Jaji Lubuva (kushoto) akifafanua kuhusu taarifa aliyoitoa iliyohusu Upigaji kura kwa Majimbo ya Masasi Mjini na Jimbo la Ludewa, kulia ni Mkurugenzi wa Uhcgauzi wa Tume hiyo BwanaKailima Ramadhani. |
Majimbo ya Masasi Mjini mkoani Mtwara na Ludewa mkoani Njombe
yanatarajia kufanya uchaguzi wa wabunge kesho (20.12.2015) ili kuwapata
viongozi watakaoongoza majimbo hayo kwa kipindi cha miaka mitano.
Majimbo hayo hayakufanya uchaguzi tarehe 25.10.2015 kutokana na baadhi ya wagombea katika majimbo hayo kufariki dunia.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mst. Damiani Lubuva
amewasihi wananchi kujitokeza na kupiga kura kwa amani na utulivu. Jaji
Lubuva amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akiongea na
waandishi wa habari.
Jaji Lubuva (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Uchaguzi Bwana Kailima Ramadhani wakijadili jambo mara baada ya kutolewa kwa tarifa ya Upigaji kura kwa Majimbo ya Masasi Mjini na Jimbo la Ludewa. |
“Tume inawasihi na kuwashauri wananchi kujitokeza kupiga kura kwa
amani. Hakuna sababu Masasi na Ludewa kuwa tofauti na majimbo mengine
yaliyofanya uchaguzi kwa amani na utulivu,” alisema Lubuva.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo amewaonya Viongozi wa vyama vya siasa kutoingilia kazi ya tume katika uchaguzi huo.
“Viongozi wa vyama vya siasa wasiingilie kazi ya Tume ya Uchaguzi.
Ulimwengu unatusifia kuwa uchaguzi uliopita ulifanyika kwa amani. Kila
mwananchi, viongozi wa dini na vyama vya siasa tushirikiane wote
kuhakikisha kuwa viashiria vya uvunjifu wa mani na utulivu vinaepukwa
ili uchaguzi uwe huru, wazi na wa haki,” aliongeza Lubuva.
Jaji Lubuva alisisitiza kuwa watu wakisha piga kura waondoke vituoni
ili kutowazuia wananchi wanaokuja kupiga kura isipokuwa Mawakala na
wasimamizi wa uchaguzi wanaoruhusiwa kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Daftari la Wapiga Kura
litakalotumika ndio lile lililotumika wakati wa uchaguzi Mkuu
uliofanyika Oktoba 25, 2015.
Baada ya uchaguzi wa majimbo ya Ludewa na Masasi Mjini, litasalia
jimbo la Kijitopele Zanzibar ambalo uchaguzi wake utategemea lini
uchaguzi wa Zanzibar utakapofanyika.
No comments:
Post a Comment