Idadi
ya watalii wanaopanda mlima Kilimanjaro kutoka nje ya nchi Mwaka huu
imepungua kwa asilimia kumi kutokana na uwepo wa tishio la matukio ya
ugaidi katika nchi za Afrika Mashariki,na ugonjwa wa Ebola hali ambayo
inaathiri upatikanaji wa mapato yatokanayo na mlima.
Hayo yamebainishwa na mhifadhi mkuu wa mlima Kilimanjaro Bw.Erastus
Lufungulo wakati akipokea msafara wa maafisa 39 wa jeshi la Magereza
nchini ambao walipanda mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika wenye
mita 5895 kutoka usawa wa bahari kwa ajili ya kuhamasisha utalii wa
ndani.
Amesema wageni wengi kutoka nje ya nchi wamesitisha ziara za
kutembelea hifadhi hiyo ikilinganishwa na miaka iliyopita na kwamba
tafiti zimeonyesha pia uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba Mwaka huu
umechangia kwa kiasi kikubwa kukosa watalii kutokana na wengi wao
kuhofia uwepo wa vurugu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa klabu ya utalii wa jeshi la Magereza
nchini Bw.Estomii Hamis amesema safari ya kupanda mlima Kilimanjaro
ilikuwa ngumu na kwamba kati ya maafisa 39 waliopanda mlima ambao
wamefanikiwa kufika katika kilele cha mlima huo kituo cha uhuru ni 25
pekee.
Nao baadhi ya maafisa wa jeshi la Magereza waliofanikiwa kufika
katika kilele cha mlima Kilimanjaro wamewataka watanzania kujenga tabia
kuthamini vivutio vya utalii vilivyopo nchini na kuvitembelea ili
kuchangia pato la taifa kupitia utalii wa ndani.
No comments:
Post a Comment