Wabunge wote wa vyama vya
upinzani waliokuwa bungeni katika kikao kinachoendelea jioni hii
wametoka nje ya Bunge, wakipinga wenzao kufukuzwa bungeni pamoja na
kitendo cha Mbunge Tundu Lissu kukamatwa.
Zitto Kabwe akiwa na wabunge wa upinzani mara baada ya wabunge hao kutoka nje ya Bunge |
Wabunge
waliokuwa wameamuliwa kutoka nje ya ukumbi wa Bunge na Naibu Spika Dkt
Tulia Ackson ni pamoja na mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda
Mjini Ester Bulaya na Mbunge wa Serengeti Marwa Ryoba.
Wabunge hao watatu wamedaiwa kupinga
uamuzi wa Naibu Spika kuhusu muongozo ulioombwa na mbunge wa Kigoma
Mjini Zitto Kabwe, kuhusu utaratibu uliotumika kumkamata mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Mara baada ya Naibu Spika kutoa maamuzi
ya kuwaondoa wabunge hao watatu bungeni, ndipo wabunge wengine wa
upinzani pia wakaamua kutoka kama ishara ya kupinga maamuzi hayo, pia
ikiwa ni ishara ya kupinga utaratibu wa kukamatwa kwa mbunge Tundu
Lissu.
Nje ya ukumbi wa Bunge, Mbunge wa Kigoma
Mjini Zitto Kabwe, amesema wamefikia hatua hiyo kuonesha kuwa
uataratibu unaotumiwa kukamata wabunge wakiwa bungeni siyo sahihi, na
kwamba kesho wataendelea na vikao vya bunge lakini mapambano
yataendelea.
"Kesho tunarudi bungeni, lakini
mapambano yataendelea, tunataka kuonesha kuwa utaratibu huu wa kuvizia
wabunge kwenye milango ya bunge bila taarifa rasmi ya Spika na bila
kuwaeleza wabunge sababu za kukamatwa kwao siyo sawa. Tukilifumbia macho
litakuja kumtokea mbunge yoyote hata wa CCM" Amesema Zitto.
No comments:
Post a Comment