Maandamano ya wananchi ya ukosefu wa maji maeneo mbalimbali jijini Arusha,yametikisa jiji hilo leo, baada ya wananchi kuandamana hadi ofisi ya mamlaka ya maji safi na taka jijini Arusha,(AUWSA), wakidai hawajapata maji kwa zaidi ya wiki mbili sasa.
Moja ya Utambulisho wa Jiji la Arusha.
Maandamano hayo yaliyokuwa ya kisayansi, kwa kutumia usafiri wa magari na kuingia hadi ofisi za mamlaka hiyo, yaliwashtukiza maafisa wa Mamlaka hiyo pamoja na wajumbe wa bodi waliokuwa kwenye kikao cha kujadili maadhimisho ya wiki ya maji, kilichoanza juzi na kilele chake machi 21 mwaka huu.
Maandamano hayo yamesababisha kikao cha bodi kuahirishwa kwa muda, na Mwenyekiti wa bodi hiyo Felix Mrema na mkurugenzi wa mamlaka ya maji safi na taka jijini Arusha, AUWSA, Mhandisi Lucy Koye, na wajumbe walilazamika kukutana na wananchi hao kutoa ufafanuzi.
Mkurugenzi wa AUWSA , Mhandisi, Koye, alisema maji yaliyopo kwenye chanzo hicho hayatoshelezi mahitaji ya wananchi, hivyo mamlaka inatafuta vyanzo vingine.
Ameongeza eneo hilo lenye chanzo hicho cha maji halimilikiwi na AUWSA, ndio maana maji yanayozalisha kutoka kwenye eneo hilo ni machache .
Naye Mwenyekiti wa bodi ya mamlaka hiyo, Felix Mrema, amewaambia wananchi hao kuwa kisima hicho hakina maji ya kutosha na pia eneo hilo halijamilikishwa kwa mamlaka hiyo.
Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, amesema hakwenda kuungana na wananchi hao kwa ajili ya siasa, bali amefika kusaidiana kutafuta ufumbuzi na kuwataka wananchi kuondoa vikwazo vilivyopo, ili kuiwezesha AUWSA, kuzalisha maji.
Katika hatua nyingine wajumbe wa bodi, mbunge na wananchi walitembelea chanzo cha maji kilichopo Moshono na kisima (tanki) ambapo wameteua kamati ya watu 15, ambayo itafuatilia upatikanaji wa maji katika eneo hilo la Moshono.
Akitoa maelezo, mhandisi wa maji, Gasto Francis Mkawe, amesema tatizo lililopo ni mgao wa umeme ambao unaathiri uzalishaji wa maji .
Amesema tatizo la maji ni kubwa jijini Arusha, ambapo mahitaji kwa siku ni lita milioni 100 lakini kutokana na mgao wa umeme uzalishaji umeshuka hadi kufikia lita milioni 45 tu ambapo katika eneo la Moshono pekee, uzalishaji umeshuka hadi kufikia galoni 100.
No comments:
Post a Comment