TTCL

EQUITY

Monday, March 16, 2015

WALIOMTESA BODIGADI WA ZAMANI WA DKT. SLAA WAFIKISHWA MAHAKAMANI

Viongozi watatu wa Chadema, akiwamo diwani wa Ubungo, wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili ya  kuteka na kujeruhi.
 
Diwani huyo, Boniface Jacob (32), mkuu wa walinzi wa Chadema, Hemed Sabula (48) na ofisa utawala wa chama hicho, Benson Mramba (30) walipandishwa kizimbani juzi wakituhumiwa kumteka aliyekuwa mlinzi wa katibu mkuu wa chama hicho, Khalid Kagenzi.
Akiwasomea mashtaka hayo, Wakili wa Serikali Janeth Kitali alidai kuwa Machi 7, 2015 walimjeruhi na kumteka nyara Kagenzi kwa nia ya kuzuia uhuru wake.

Kitali alidai kuwa washtakiwa hao walifanya makosa hayo kinyume na kifungu cha 225 na 249 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Akisoma hati hiyo ya mashtaka Kitali alidai kuwa Machi 7,2015 washtakiwa hao kwa pamoja wakiwa katika ofisi za makao makuu ya Chadema ziliyopo Mtaa wa Ufipa, Kinondoni walimjeruhi Kangezi katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Kitali alidai kuwa siku hiyo ya tukio washtakiwa hao kwa pamoja, wakiwa katika ofisi hizo za Chadema, walimteka Kagenzi na kumpeleka Hoteli ya River View iliyopo Sinza.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Wakili wa washtakiwa hao, Peter Kibatala akishirikiana na wakili John Mallya waliiomba mahakama kuwapa dhamana wateja wao kwa kuzingatia kifungu cha 148 cha Sheria ya Makosa ya Jinai Sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho 2002.

Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema alimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili na kila mmoja asaini hati ya dhamana ya maneno ya Sh10 milioni na kwamba wadhamini hao wasiwe walimu.

Wadhamini wa washtakiwa hao waliwasilisha nyaraka zao, lakini Kitali aliomba kupewa nafasi kuzihakiki, lakini hazikukidhi masharti na hivyo washtakiwa kutakiwa kupelekwa mahabusi.

Hakimu Lema aliiahirisha kesi hadi Machi 26,2015 kwa ajili ya kutaja kuangalia upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Chanzo cha washtakiwa hao watatu kufikishwa mahakamani ni tuhuma zilizotolewa kuwa Kagenzi alihojiwa na maofisa wa Chadema waliomtuhumu kumwekea sumu Dk Slaa.

Tuhuma hizo zilitolewa hadharani na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando, ambaye alisema Kagenzi alikuwa akishirikiana na maofisa wa usalama wa taifa kutekeleza tukio hilo.

Kagenzi alichukuliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano na baada ya siku kadhaa, aliachiwa huru na kuzungumza na vyombo vya habari yale yaliyomtokea na jinsi alivyoteswa.

Wakati Kagenzi akieleza hayo, washatakiwa hao watatu walikamatwa na polisi kwa mahojiano hadi walipofikishwa mahakamani.

No comments:

Post a Comment