RAIS wa Awamu ya Tano nchini, Dk John Magufuli anatarajiwa kuwa mmoja
wa mashabiki watakaoipa nguvu timu ya soka ya taifa ya Tanzania `Taifa
Stars’ katika mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia Urusi 2018 dhidi
ya Algeria kwenye Uwanja wa Taifa keshokutwa Jumamosi.
Akizungumza jana ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said
Mecky Sadiki alisema Dk Magufuli ataongoza watanzania kwenye mechi hiyo
na taratibu zote zimekamilika. “Rais Dk Magufuli amekubali kuja kwenye
mechi kuungana na watanzania wengine, labda kama atapata dharura
nyingine za kiofisi, lakini tunatarajia atahudhuria,” alisema.
Aidha, Sadiki alitumia nafasi hiyo kumwalika Rais mstaafu wa Awamu ya
Nne, Jakaya Kikwete kuhudhuria mechi hiyo pia ili kuwapa hamasa
wachezaji. Kikwete juzi alizungumza na baadhi ya vyombo vya habari na
kusema kama Stars itahitaji ushindi dhidi ya Algeria haina budi
kujituma.
Katika utawala wake, Kikwete alikuwa akihudhuria mechi za timu ya
taifa mara kwa mara, huku Serikali ikibeba jukumu la kulipa mishahara ya
jopo la makocha wa timu za taifa za michezo mbalimbali. Endapo Dk
Magufuli atahudhuria pambano hili, itakuwa mara yake ya kwanza
kujitokeza kwenye shuguli za michezo tangu alipoapishwa wiki iliyopita.
Rais huyo ni mpiga ngoma mzuri. Wakati huo huo, kocha mkuu wa timu ya
soka ya taifa, Taifa Stars, Charles Mkwasa amesema wamejipanga kuifunga
Algeria keshokutwa. Timu hiyo iliyokuwa Afrika Kusini kwa kambi ya siku
10 imerejea jijini Dar es Salaam jana.
Akizungumza na gazeti hili muda mfupi kabla ya kupanda ndege kurejea
Dar es Salaam Mkwasa alisema anafahamu wanakutana na timu ngumu na bora
kisoka, lakini kwenye soka lolote linaweza kutokea.
Alisema katika kambi ya Afrika Kusini amerekebisha makosa kadhaa
aliyoyaona katika mechi zilizopita ikiwemo ya kirafiki dhidi ya timu ya
vijana chini ya umri wa miaka 23 ya Afrika Kusini iliyochezwa juzi na
Stars kulala kwa mabao 2-0.
“Kuna mambo mengi tumerekebisha kama umaliziaji, najua hatuwezi
kumaliza mapungufu yote yaliyopo lakini kwa sehemu kubwa tumejitahidi
kurekebisha,” alisema. “Si kwamba naidharau Algeria, hapana tunaiheshimu
sana, lakini mpira wa siku hizi si kama wa zamani, timu zinajituma
kushinda hivyo nasi tutajituma na tumeshajipanga kila mmoja anafahamu
jukumu lake,” alisema.
“Tunacheza na wapinzani wetu tukijua fika kwamba mpira wa sasa hauna
nyumbani wala ugenini, tumejipanga kupata matokeo mazuri tunajua matokeo
mazuri ndiyo yatakuwa silaha yetu kwenye mechi ya marudiano,” alisema.
Aliwaomba watanzania kujitokeza kwa wingi keshokutwa ili kuwapa nguvu
wachezaji katika kusaka ushindi. “Mabadiliko kwenye timu tunayaona…
ninachoomba watanzania waje kwa wingi Uwanja wa Taifa kushuhudia mechi
hii wachezaji wakiwaona wamejaa uwanjani wanazidi kuwapandisha morali ya
ushindi,” alisema.
Algeria na Tanzania zimeachana kwa mbali kwenye viwango vya ubora vya
Fifa vilivyotolewa Novemba 5 mwaka huu ambapo Algeria ni ya 26 na
Tanzania ikishika nafasi ya 135 duniani.
No comments:
Post a Comment