Meneja wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) mkoa wa Dodoma, Zakayo Temu amesema kuwa Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 43.89 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya umeme katika mkoa wa Dodoma kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili.
Temu aliyasema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyopo mkoani Dodoma kwa ajili ya kukagua miradi ya umeme ili kujionea utekelezwaji wake pamoja na kuzungumza na wawakilishi wa wananchi. Mbali na mkoa wa Dodoma, kamati hiyo inatarajia kufanya ziara ya kukagua miradi ya umeme katika mikoa ya Singida, Arusha na Kilimanjaro pamoja na kuzungumza na wadau wa madini katika mkoa wa Manyara.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme katika mkoa wa Dodoma chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili, Temu alisema kuwa mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini awamu ya pili unahusisha wilaya zote za mkoa wa Dodoma, wilaya za Chamwino, Kongwa zikiwa mojawapo.
Akielezea kazi ya usambazaji wa umeme katika wilaya ya Chamwino Temu alisema kazi ya kupeleka umeme itahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovolti 33 urefu wa kilomita 171.5 na njia ya msongo wa kilovoti 0.4 urefu wa kilomita 95.
Alisema ujenzi utahusisha pia ufungaji wa transfoma 22 za ukubwa mbalimbali pamoja na kuunganisha wateja wapatao 1,195 kwa gharama inayokadiriwa kuwa shilingi za kitanzania bilioni 8.67.
Aliongeza kuwa katika wilaya ya Chamwino hadi sasa ujenzi wa miundombinu ya umeme umefikia asilimia 52 na wateja 105 kati ya 1,195 wamekwisha unganishwa na huduma ya umeme na kusisitiza kuwa mradi huu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Alitaja maeneo yatakayofaidika na umeme huu kuwa ni pamoja na vijiji vya Fufu, Masanze, Mloda, Handari, Chololo, Kikombo, Igandu, Msanga, Chinangali, Mwegamile, Mpera, Chamwino Ikulu, Solowu, Zajilwa, Segala, Izava, Itiso, Magungu, Osteti, Dabalo, Nzali, Majeleko, Mlimwa, Igamba, Membe na Ikowa.
Alitaja vijiji vingine ni pamoja na Msamalo, Makoja, Mnase, Mgunga, Mlebe, Ndebwe, Handali, Chanhumba, Matumbulu, Igogi, Chaludema, Sazima, Nkowe, Chinyika, Chinyanguku, Nghaheleze, Ikombolinga, Idifu, Miganga, Muungano, Ilolo, Chalinze B, Azimio B na Shule ya Msingi Chinangali II
Wakati huo huo akielezea hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa miundombinu ya umeme katika wilaya ya Kongwa, Temu alieleza kuwa kazi ya kupeleka umeme katika wilaya hiyo inahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovolti 33 urefu wa kilomita 197 na njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4 urefu wa kilomita 66.
Alisema pia ujenzi huo unahusisha ufungaji wa transfoma 51 za ukubwa mbalimbali pamoja na kuunganisha wateja wapatao 1,195 kwa gharama inayokadiriwa kuwa shilingi za kitanzania bilioni 9.24
Alisema hadi kufika sasa ujenzi wa miundombinu ya umeme umefikia kwa asilimia 68 na wateja 30 kati ya 1,640 wamekwisha unganishiwa umeme na kusisitiza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Alitaja vijiji vitakavyonufaika na mradi huo kuwa ni pamoja na Manguto, Matongoro, Nororia, Mlanje, Manyata, Ngomai, Njoge, Chiwe, Moleti, Pingakame, Mlanje, Sejeli, Mkutani, Banyibanyi, Mageseni, Makawa, Mkoka na Magereza Vijiji vingine ni pamoja na Nilini, Ndurugumi, Laikala, Mlali Ng’umbi, Mranana, Chingwilingwili, Ndalibo, Zoissa na Chitego.
Akielezea changamoto katika utekelezwaji wa mradi wa REA Awamu ya Pili Temu alieleza kuwa ni pamoja na wananchi wengi kuhitaji huduma ya umeme katika awamu hiyo japokuwa hawapo kwenye mpango huo kwa sasa na njia ya umeme kutembea kwa umbali mrefu sana kupita kiwango cha kawaida na hivyo kuwa na viashiria vya kupata umeme mdogo kwa muda mfupi. Aidha, alisisitiza kuwa katika utekelezaji wa mradi, baadhi ya wananchi wamekuwa wakijitokeza kudai fidia.
Alisema ili kutatua changamoto hizo kama shirika la Tanesco litaendelea kubaini maeneo ambayo yanahitaji umeme ili yawekwe kwenye bajeti ya Tanesco inayoandaliwa kila mwaka na kwenye maeneo ya vijijini shirika litaendelea kuweka miradi ya REA kwa kadri itakavyokuwa inahitajika lengo likiwa ni kuhakikisha kila mwananchi anafurahia huduma ya umeme.
“Pia tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa miradi ya umeme hususan vijijini kwa maendeo ya taifa ili kuondokana na dhana ya kudai fidia ambayo ni kubwa kuliko bajeti iliyotengwa”, alisisitiza Temu.
No comments:
Post a Comment