TTCL

EQUITY

Thursday, March 5, 2015

ZITTO AMJIA JUU NGELEJA KWA KUMTAJA

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto amemjia juu Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja kwa kumtaja juzi mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma wakati akijitetea, kuwa Zitto alipewa fedha na kampuni ya PAP na NSSF.

Aliomba Sekretariati ya Maadili kuchukua kwa uzito maoni ya Ngeleja na kama yana uzito kwa mujibu wa sheria na kanuni, yafanyiwe uchunguzi.

Alisema yuko tayari kwa uchunguzi mahususi dhidi yake kuhusu tuhuma zilizotolewa na nyingine zitakazotolewa na mtu yeyote, ikiwemo madai hayo ya Ngeleja.

“Katika kujitetea mbele ya Baraza la Maadili kuhusu tuhuma dhidi yake za kugawiwa mgawo wa fedha kutoka akaunti ya Escrow, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja alisema kuwa ni kawaida wabunge kupewa misaada na wafanyabiashara na taasisi za umma,” alisema Zitto.

Alisema Ngeleja alirudia tuhuma ambazo kwa mujibu wa Zitto, zilizokwishatolewa huko nyuma kwamba alipewa fedha na kampuni ya PAP na shirika la NSSF.


“Hivyo narudia kutamka kwamba ninataka uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo ufanyike mara moja, wenye ushahidi wapeleke kwenye vyombo vya uchunguzi na niitwe mbele ya Baraza la Maadili kujieleza,” alisema.

Zitto, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema licha ya yeye kushambuliwa, vile vile wajumbe wa kamati wanashambuliwa.

“Nashambuliwa, tunashambuliwa! PAC tunasema hatutetereki,” alisema na kusisitiza tuhuma hizo alizoshazifafanua na hazina msingi wowote, zilikuwa siasa za majitaka.

Aliendelea kusema, “Hata hivyo bado zimekuwa zikijirudia rudia kwa malengo maalumu wanayoyajua wanaotoa tuhuma hizo…Watuhumiwa wa ufisadi wa Escrow hawajazoea kuona taasisi za maadili zikifanya kazi kwa namna ilivyo sasa na hivyo wanajaribu na watajaribu kuhangaika, ikiwemo kutaka kila mtu aonekane ni mtuhumiwa kama wao”.

Alisema ndiyo maana Ngeleja ametaja watu wakiwemo wafanyabiashara, kwamba huwapa fedha wabunge bila ushahidi. Alisema akiwa mbunge ambaye maisha yake ya siasa, ameyatumia kupambana na ufisadi na kuchochea mabadiliko kujenga misingi madhubuti ya uwajibikaji na kuimarisha taasisi zake, yuko tayari kuchunguzwa.

Apongeza Baraza Mbunge huyo alisema anaunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Baraza la Maadili kwa kusisitiza kwamba, ilipaswa kuwa imefanyika kwa muda mrefu kwa kashfa mbali mbali zilizohusisha viongozi wa umma.

Alisema katika kujenga misingi madhubuti ya uwajibikaji nchini ni lazima kila kiongozi aheshimu taasisi kama Baraza la Maadili. Alisema likiendelea kufanya kazi kama inavyofanyika sasa, vita dhidi ya ufisadi itakuwa imepiga hatua na porojo za kuzushiana mitaani, zitapungua.

Utetezi wa Ngeleja Katika utetezi wa Ngeleja mbele ya Baraza la Maadili, Ngeleja aliwasilisha kielelezo cha tuhuma zilizowasilishwa bungeni na Kambi ya Upinzani na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde dhidi ya Zitto kuwa alipokea zaidi ya Sh milioni 30 kutoka Tanapa, NSSF na kampuni ya PAP inayohusishwa na akaunti ya Tegeta Escrow.

Alisema pamoja na tuhuma hizo dhidi ya Zitto kuwasilishwa bungeni na vielelezo na kutaka Zitto afikishwe mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, hakuna hatua zilizochukuliwa.

“Ndio maana nasema hata kama ningepokea msaada huo kutoka VIP Engineering, haukuwa kwa ajili ya maslahi yangu kwa sababu ni utamaduni uliojengeka kwa kampuni duniani kote kutumia sehemu ya faida zao kusaidia jamii, lakini pia nisingekuwa mbunge wa kwanza kupokea msaada wa aina hiyo,” alisema Ngeleja.

Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 2006 kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya uwekezaji (capacity charges), zilizokuwa zinalipwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kabla hazijakabidhiwa kwa anayelipwa, ambaye ni kampuni binafsi ya kufua umeme ya IPTL.

Kabla ya kuzuka kwa mabishano kuhusu tozo hiyo, TANESCO ilikuwa inalipa moja kwa moja kwa IPTL.

No comments:

Post a Comment