Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa Ladhu
Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar,
kikiwataka wanachama wake kujitayarisha na uchaguzi mkuu wa marudio,
Chama cha Wananchi (CUF), kimesema hakuna makubaliano yaliyofikiwa ya
kurudiwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar na kuwataka wanachama wake kuendelea
kusubiri maamuzi yatakayotolewa na Kamati ya Mazungumzo inayoongozwa na
Mwenyekiti Rais wa Dk. Ali Mohamed Shein.
Tamko hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Ismail
Jussa Ladhu, katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika
katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo eneo la Vuga, Mkoa wa Mjini
Magharib na kuzungumzia mkwamo wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Jussa alisema mazungumzo ya kutafuta muafaka yanaendelea kufanyika
na kuwakutanisha viongozi wa kitaifa wakiwamo Marais wastaafu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambao
ni Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Amani Abed Karume na Dk. Salmin Amour Juma.
Alisema kitakachoamuliwa na kamati ya mazungumzo ambayo wajumbe
wake wengine ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif
Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi,
ndicho kitakachotoa hatma ya mkwamo wa uchaguzi wa Zanzibar.
Alisema taarifa iliyotolewa na CCM ya kuwataka wanachama wake
wajitayarishe kwa uchaguzi wa marudio haina msingi na ukweli juu ya
kinachoendelea kutokana na kuwa na kauli mbili zinazogongana, ya
kuwataka wanachama wajiandae na uchaguzi na kuridhishwa na mazungumzo
yanayoendelea Ikulu Zanzibar, wakati maazimio ya kikao hicho bado
hayajatolewa.
Alisema Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CUF ililazimika
kukutana Desemba 27, mwaka huu na kujadili kwa kina kauli ya CCM na
kuamua kutoka na maazimio matano ikiwamo kuwataka wanachama wapuuze
taarifa ya Katibu wa Uenezi wa CCM Zanzibar, Waride Bakari Jabu, huku
ikiwataka wanachama wake wajipange kwa uchaguzi wa marejeo.
Aidha, Jussa aliwataka wanachama wa CUF kumpa nafasi Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, kuendelea na juhudi
za ngazi ya juu za kuhimiza upatikanaji wa ufumbuzi wa haraka juu ya
mkwamo wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
“CUF haitatetereka, na itasimamia kwa dhati maamuzi yao
waliyoyafanya Wazanzibari kwa njia ya kidemokrasia kupitia Uchaguzi Mkuu
wa Oktoba 25 na italinda chaguo lao la Rais wa Zanzibar, Wawakilishi na
Madiwani wao,” alisema Ismail Jussa.
Alisema wakati macho na masikio ya wananchi yametega Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), Wazanzibari wanastahili kupongezwa kwa
kuonyesha ukomavu wa hali ya juu wa kisiasa kwa kuendelea kutunza amani
na utulivu wakati viongozi wa kitaifa wakiendelea na mazungumzo ya
kutafuta muafaka wa kutanzua mkwamo huo.
No comments:
Post a Comment