TTCL

EQUITY

Monday, March 16, 2015

MSAKO WA WAGANGA WAJADI WAZUA VIKWAZO MKOANI SIMIYU

Kamanda wa polisi Mkoa wa Simiyu Charles Mkumbo akiongea na waganga wa jadi katika wilaya ya Itilima mkoani Simiyu jana wakati wa mkutano na waganga hao ambapo mkutano huo ulifanyika katika viwanja vya shule ya sekondari Lagangabilili.



Wakati jeshi la polisi katika mikoa ya kanda ya ziwa likiwa katika msako mkali wa kuwakamata waganga wa kienyeji wanaopiga ramli chonganishi katika hali  isiyokuwa ya kawaida Chama cha Mapinduzi wilayani Itilima Mkoani Simiyu  kimemtaka Mkuu wa polisi Mkoani hapa kusitisha msako huo.

Mbali na kumtaka kusitisha mara moja zoezi la msako huo chama hicho kimemtaka kutoa muda wa kutosha kwa waganga wa jadi, ili kupatiwa leseni kwa ajili ya kutambulika kazi zao na serikali ili wasikamatwe katika msako huo.

Agizo hilo limetolewa jana na Mwenyekiti wa CCM Wilayani humo Mohamudu Mabula, wakati wa mkutano wa waganga wa jadi uliofanyikia katika viwanja vya shule ya sekondari Lagangabilili.

Mabula alimtaka Mkuu huyo wa Polisi Mkoa Charles Mkumbo ambaye alihudhulia Mkutano huo, kusitisha zoezi hilo ikiwa pamoja na kutoa muda kwa waganga hao kwa kile alichoeleza baadhi yao wamekamatwa kutokana na kukosa leseni lakini hawajihusishi na upigaji wa ramli.

Alieleza kuwa anatambua umuhimu wa agizo la kiongozi wake Rais Jakaya Kikwete, lakini juu ya uendeshaji wa zoezi hilo amelipinga kutokana na waganga wengi kutopewa muda wa kujiandikisha ili kupatiwa leseni hizo.

"zoezi hili linataka kutukumbusha oparesheini kimbunga kwa wahamiaji haramu pamoja na kukamata majangili..operesheni hizi zimeondoka na viongozi wengi wachapakazi..sasa hatutaki chama kurudia makosa..tunataka operesheini zifanyike kwa amani na siyo kuwashtukiza watu” Alisema Mabula.

Alieleza kuwa maagizo ambayo yamekuwa yakitolewa na viongozi wao ngazi za juu kwa upande wa serikali, yamekuwa yakiwapatia wakati mgumu viongozi wa chama ngazi za mkoa na wilaya kutokana na maagizo hayo kutekelezwa kwa nguvu.

“ sisi kama chama tumeanza kupata malalamiko kutoka kwa wapiga kura wetu..wanasema CCM inataka kuwafukuza waganga wa jadi…kwa hili hatukubali tulalamikiwe tunachoitaji msako ufanyike lakini kwa amani na watafutwe wapiga ramli tu na siyo waganga wote” Alisema
Kiongozi huyo akishangiliwa na umati wa waganga wa jadi zaidi ya 200 waliohudhuria mkutano huo na alisema kuwa yuko tayari kwenda jela kwa niaba ya waganga katika wilaya hiyo, ikiwa zoezi hilo halitasitishwa ikiwa pamoja na waganga wake kutopewa muda wa kutosha kwa ajili ya kupatiwa leseni hizo.

Mbali na kauli hizo mwenyekiti huyo alisema kuwa atapambana hadi ngzi za juu kuhakikisha waganga ambao wanafanya kazi yao kwa kufuata misingi ya sheria na kanuni za nchi hawaonewi kwa kisingizio cha kupiga ramli chonganishi.
Rpc atii amri, asitisha operaisheni.

Kutokana na kauli ya kiongozi huyo Mkuu huyo wa polisi aliposimama kujibu hoja mbalimbali alitamka kusitishwa kwa zoezi hilo katika wilaya hiyo, na kutoa muda wa mwezi mmoja kwa kila mganga kuhakikisha anapatiwa leseni.

Mkuu huyo wa Polisi aliwataka waganga hao kuhakikisha ndani ya muda huo wanakamilisha taratibu zote za kupatiwa leseni, huku akieleza kuwa mara baada ya muda huo kumalizika operesheni itaanza upya.

“ tumesitisha zoezi kama alivyosema mwenyekiti na tunatoa muda wa mwezi mmoja..lakini baada ya muda huo tutaanza msako..ninachowaomba waganga nyote nendeni kwa viongozi wenu mkajiandikishe ili taratibu za leseni ziweze kufanyika.

Alisema kuwa anafahamu taratibu wa kupatiwa leseni hizo unachukua muda mrefu, ambapo aliwataka kufanya zoezi la kujiandikisha ili muda aliotoa ukimalizika ambao watakakuwa wamejiandikisha na kutambulika kwa viongozi wa serikai ngazi zote hawatakamatwa.
Shimautita waunga mkono msako.

Hata hivyo shirika la maendeleo la utafiti tiba asili Tanzania limeunga mkono serikali kuanzisha zoezi hilo la msako mkali la kuwatafuta wapiga ramli chonganishi.

Katibu Mkuu wa shirika hili Dk Aron Machokosi alisema kuwa kutokana na hali ilivyo hivi sasa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi pamoja na vikongwe operesheini hiyo imekuwa katika muda muhafaka.

“ tunaipongeza serikali kwa uamuzi wake huo..ni lazima waganga wa jadi kufuata misingi ya sheria na kanuni za nchi…tunachowataka waganga wote nchi nzima wajiandikishe katika sehemu husika kwa ajili ya kujipatia leseni” Alisema Machokosi.

Hata hivyo katibu huyo alimshangaa mwenyekiti wa CCM kuagiza kusitishwa kwa zoezi hilo, ikiwa pamoja na mkuu wa polisi kutii amri hiyo na kutoa muda huo, kwa madai kuwa agizo hilo limetolewa na kiongozi wa nchi hivyo linatakiwa kufanyiwa kazi bila ya mzaha.

Hata hivyo mikutano ya waganga wa jadi inafanyika huku kukiwepo msako mkali kwa wapiga ramli chonganishi ambao wameelezwa kuchochoa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) pamoja na vikongwe.

No comments:

Post a Comment