HALMASHAURI ya Jiji la Arusha inakamilisha mchakato wa kupata Sh
bilioni 28 za mkopo kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) kwa ajili
ujenzi wa soko jipya la Kilombero.
Hayo yalisemwa jana jijini hapa na Mkurugenzi Mtendaji wa jiji hili,
Juma Idd wakati alipozungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa,
miundombinu ya soko hilo kwa sasa imechakaa na imefikia mwisho wa uhai
wake.
Idd alisema, soko hilo halifai kukarabatiwa hivyo hatua iliyopo ni
kubomolewa na kujengwa soko jipya litakalokuwa na miundombinu bora
kuliko ilivyo sasa.
Alisema wanamalizia uboreshaji wa miundombinu ya Soko la Shuma
lililopo kata ya Elerai ambalo kuanzia sasa litakuwa likitumika
kushushia bidhaa zote zikiwemo matunda, samaki na vitunguu, na
wafanyabiashara watakuwa wakitumia magari madogo kubeba bidhaa zao hadi
soko la Kilombero.
Mkurugenzi huyo alisema, magari yote ya mizigo ya biashara
hayaruhusiwi kushusha wala kupakia mizigo ndani ya soko la Kilombero na
hayo ni maandalizi ya kulibomoa soko hilo ili lijengwe upya.
Akijibu swali la kuondoa harufu ya maji taka na uchafu inayotoka
kwenye chemba za kusafirishia maji taka na kusambaa maeneo mbalimbali ya
jiji, alisisitiza kuwa hilo ni jukumu la Mamlaka ya Maji Safi na Taka
Arusha (AUWSA).
Alisema AUWSA inapochelewa kushughulikia uondoaji wa maji taka
Halmashauri ya Jiji imekuwa ikiwatoza faini ambayo ni adhabu kwa ajili
ya kuwakumbusha wajibu wao.
Aliongeza kuwa, AUWSA imekamilisha mchakato wa kupata mkopo wa fedha
Sh bilioni 200 kwa ajili ya kukarabati miundombinu yake ikiwemo
usafirishaji wa maji taka, kuhamisha mabwawa ya maji taka kutoka eneo la
Lemara kuyapeleka Terat kwenye eneo lililotengwa.
No comments:
Post a Comment