumefiwa na Mzee Small Said Ngamba na Salum Tambalizeni.  Ukiombwa leo kufufua sanaa za maonyesho kwa kuanzisha kikundi cha taifa na ukahakikishiwa kuungwa mkono na Serikali utakubali kurudi?
Salma: Mimi sanaa iko kwenye damu. Ninapatwa na uchungu  kuona sanaa za maonyesho zinapotea wakati wasanii ndio tumetumika tokea enzi za uhuru.  Nikimbukumba  Mzee Mwinamila, Mzee Mayagilo, Mzee Morris na wengi wazee wetu. Nikikumbuka wakati tunashindana na John Komba akipiga DDC Kondoa napiga DDC Kariakoo na kumbi zinajaa. Si kweli kwamba watu hawapendi sanaa hata kidogo naamini sanaa ikifanyika kikamilifu watu watakuja tu. Mashirika mengi yameacha kudhamini kama Bima na majeshi. Vikundi havina msisimko.  Napenda vizuri kumzungumzia Tambalizeni. Nilichangia kwa kiasi kikubwa kukuza kipaji chake. Nilimuona Manzese, nikasikiliza ngonjera yake nikamchukua mwaka 1983.
Nikamfanyia mpango RTD alikuwa anatoka kila siku watu wakampenda , akaenda kusoma Kivukoni. Alizunguka na Rais Mkapa Tanzania nzima wakati wa kampeni.  Niko  tayari kuja kuanzisha kikundi cha taifa. Ninapinga vikali  sherehe zote zinazofanyika bila kuashirikisha wasanii  wa sanaa za maonyesho. Mashirika na serikali kila mara wamekuwa wanaalika Bongo Fleva au taarab. Hata siku moja  hawajawahi kuchukua vikundi vya ngoma ambavyo ndivyo vinaonyesha utamaduni wetu. Matamasha yapo lakini kwetu sisi  hawapelekwi walengwa, unaona vikundi kutoka Zimbabwe, Afrika Kusini, Burundi wanazitumia nafasi hizo.  Wasanii wetu wamekuwa masikini wanatumwa tu uwanja wa ndege na sehemu ambazo hazina kipato. 

Raia Tanzania: Nini maoni yako kuhusu utaratibu wa Serikali kama tulivyoona hivi karibuni kwa Waziri wa maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kumpeleka mwigizaji wa filamu Aunty Ezekiel kwenda kutangaza Utalii Marekani badala ya wasanii wa sanaa za maonyesho?
Salma: Kusema kweli katika suala la utalii au sherehe za uhuru, watu wa nje watapenda kuja kuona utamaduni wetu halisi na kuutangaza na siyo kuona watu kama Naomi Campbell ambao wako wengi kwao. Nilitarajia vikundi vya sanaa kutumika kwa lengo la kuutangaza utalii na vivutio vya utalii ni ngoma za asili siyo kuja kumuona mtu kama Naomi Campbell ambaye kwa utalii wa kwetu hana nafasi. 

Raia Tanzania: Bado unaonyesha sanaa ya kucheza na nyoka huko Marekani? 

Salma: Huku si sana. Nyoka waliopo huku si wakubwa, ni wadogo. Mazingira ya kuwaweka na masharti kuhusu wanyama ni mambo yanayonifanya nifanye sanaa hiyo mara chache sana. Sanaa zingine kama maigizo na ngoma nazipenda sana. Nilicheza siku moja  wazungu wakaniambia mimi ni msanii halisi, walifurahi sana. 

Raia Tanzania:  Hivi ukikaa na kuwaza, huoni kwamba ulipata bahati ya mtende  kwenda huko Marekani? Sanaa za maonyesho zilivyodorora sasa maisha yako yangekuwaje?
Salma: Nashukuru sana kupata bahati ya kuja huku. Kutoka nje kumenisaidia sana kujua tamaduni za wenzetu na kujifunza mengi kuhusu sanaa. Najua sasa ni kwanini wasanii wa nje wanakuwa matajiri. Ukweli ni kwamba wanajituma na kuwapo kwa hakimiliki kunawasaidia.  Wanakuwa makini mno na shughuli zao kwa kuwa na mameneja wa uhakika na wanasheria.  Naamini ningekuwa Tanzania ningekuwa mbali zaidi katika sanaa kwa sababu ningejituma kupambana na hali iliyoko.  

Raia Tanzania: Unawashauri nini vijana wenye damu ya kisanii katika sanaa za maonyesho hapa nchini. Je, watafute shughuli nyingine za kufanya au kuna matumaini ya sanaa za maonyesho kufufuka na kuwa kama zamani?
Salma: matumaini yapo, tena kwa sanaa kama ngoma ni rahisi sana. Matamasha mengi yapo. Wapewe wakashiriki wakajifunze na kuongeza kipato. Serikali kupitia BASATA (Baraza la Sanaa la Taifa) lisaidie kuhamasisha mashirika na watu binafsi kuinua sanaa. Kuna kipindi Tanzania Breweries ilidhamini wasanii kutangaza kampuni. 

Raia Tanzania: Unajisikiaje unapowaona wasanii kama wa Botswana wanapocheza makhirikhiri na kutamba kimataifa na huku nyumbani Tanzania hakuna kikundi au ngoma yoyote kati ya makabila zaidi ya 120 inayofua dafu wakati zipo nyingi zinazovutia kama Sindimba na Lizombe?
Salma: Ngoma za Botswana zimepata Promotion (kutangazwa). Haziwezi kuchuana na ngoma za kwetu kama Sindimba, Lizombe, Mkwaju ngoma na nyingi ngingine nzuri. Nikiwa huku nilipata kanda  ya dvd  ya ngoma kutoka Botswana. Nikaangalia nikaona tunaweza ni kusaidia tu katika kurekodi. 

Raia Tanzania:  Wewe kwa maoni yako, wa kulaumiwa hasa ni nani? Wasanii wenyewe au Serikali?
Salma: Sehemu ambazo zinazostahili kubeba lawama ni Serikali kupitia wizara yake ya utamaduni na BASATA.  Wasanii wengi tunao tena wenye vipaji.  Wanabanwa na utaratibu na kujikuta wanakatishwa tamaa kwamba si kazi yenye tija.  Vibali vinatolewa kwa mapromota lakini mapromota waliopo wengi si mapromota bali ni wafanyabiashara wanaua sanaa. Anamtumia msanii na kumkuacha. Hawapeleki wataalam ambao wako ofisini kuwasaidia wasanii na wakati mwingine waliopo kwenye nafasi nyeti za kuwasaidia wasanii wakati mwingine hukalia mialiko inayokuja. Hawaipeleki kwa wasanii au kuitangaza. Wageni wengi wanaokuja hawawekewi programu wapi watakwenda kuona utamaduni wetu.  Mimi nakumbuka kwa macho yangu kuna msanii alipewa mwaliko tarehe ya tamasha imepita. Tatizo jingine ni kwamba wasomi wa sanaa hawajikiti kusimamia sanaa za maonyesho. Hata wakiwa kwenye  makundi wanajichagua wenyewe. Niliona wakati ule walianzisha mzee Godwin Kaduma  (marehemu) na Mgunga Mnywenyela kama taasisi ya utamaduni ilikuwa pale Kariakoo na haikushirikisha wasanii wa kawaida. Wasanii wa kawaida hawapaswi kulaumiwa, mtiririko wa sanaa unawaumiza.
Kama kuna mradi wa fedha kama ule uliokuwapo wa kutafsiri kwa Kiswahili filamu ya Neria utakuta wanachaguana wenyewe wasomi, hawashirikishi wasanii wa kawaida.
Nakumbuka kuna wakati unatakiwa kwenda airport au kwenye sherehe bure na usipokwenda kikundi chako kunafungiwa, inaumiza sana.        

Raia Tanzania: Ni juhudi za mwanasiasa gani ambazo unazikumbuka ziliendeleza sanaa nchini?
Salma: Juhudi kubwa za mwanasiasa ambazo nazikumbuka kwa kujituma ye binafsi katika sanaa ni za Mzee Moses Nnauye (marehemu). Mwansiasa huyu alikwenda kwenye majeshi na kuwahamasisha wasanii. Ndiye aliyemvumbua kapteni John Komba (marehemu). Akamwingiza jeshini  akaanza kufanya vitu vyake kwa kutunga nyimbo nzuri.
Mzee Nnauye alikuwa anatunga nyimbo anagawa kwa wasanii, anaingia jukwaani, anashiriki na anakwenda vijijini kusaka vipaji. Mimi binafsi nimefanya naye kazi.  Alikuwa akija DDC  Kariakoo na kwenye kumbi mbalimbali.  Mpaka leo huwa najiuliza kwanini hakupewa Wizara ya Utamaduni.  Angekuwapo hadi leo asingekubali kuona sanaa za maonyesho zinapotea hivi hivi. 

Raia Tanzania:  Ni msanii gani mkongwe ambaye unadhani  alikuwa kama ni alama ya taifa?
Salma:  Msanii mkongwe ambaye nadhani alikuwa alama ya taifa ni mzee Morris Nyanyusa.  Ngoma zake zimetumika sana kwenye  taarifa ya habari. Ilikuwa ukisikia tu unajua sasa ni taarifa ya habari, sijui kama alilipwa inavyostahili  au ilikuwa sifa tu anazopewa.  Alisafiri nchi tofauti duniani na alikuwa kivutio kikubwa Japan.  Licha ya kuwa alikuwa mlemavu wa macho, aliweza kupiga ngoma kumi. Watu  wakija kutoka nje walikuwa wanataka kuchukua notii (wasome alama za mipigo ya ngoma zake) wakapige kwao kama yeye. Hapa (Marekani) kuna msanii Steve Wonder amekuwa kivutio kikubwa kama mzee Morris. 

Paparazi: Ungepata nafasi ya kuwa Waziri wa Utamaduni, ni vitu gani ambavyo ungerekebisha au kuvianzisha?
Salma: Ningekuwa waziri wa utamaduni ningebadilisha sera. Tunataka sanaa itambuliwe kama kazi na pia kama biashara.  Wasanii wanufaike na mtindo wa mameneja au mapromota kuwa ndio wasemaji wa wasanii, hapana. Tunataka wasanii wenyewe waseme. Nakumbuka Bagamoyo marehemu Muhidin Mwalimu aliwahi kumkalisha mtu chini. Tulikuwa kwenye semina ya wasanii marehemu  akamwuliza huyo mtu uko kwenye kikundi gani unapiga chombo gani, akababaika kujibu akamwambia kaa chini, tunataka wasanii.  Nitahakikisha BASATA, COSOTA (chama kinachohusika na hatimiliki za wasanii) vinafanya kazi kwa kushirikiana na wasanii na kuwasikiliza. 

Paparazi: Ukipata nafasi ya kukifufua kikundi chako cha  Ujamaa Ngoma Theatre ungekiendesha vile vile au au ungefanya mabadiliko?
Salma: Nitafanya mabadiliko. Nitaongeza vyombo vya kisasa, mavazi mazuri, kuwa na ukumbi wetu wenyewe. Tunakutana na kujiwekea mafao kama bima za ugonjwa, vifo, kuwa na hisa, kutafuta mikataba nje na kuwasaidia kwenye mikataba yao binafsi. Pia kuboresha maisha yao ili jina la kikundi liwe sawa na jinsi tunavyosaidiana. 

Paparazi:  Unajuta  kujikita kwenye sanaa kwamba ulipotea njia?
Salma: Swali kama hilo niliulizwa pia na mwandishi mmoja kutoka Uingereza. Alipotambulishwa alitaka aandike Mama Salma anasema sanaa imekufa na anajuta. Nikamweleza sanaa haijafa Tanzania, bado ipo.  Ingawa tunaona hivyo wasanii wenye  moyo wapo.  Mimi sijuti kabisa kujiingiza kwenye sanaa. Nashukuru nimeweza kuiwakilisha nchi yangu, India, Zambia na Marekani. Pia sanaa imenipa umaarufu mkubwa.  Naamini  hili suala la kunyonywa wasanii litaondoka, wasanii watafurahia jasho lao. 

Paparazi:  Una ndoto za kuingia kwenye siasa kuwa mbunge au Rais?
Salma:  Napenda siasa. Napenda sana kazi za uongozi. Katika maisha yangu yote nimekuwa kiongozi. Hata nilipotoka nyumbani nilikuwa kiongozi wa Mtaa na huku ni Katibu wa Uenezi. Nina ndoto ya kuwa mbunge na hata kuwa Waziri wa Utamaduni.  Kuwa Rais siwezi kukataa nikiombwa na wananchi. 

Paparazi: Wewe ni miongoni mwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi.  Nini maoni yako kuhusu uraia pacha?
Salma: Suala la uraia pacha ni muhimu kote kote. Kwanza ieleweke kwamba hakuna mtu anayetaka kuikana nchi yake. Watu wengi wanachukua uraia wa kigeni kwa kutaka kupata unafuu wa maisha na hasa  kazi katika nchi walizohamia.  Kuna kazi ukiwa raia ni rahisi kuipata na hata kusomeshwa  na ndiyo utakuta zenye maslahi mazuri zaidi.  Unapata unafuu wa maisha, unapunguziwa gharama.  Ukiwa raia unafuu ule ndiyo unaoutumia kupeleka chochote nyumbani.  Watu wengi wanataka kuwekeza nyumbani lakini tatizo wanajua kwamba watachukuliwa kama wageni. Watoto waliozaliwa huku wakitaka kuja nyumbani itawapa shida.  Kuna Mtanzania mmoja alisimama kumwuliza kiongozi mmoja kwenye mkutano, tutaongozwaje na Mmarekani na sisi ni Watanzania. Yule mhusika akahamaki, utanambiaje Mmarekani na mimi kitovu changu kimezikwa Barabara ya 18 Tanga?  Kusema kweli, watu wengi wanataka waje wawekeze nyumbani.  Ningependa kuwa raia wa Marekani na Tanzania kwa pamoja iwapo itapitishwa sasa.  lakini kwa vile haijapitishwa nitabaki kuwa raia wa Tanzania na kuwezesha kushawishi wawekezaji. 

Paparazi: Kama katibu wa uenezi nini shughuli zako?
Salma: Kama katibu wa uenezi na pia Mtanzania, shughuli zangu ni nyingi hapa Marekani.  Kwanza mimi ni kiunganishi muhimu cha Watanzania waliopo hapa.  Tunaishi kama ndugu. Kila siku tunajadili mambo muhimu yanayofanyika nyumbani au hata hapa Marekani na duniani kwa ujumla. Tunasaidiana kwa hali na mali na kupashana habari sana sana za nyumbani. Nimeanzisha kundi kwenye mtando wa simu wa whatsapp ambalo ni maalum kwa ajili ya Watanznaia waishio ughaibuni na tumewashirikisha pia hata walioko nyumbani wakiwemo viongozi wa ngazi mbalimbali na wasanii. Kwa kweli tunakwenda vizuri sana na nafurahi kwamba mijadala yetu inakuwa mizuri kwani kila mmoja huchangia kwa lengo la kujenga kama Mtanzania. Analaumu panapostahili na kusifia pia panapostahili na hata kutoa mawazo yake mambo gani yanafaa kurekebishwa. 
Mengi tumefanya. Kwa mfano majuzi yaliyopotokea maafa  ya kisiwani Pemba hivi majuzi tulichakarika kuchangisha fedha na kampeni yetu ilikuwa na mafanikio ya kuridhisha.
Kaika misiba na sherehe zote za kitaifa huko nyumbani huwa atunakuwa na wawkilishi wetu ambao hutujuza kila kinachojiri. Kwakweli inapendeza.PapaWanapokuja viongozi wa kitaifa na wa vyama mbali mbali hapa huwa tunafanya juhudi za kukutana nao. Tunafanya mkutano na kuwauliza maswali ambayo tunadhani yanahitaji ufafanuzi wao kuhusiana na misimamo yao binafsi na vyama vyao juu ya mustakabali wa nchi yetu.

No comments:

Post a Comment