Wadau
nchini wamependekeza marekebisho ya sheria ya ndoa ilikumsaidia mtoto
wa kike kuondokana na ndoa za utotoni ambapo wametaka umri wa kuanzia
miaka 18 ndiyo sahihi na sio kama ilivyo sasa katika sheria ya ndoa
ambayo imeonekana kupitwa na wakati kwa dhama za sasa.
Hayo
yalisemwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Mwanasheria wa Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Januari Kitunsi
wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kusitisha ndoa za utotoni nchini.
Kampeni hiyo inasimamiwa na Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia masuala ya watoto ya Save the Children.
Lengo
la kurekebisha sheria hiyo ni kupambana na tatizo la ndoa za utotoni
ambazo ni changamoto ya muda mrefu, ambayo imekuwa ikilalamikiwa mara
kwa mara, Kitunsi alisema.
“Sheria
ya Ndoa ya mwaka 1971, kifungu namba 13, kinaruhusu ndoa kwa mtoto wa
kike kuanzia miaka 15, lakini sasa serikali inataka umri wa kuolewa
uanze miaka 18,” alisema.
Aidha,
Kitunsi alisema mapendekezo hayo yametolewa kutoka katika maoni
yaliyotolewa na Tume ya Marekebisho ya Sheria mwaka 1994 ambayo ilitaka
ili mtoto wa kike aolewe lazima awe amefikisha miaka 21.
Wakati
huo huo, Mwanasheria wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Kitunsi alisema wizara hiyo pia imependekeza kuondolewa
kwa kipengele cha kutaka mtoto aolewe kwa ridhaa ya wazazi. Badala yake, serikali imetaka muhusika aridhie ndoa hiyo.
“Hayo
mapendekezo yote tumeyawasilisha Wizara ya Katiba na Sheria ambapo
ndiyo ina uwezo wa kupitisha marekebisho hayo kabla ya kuanza kutumika,”
alisema Kitunsi.
Aidha,
Mwanasheria wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee huyo
alisema wizara hiyo inaendelea kufanya juhudi za kupunguza ndoa za
utotoni lengo likiwa ni kuhakikisha linamalizika.
Naye
Meneja wa mradi huo, Jasminka Milovanic alisema kampeni hiyo
itashirikisha mashirika mbalimbali ya kimataifa yanayopigania haki za
watoto, lengo likiwa kupunguza ndoa za utotoni ambazo zinasababisha vifo
kwa asilimia 20.
Alisema
kampeni hiyo itakayoendeshwa katika mikoa yote nchini ambayo ina ofisi
za Save the Children, inataka kuhakikisha ndoa za utotoni zinakuwa
historia katika kipindi cha miaka mitatu.
Kwa
upande wake, Mwakilishi kutoka Baraza la Watoto mkoani Arusha, Raphael
Denis alisema ndoa nyingi zinasababishwa na wasichana kuacha shule
kutokana baadhi ya walimu kutoa adhabu kali pindi mtoto anapokosa.
Naye
Balozi wa kupinga ndoa za utoto Tanzania, Valeria Msoka, alisema
anaungana na wadau hao katika vita ya kupambana na ndoa za utotoni kwani
itasaidia kumaliza tatizo hilo, ambalo limekuwa changamoto nchini.
No comments:
Post a Comment