Mimi namshukuru Mungu kwa kuwa amenipa
afya njema na maarifa ambayo nayatumia katika kuyaboresha maisha yangu
lakini pia kuboresha maisha yako kwa kukuandikia makala ambazo naamini
zinaweza kuyabadili maisha yako endapo utazifanyia kazi.
Mpenzi msomaji wangu, katika kipindi
chote ambacho nimekuwa nikizungumzia kuhusu masuala ya mafanikio,
nimekuwa nikisema kwamba unaowaona leo wana mafanikio, walipambana na
hawakukata tamaa pale walipokumbana na changamoto mbalimbali.
Hawa ni wale ambao walijua fika kwamba
kukata tamaa ni adui mkubwa wa mafanikio. Unapojaribu jambo mara moja
ukashindwa kisha ukakata tamaa, ni dhahiri hukuwa umedhamiria kusaka
mafanikio.
Wenye dhamira ya dhati huwa hawakati
tamaa, watajaribu tena na tena na tena mpaka pale ambapo wataona ndoto
zao zimetimia. Na wewe unayesoma makala haya unatakiwa kuwa hivyo.
Lakini, tambua wapo baadhi ya watu
wanaokuzunguka ambao watafurahi kukuona unaendelea kuishi maisha duni.
Wanakuwa na ile dhana kwamba ukifanikiwa utaringa, hutawaheshimu lakini
pia utaonekana uko juu yao.
Kutokana na hilo usishangae watu hao
wakakupiga vita na wakati mwingine kukukatisha tamaa kwenye yale
unayoyafanya. Watakuambia huwezi kufanikiwa kwa sababu elimu yako ni
ndogo au watakuambia huwezi kupata mafanikio kwa kuwa uko kijijini.
Watakuaminisha kwamba bila kuwa na elimu
kubwa, bila kwenda mjini huwezi kufanikiwa. Ukiwa na akili ndogo
zisizojua kuchambua mambo, unaweza kuona wanachokisema ni kweli na
ukajikuta unapunguza kama siyo kuacha kabisa jitihada za kupambana
kutafuta mafanikio.
Ndiyo maana nikasema kwamba, wewe kama
wewe unatakiwa kujiaminisha kwamba unaweza kuwa kama hao unaowaona wana
mafanikio makubwa. Jiambie kabisa kwamba kukata tamaa kwako ni mwiko.
Ukiwa na mawazo hayo, wale waliojikatia
tamaa ya maisha hawawezi kukushawishi muwe kwenye mkumbo mmoja. Lazima
utakaa mbali nao na kutafuta wale ambao unaamini wanaweza kuwa na mawazo
kama yako.
Nilishawahi kusema kwamba, ukiwa ni mtu
wa kutaka mafanikio, marafiki zako wawe na mawazo hayo. Kaa mbali na
watu wanaokuambia maneno ya kukukatisha tamaa, fahamu hao ni adui
wengine katika kufanikiwa kwako.
Kwa maana hiyo usikubali wale waliokata
tamaa wakukatishe tamaa, pambana huku ukijua kwamba hakuna wa
kuyabadilisha maisha yako isipokuwa wewe mwenyewe.
Ukikubali ndani ya nafsi yako kwamba
umeshindwa na huwezi kufanikiwa, hakuna muujiza utakaojitokeza.
Utaendelea kuogelea kwenye dimbwi la umasikini mpaka pale utakapoamua
kubadili fikra zako.
Hivyo basi, dawa ya wale wasiopenda
mafanikio yako ni kukaa nao mbali na kukubali uwezo ulionao bila
kufikiria watu wanasema nini juu yako. Amini unaweza, kubali changamoto
na uzifanyie kazi kisha muombe Mungu akuongoze katika kila unalolitenda.
Kwa leo naomba niishie hapo ila
nikuambie tu kwamba kama una lolote ambalo linakukosesha amani, usikae
nalo likazidi kukuumiza, unaweza kuwasiliana na mimi kupitia namba za
simu zilizopo hapo juu ili niweze kukushauri.
No comments:
Post a Comment