Stephen Mwingira na Wendy Ni,
wakiangalia kwa makini jinsi Rais Obama anavyoelekezwa namna ya kutumia
simu kuendesha mashine hiyo katika Onyesho la ubunifu wa kisayansi
ambalo lilifadhiliwa na Rais Barack Obama katika Ikulu ya Rais ( White
House Science Fair 2016)
April 13, 2016, Rais wa Marekani, Barack
Obama, alifadhili onyesho la mwisho katika utawala wake, onyesho
lililohusu ubunifu katika Nyanja za sayansi ambalo limewahusisha
wanafunzi kuanzia shule za awali, msingi hadi za sekondari kutoka States
mbalimbali za Marekani.
Kwa miaka sita tangu mwaka 2010, Kiongozi huyo wa Marekani amekuwa
akifadhili onyesho hilo lijulikanalo kama White House Science Fair
ambalo limekuwa likifanyia katika Ikulu yake (White House) lengo likiwa
ni kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi, hisabati, teknolojia
na ufundi ( STEM)na hivyo kuibua vipaji vya ubunifu m iongoni mwa
wanafunzi ( young inventors).
Katika onyesho hilo la Aprili 13 jumla ya wanafunzi 130 walishiriki
baada ya kukidhi vigezo vya kuingia katika onyesho hilo. Miongoni mwa
wanafunzi waliopata fursa hiyo adhimu ya kushiriki baada ya kukidhi
vigezo ya ubunifu wao ni mwanafunzi mtanzania Stephen Wilfred Mwingira
ambaye pamoja na wenzake wawili Armo Halwah na Wendy Ni wanaosoma Baruch
College Campus High School ya jijini New York, wamebuni kifaa cha
gharama nafuu (vacuum cleaner) kinachoweza kutumika katika kusafisha
njia za reli za chini ya ardhi ( Subways).
Stephen Mwingira na timu yake, walipata fursa ya kuelezea na
kuonyesha mbele ya Rais Obama namna gani kifaa walichobuni ( Vacuum
Cleaner) kinavyoweza kufanya usafi kwa kufungwa kwenye treni na hivyo
kusaidia katika kuzifanya njia za treni ( subways) kuwa katika mazingira
ya usafi na hivyo kupunguza gharama za usafishaji.
Katika miaka sita tangu Rais Obama ambaye yeye binafsi amejipambanua
kama mpenzi na shabiki mkubwa wa sayansi na ubunifu, onyesho hilo
limekuwa motisha na kivutio kikubwa kwa walimu, wanafunzi, wafadhili na
wataalamu waliobeba katika masuala ya sayansi, teknolojia na hesabu.
Kila mwaka State dining room ya Ikulu hugeuzwa kuwa eneo la maonyesho
ambapo wanafunzi hujipanga na kuonesha vifaa walivyobuni au kutoa
maelezo ya kisayansi ya namna ya kutatua tatizo Fulani kwa kutumia
teknolojia nafuu.
Katika kutambua mchango wa Rais Barack Obama katika kuwahamasisha
wanafunzi kupenda masomo ya sayansi, Ikulu ya White House imetangaza
kwamba Kampuni ya Oracle inayojihusisha na masuala ya teknolojia ya
Komputa katika miezi kumi na nane ijayo itawekeza dola za kimarekani 200
milioni kwaajili ya masomo ya sayansi ya computa kwa wanafunzi wa
kimarekani.
Katika maelezo yake kwa vyombo vya habari kabla na baada ya
kuhitikishwa kwa onyesho lake la mwisho, Rais Barack Obama amesema, mara
zote ambazo ameshiriki kujionea ubunifu wa vijana hao wadogo na wenye
kiu na ari ya kuibua mambo mapya, amekuwa akijifunza kitu kipya na mara
zote amejiona kama anayepungukiwa na kitu kutokana kile anachojifunza
kutoka kwa wanafunzi hao.
“Nimeweza kujionea ubunifu wa hali ya juu, kiu, na hamu ya watoto na
vijana wetu wataalamu wa kesho wa taifa letu la marekani. Ipo siku huko
mbeleni nitajivunia pale ambapo miongoni mwa vijana wetu hawa
watakapoweza kubuni tiba ya kansa.
Nitaangalia nyuma kwa fahari kubwa kwamba niliwawezesha vijana hawa
kuibua vipaji vyao ”. Akasema Rais Obama kwa furaha huku akiwashukuru
wale wote ambao kwa miaka sita mfululizo wamewezesha kwa namna moja ama
nyingine kufanyika kwa onyesho hilo.
No comments:
Post a Comment