Ni matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko
poa! Leo utakuwa nami Rammy Gallis nataka kuzungumza nawe msomaji kuhusu
ishu ya msamaha. Penzi la kweli husamehe! Yawezekana kauli hiyo ikawa
nyepesi sana kuitamka mdomoni lakini ni wachache wenye moyo wa
kuitekeleza.
Tunashuhudia katika maisha yetu ya kila siku jinsi watu waliowahi
kupendana kwa dhati au wanandoa walioishi kwa furaha kwa muda mrefu
wakiachana kwa vurugu na ugomvi kwa sababu ya mmoja wao au wote wawili
kushindwa kusameheana na kufungua ukurasa mpya katika mapenzi yao.
Takwimu zisizo rasmi zinaonesha kuwa zaidi ya nusu ya wanandoa
wanasalitiana na kati ya hao ni wachache mno huweza kuendelea na
uhusiano baada ya kugundua kuwa wamesalitiwa na wenzi wao.
Zipo sababu nyingi zinazosababisha usaliti lakini lengo langu leo
siyo kuzungumzia hilo bali ni kujaribu kuiponya mioyo ya wanandoa au
watu wanaoishi kwenye uhusiano wa kimapenzi, waliojeruhiwa na usaliti.
Yawezekana ulitokea kumpenda sana mwenzi wako, ukaamini wewe ndiyo
kila kitu kwake, ukamtimizia kila kilichokuwa ndani ya uwezo wako lakini
mwisho, ukaambulia maumivu baada ya kugundua kuwa anakusaliti.
Vitabu mbalimbali vya dini vinaeleza kuwa kosa pekee linaloweza
kuivunja ndoa, hata ile iliyofungwa kwa baraka za Mungu, iwe ni
madhabahuni au msikitini, ni USALITI.
Sitaki kupingana na maandiko hayo lakini nataka tujadiliane, ni
lazima kila unapogundua kuwa mwenzi wako amekusaliti dawa yake ni
kupeana talaka au kuachana kwa ugomvi? Dunia imebadilika, wanaume wengi
wanasaliti ndoa zao kwa sababu moja au nyingine, hali kadhalika
wanawake.
Mathalani umefunga ndoa na kuishi na mwenzi wako kwa kipindi kirefu
mkipendana, kujaliana na kuoneshana kila aina ya mahaba lakini akateleza
na kukusaliti ilihali bado anakupenda, utakapoamua kuachana naye na
kwenda kwa mwingine, ukigundua naye anakusaliti utafanya nini? Utaachana
na wangapi? Utaolewa na kuachika mara ngapi?
Bila shaka umeanza kunielewa kwamba siyo mara zote talaka au kuachana
ndiyo suluhisho la usaliti ndani ya ndoa. La hasha! Siwafundishi watu
wasaliti ndoa zao au uhusiano wao kwa makusudi wakitegemea kusamehewa,
hapana.
Ninachotaka kukijengea hoja ni kwamba, hata baada ya mwenzi wako
kukusaliti, bado mna nafasi ya kuendelea na maisha yenu ikiwa tu mtaamua
kulishughulikia tatizo hilo kwa kina bila kujali watu wa nje
wanasemaje.
Usikilize moyo wako, ni kweli amekusaliti! Amekuumiza, unahisi dunia
yote imekuelemea, unatamani kufa au kuua, lakini je, moyo wako
unakuambia nini? Upo tayari kumruhusu mwizi wako ndiye awe mmiliki
halali wa mwenzi wako ambaye umetumia muda mrefu kumjenga awe vile
unavyotaka?
Jibu sahihi halitapatikana kwa kukurupuka, hakuna uamuzi wa busara
unaotoka ukiwa na hasira, jazba au ukiwa na shinikizo kubwa kutoka kwa
marafiki, ndugu, majirani na watu wanaokuzunguka.
Pata muda wa kurelax kisha usikilize moyo wako, majibu yatakayotoka
ukiwa umetulia, ndiyo yatakayoamua kama uendelee au usiendelee na
uhusiano uliosababisha ukaumia.
Yawezekana wewe ndiyo ulikuwa sababu ya mwenzako kuchepuka, au ni
tamaa za kimwili ndizo zilizomsukuma kuyafanya hayo, lakini jambo la
msingi ni kujiuliza; bado anakupenda? Anaonesha kujutia makosa yake?
Anakiri na kukuomba msamaha? Kabla hajakusaliti, mmefanya mambo mangapi
mazuri? Tuliza akili kisha amua.
Wanachokosea watu wengi, inapotokea ugomvi ndani ya nyumba au katika
uhusiano wa mapenzi, wengi huweka vinyongo na matokeo yake, vinyongo
hivyo hukua taratibu na siku matatizo yakitokea tena, ukichanganya na
vinbyongo vya muda mrefu ambavyo mtu anakuwa amevihifadhi, matokeo yake
hasira zinakuwa kali mara dufu na mtu anashindwa kabisa kusamehe, hata
kama ni tatizo dogo limetokea.
Ushauri wa msingi, inapotokea mwenzi wako amekukosea na akakuomba
msamaha, msamehe kwa moyo wote na siyo kuweka vinyongo moyoni. Na wewe
unapomkosea mwenzako, muombe msamaha nausirudie makosa. Kwa namna hiyo,
itakuwa ni rahisi kukusamehe.
No comments:
Post a Comment