Kufuatia
ripoti ya shirika la umoja wa mataifa la idadi ya watu ( UNFPA ) ya
mwaka 2013 kuitaja Tanzania kama moja ya nchi zilizokithiri kwa tatizo
la mimba za utotoni, serikali mkoani Mwanza imewataka wazazi kuacha kuwa
mawakala wa ndoa za utotoni,wala kukubali kufanya mazungumzo na wabakaji
au baadhi ya wanaume wanaowapa mimba watoto wa kike nje ya utaratibu wa
mahakama au vyombo vingine vya dola.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza Magessa Mulongo ameyasema hayo katika hotuba
iliyosomwa kwa niaba yake na mkuu wa wilaya ya ilemela Manju Msambya
wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa
kijinsia, zilizoratibiwa na chama cha wanasheria wanawake Tanzania (
TAWLA ) na kufanyika katika uwanja wa furahisha jijini Mwanza, ambapo
ameliagiza jeshi la polisi kuhakikisha kesi zinazohusu vitendo vya
ukatili wa kijinsia haziishii tu polisi bali zinapelekwa Mahakamani ili
haki iweze kupatikana.
Akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho hayo amesema makundi
ya waathirika wa mifumo kandamizi yakiwemo wanawake na watoto katika
nchi nyingi za bara la Afrika zenye migogoro ya kisiasa na kivita
wamenyimwa haki ya elimu na wengine kuishia kutumikishwa vitani,ambapo
ametumia fursa hiyo kuwahimiza viongozi wenzake, watawala,viongozi wa
kisiasa,viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kusimama kidete kupinga
vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Makamu mwenyekiti wa chama cha wanasheria wanawake Tanzania
Margareth Ngasani pamoja na wakili Costantine Mutalemwa kutoka chama cha
mawakili wa kujitegemea tanganyika tawi la Mwanza wamekemea matukio ya
ubakaji, ulawiti na vipigo visivyokubalika kwani vimechangia kurudisha
nyuma maendeleo ya kielimu kwa watoto wa kike.
No comments:
Post a Comment