Madaktari
bingwa wa hospitali ya rufaa Bugando jijini Mwanza wameendesha zoezi la
huduma ya bure ya ushauri wa afya kwa watu wenye magonjwa mbalimbali
pamoja na kutoa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya milipuko,
ukiwemo ugonjwa wa kipindupindu ambao mpaka sasa umesababisha vifo vya
watu 21 katika mkoa wa Mwanza na wengine 687 kuugua ugonjwa huo kuanzia
mwezi septemba hadi Desemba mwaka huu.
Madaktari bingwa waliojitokeza kushiriki katika zoezi hilo
lililofanyikia hospitalini hapo ni wa magonjwa ya saratani, akinamama,
watoto, magonjwa ya akili, upasuaji, mfumo wa mkojo, macho, meno, tiba
na mfumo wa hewa.
Lengo la zoezi hilo lilikuwa ni kuonyesha umahiri wa huduma za tiba
zinazotolewa na hospitali hiyo pamoja na kufanya usafi wa mazingira,
ambapo wakazi wa jiji la Mwanza na mikoa jirani wamejitokeza kwa wingi
kupata huduma za ushauri wa kiafya.
Naye daktari bingwa wa upasuaji mfumo wa mkojo katika hospitali
hiyo Dk. John Igenga amesema kuwa wagonjwa wengi wamekuwa na uelewa
finyu kuhusu aina ya ugonjwa unaowasumbua, huku daktari bingwa wa
upasuaji wa magonjwa ya koo, pua na masikio (ent), ambaye pia ni
mkurugenzi wa huduma za hospitali hiyo Prof. Japhet Gilyoma ameridhishwa
na mwitiko wa wananchi katika zoezi hilo.
No comments:
Post a Comment