AGIZO la Rais na Amiri Jeshi mkuu Mh. Dkt. John Magufuli la kutaka Sikukuu ya Uhuru kuadhimishwa kwa kufanya usafi, limetekelezwa
kwa kasi kubwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Huku viongozi wa serikali, na baadhi ya taasisi na watu binafsi, wamejitolea kufanya usafi
katika maeneo yao ya kazi na maeneo mengine yanayowazunguka.
Juzi
eneo la Kipunguni, wananchi wa maeneo hayo walijitokeza kufanya usafi wa
mazingira kwa kufyeka miti na kulima nyasi pamoja na kuhakikisha
wanazibua mifereji ya majitaka.
Jana pia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo alishiriki kufanya
usafi wa Jiji la Mwanza kwa kushirikiana na wafanyabiashara wa soko kuu,
ambako alitumia fursa hiyo pia kuwataka walipe kodi sahihi kwa
serikali.
Mjini Songea, wafanyabiashara wa samaki katika soko kuu la Manispaa
ya Songea mkoani Ruvuma, wametakiwa kufanya biashara zao za kuzingatia
usafi ili kuendelea kuvutia wateja wao kununua kitoweo hicho.
Mwito huo ulitolewa jana na Mkuu wa Masoko wa Manispaa hiyo, Salum
Homela alipokuwa akikabidhi vifaa vya usafi kwa wafanyabiashara wa soko
hilo ili wavitumie kwa ajili ya kufanya usafi wa mazingira kuzunguka
maeneo wanayofanyia shughuli zao ikiwa ni utekelezaji wa agizola Rais
John Magufuli.
Homela alisema usafi kwa wafanyabiashara ni jambo la muhimu kwani
itasaidia kuepusha watumiaji wa bidhaa zao uwezekano wa kupata magonjwa,
yanaosababishwa na uchafu, ikiwemo ugonjwa hatari wa kipindupindu.
Alisema kuna umuhimu kwa wafanya biashara wote wakiwemo wale wa
matunda, nyama, na bidhaa nyingine sokoni hapo kuzingatia usafi kwa kuwa
watu wengi hasa wageni wanaotembelea manispaa hiyo, jambo la kwanza
wanalohitaji kuona ni namna ya wakazi wa Songea walivyoweza kuzingatia
suala la usafi wa mazingira katika maeneo muhimu yanayotoa huduma
mbalimbali za kijamii.
Aidha naye mkuu wa mkuoa wa Ruvuma ameongeza kwakutoa agizo kali kwa mtu yeyote
atakayebainika kuchafua mazingira atatozwa faini ya Tsh. 50,000/=
papohapo na iwapo atashindwa kutekeleza hilo atakwenda Jela.
Kwa upande wao, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
limeshirikiana kikamilifu na wananchi kufanya usafi katika maeneo
mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu ya Uhuru
Desemba 9.
Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga
alisema jana kuwa usafi ni utekelezaji wa agizo la
Rais John Magufuli. “Mwaka huu, Serikali imeamua kubadilisha utaratibu
wake wa kawaida na shamrashamra za gwaride badala yake imeagiza
kufanyika kwa usafi nchi nzima” alisema Kanali Lubinga.
Alisema, “Usafi kwa sisi wanajeshi siyo jambo la kufundishwa, ni jadi
yetu na ni tabia yetu siku zote kwa hiyo kwa kuwa kambi zetu ni safi
kila siku tutaungana na wananchi wote kufanya usafi katika maeneo
mbalimbali nchini.”
Kutokana na agizo hilo la Rais, taasisi na mashirika mbalimbali
yamekuwa yakijitokeza kushiriki juhudi hizo za kufanya usafi wa
mazingira, lengo likiwa ni utekelezaji wa agizo hilo na kuepukana na
ugonjwa wa kipindupindu.
No comments:
Post a Comment