TTCL

EQUITY

Wednesday, March 13, 2013

Zanzibar kuelimishwa Polisi Jamii kudumisha amani

KAMATI ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imependekeza elimu ya Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi iendelee kutolewa visiwani humo ili wananchi wengi waweze kuifahamu na kuitekeleza kwa vitendo kwa lengo la kudumisha amani na utulivu.
Kamati hiyo yenye wajumbe tisa inayoongozwa na Mwenyeketi wake, Hamza Hassan Juma, imetoa mapendekezo hayo katika kikao chake kilichoketi juzi jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema.
Taarifa ya Jeshi la Polisi nchini iliyotolewa na Msemaji wake, Advera Senso, ilieleza kwamba wajumbe hao wameliomba pia jeshi hilo kutosita kuwachukulia hatua za kisheria wote wanaochochea vurugu.
Wamemwomba IGP Mwema kuendelea kuboresha makazi ya askari polisi yaliyopo Zanzibar ili kuwafanya askari hao waishi katika mazingira mazuri yanayowawezesha kufanya kazi zao bila bughudha.
Wamependekeza pia kuendelea kuboresha masilahi ya watendaji wa jeshi hilo ili yaweze kuendana na hali halisi ya maisha, kwa kuwa kazi wanayoifanya ni kubwa na inapaswa kuungwa mkono.
Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Alli Mussa, amesema wataendelea kuboresha makazi ya askari kwa kutumia rasilimali zilizopo pamoja na kuwashirikisha wadau wengine wa ndani na nje.
Katika kikao hicho wadau hao wameazimia kukutana mara mbili kwa mwaka kwa upande wa Zanzibar na mara moja kwa Tanzania Bara kwa lengo la kuweka mikakati ya kuimarisha usalama nchini pamoja na kufanya semina za mara kwa mara kwa lengo la kujifunza dhana nzima ya Ulinzi Shirikishi na Polisi Jamii.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Kamishna wa Polisi, Utawala na Rasilimali, Kamishna wa Polisi (CP) Clodwig Mtweve, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Agustino Shio, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano, Lupi Mwaikambo na maofisa wakuu waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu.

No comments:

Post a Comment