TTCL

EQUITY

Tuesday, February 7, 2017

Fahamu Sababu za U.T.I kuwapata Wajawazito


Dk. Marise anapatikana Marise Dispensary, njia panda ya Mabibo mkabala na kituo cha mafuta. Simu: 0713 252 394au tutembelee katika ukurasa wetu wa facebook Sweetness of afenction
Na Dk. Marise Richard WAPO wanawake wengi wanataka kujua sababu za wengi wao kuugua ugonjwa wa U.T.I (Urinary Tract Infection). Wengine wamekuwa wakidhani kwamba tatizo la kutokwa na uchafu ukeni ni ugonjwa, wazo hilo si sawa kwani huo ni ugonjwa tofauti kabisa na U.T.I
Tunapozungumzia maambukizi katika njia ya mkojo yaani U.T.I, inamaanisha ni kutoka eneo la nje ya utupu hadi kwenye kibofu na kutoka kwenye kibofu hadi kwenye figo. Kama maambukizi yako katika eneo la kutoka kwenye kibofu hadi kwenye figo, kitaalamu huitwa Lower Urinary Tract Infection na yakihusisha eneo la juu ya kibofu jina hubadilika na kuitwa, Upper Urinary Tract Infection.
Maambukizi katika njia ya mkojo au kama unavyojulikana kwa wengi U.T.I huathiri mfumo wa mkojo ikiwa ni pamoja na ureter ambayo ni kama bomba linalosafirisha mkojo kutoka kwenye figo, pia kibofu cha mkojo na mrija wa kutolea mkojo nje yaani urethra.
Ugonjwa huu unaathiri zaidi kibofu cha mkojo na urethra lakini unaweza pia kuathiri figo. Maambukizi haya yakiathiri sehemu za chini za kibofu cha mkojo kitaalamu huitwa Simple Cystitis au Bladder Infection, na maambukizi hayo yakitokea sehemu za juu za mfumo wa mkojo huitwa Pylonephritis au Kidney Infection.
Ugonjwa huu husababishwa na bakteria anayeitwa Escherichia Coli (E. Coli) na tatizo hili husababishwa kwa kiasi kikubwa na bakteria ambao makazi yao ya kawaida ni kwenye utumbo mpana, hivyo huwa wanapatikana pia kwenye haja kubwa.
Lakini baadhi ya watu wanaweza kupata tatizo hili kutokana na kuingiwa na fangasi ingawa pia zipo sababu nyingine chache. Bakteria wa Escherichia Coli hawasababishi peke yao U.T.I bali huambatana na wengine waitwao Staphylococcus, Saprophyti cus, Pseudom onas, Enterobacter na kadhalika. Maambukizi katika njia ya mkojo lazima yawe ni kwenye njia ya mkojo na si pengine popote.
SABABU ZA U.T.I KWA WANAWAKE Mara nyingi maambukizi haya kwa wanawake husababishwa na kutojisafisha vizuri sehemu za siri na kuvaa nguo za ndani zilizochafu. Pia huweza kusababishwa na matumizi ya pedi za kike zenye kemikali ya kukata harufu ambazo huua bakteria wa asili wa eneo la uke na kuwapa fursa bakteria wanaosababisha maradhi haya kuzaliana kwa wingi.
Halikadhalika upungufu wa homoni ya wanawake iitwayo Oestrogen husababisha bakteria wanaosababisha maambukizi katika njia ya mkojo kuzaliana kirahisi. Matumizi ya baadhi ya dawa kwa muda mrefu, unywaji wa vinywaji vyenye sukari kwa muda mrefu na kutokunywa maji ya kutosha pia huchangia tatizo hili.
Uwepo wa mawe katika figo na mirija ya figo pia ni mojawapo ya chanzo cha maambukizi haya katika njia ya mkojo. Sababu nyingine inayosababisha U.T.I ni matumizi ya maji machafu wakati wa kujisafisha au kuoga ambayo huweza kuweka bakteria kwa urahisi na kusababisha mwanamke kupata ugonjwa huo. Uchafu wa vyoo ni sababu nyingine, kwani matumizi ya vyoo ambavyo ni vichafu huweza kusababisha mwanamke kupata U.T.I kwa sababu ndani ya choo kuna bakteria wengi ambao wanaweza kusababisha ugonjwa huo.
Matatizo haya ya maambukizi licha ya kuwapata zaidi wanawake, huwakumba pia watoto wadogo wa kike kutokana na sababu za kimaumbile ambapo viungo vyao vya uzazi, njia ya mkojo na haja kubwa vipo jirani. Watoto wa kiume ambao hawajatahiriwa nao huweza kupata maambukizi rahisi ya U.T.I iwapo watajisafisha kwa kutumia maji yasiyo salama ambapo huwa rahisi kwa bakteria kubaki katika ngozi inayoning’inia (govi).
Pia wanaume watu wazima ambao hawajatahiriwa wanaweza kupata maambuzi ya U.T.I kutokana na sababu tuliyoitaja ambapo pia ni rahisi kwao kuambukizwa Ukimwi kama watafanya ngono zembe na ndiyo maana tohara kwa wanaume husisitizwa. Maambukizi yanayoshambulia mfumo wa mkojo husababishwa zaidi na bakteria wanaoishi katika mfumo wa haja kubwa kwa kuingia na kujikita katika mfumo wa mkojo. Bakteria wengine wanaoleta maambukizi katika njia ya mkojo ni wale watokanao na magonjwa ya zinaa kama kisonono, klamidia, trimonas na fangasi ambapo huwaathiri watu pale wanapojamiiana bila kutumia kinga na watu wenye maradhi hayo.
Ili kuepuka kupata maambukizi katika njia ya mkojo, mara kwa mara, ni vyema kutumia kinga na kwa wanawake wanashauri kila wanapomaliza kufanya tendo la ndoa wakojoe ili kuondoa bakteria walioingia au waliokaa katika tundu la mkojo wakisubiri kuingia.

No comments:

Post a Comment