MUSSA Hassan ‘Mgosi’ ameendeleza ubabe wake dhidi ya Simba juzi Jumamosi baada ya kufunga bao la kusawazisha Mtibwa Sugar ilipocheza na Simba na kutoka sare ya bao 1-1.
Hiyo si mara ya kwanza kwa Mgosi kuifunga klabu yake hiyo ya zamani, alifanya hivyo tena timu hizo zilipokutana mara ya mwisho Februari mwaka huu na kutoka sare ya bao 1-1. Mabao yote ya Mgosi yamekuwa ni ya kusawazisha.
Mbali na Mgosi, wafuatao ni washambuliaji waliowahi kuzifunga timu zao za zamani tangu msimu uliopita.
Mrwanda Vs Simba
Straika wa Polisi Moro, Danny Mrwanda aliifungia timu yake bao moja ilipotoka sare ya bao 1-1 na Simba kwenye mechi ya pili ya ligi msimu huu. Mrwanda aliwahi kucheza Simba miaka ya nyuma kabla ya kupata dili la kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi. Bao hilo dhidi ya klabu yake hiyo ya zamani linamfanya Mrwanda kuwa miongoni mwa wachezaji wachache waliopata mafanikio pale walipokutana na timu zao za zamani.
Owino Vs Azam
Msimu uliopita mechi ya Simba na Azam ilikuwa ya kihistoria kutokana na matukio yaliyoghubika mchezo huo. Katika mechi hiyo kwa mara ya kwanza mashabiki wa Yanga waliishangilia Simba wakati wale wa Simba walihamia kuishangilia Azam na kutaka timu yao ipoteze mchezo.
Yanga walitaka Azam ifungwe ili wao waweze kutwaa ubingwa na kuwafanya mashabiki wa Simba kuishangilia Azam ishinde ili mtani wao aambulie patupu. Kwenye mchezo huo beki wa Simba, Joseph Owino aliifungia Simba bao la kufutia machozi Azam iliposhinda mabao 2-1. Owino aliwahi kucheza Azam miaka ya nyuma na kuwa miongoni mwa wachezaji waliozifunga timu zao za zamani.
Kanoni Vs Simba
Beki wa Kagera Sugar, Salum Kanoni aliifungia timu yake bao ya kusawazisha ilipotoka sare ya mabao 2-2 na Simba kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita. Kanoni aliwahi kucheza Simba miaka ya nyuma na kuwa miongoni mwa wachezaji waliozifunga timu zao za zamani. Bao hilo la Kanoni lilisababisha mashabiki wa Simba kufanya vurugu na kuvunja viti kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Okwi Vs Simba
Ikiwa ni mechi yake ya kwanza baada ya kusaini kucheza Yanga, Mshambuliaji Emanuel Okwi raia wa Uganda aliifungia klabu hiyo bao la kufutia machozi ilipolala kwa mabao 3-1 mbele ya Simba, hiyo ilikuwa kwenye pambano la Nani Mtani Jembe, Desemba mwaka jana. Bao hilo lilimfanya Okwi kuwa miongoni mwa wachezaji waliozifunga timu zao za zamani kwani aliwahi kuichezea Simba miaka ya nyuma. Okwi kwa sasa amerejea kwenye kikosi cha Simba.
Msuva Vs Azam
Winga mwenye kasi zaidi nchini, Simon Msuva aliifungia Yanga bao moja, ilipoiangamiza Azam kwa mabao 3-0 kwenye mechi ya Ngao ya Hisani, Septemba mwaka huu. Msuva amelelewa kwenye kituo cha vijana cha Azam hivyo kitendo cha kufunga bao hilo ni sawa na kuifunga timu yake ya zamani ambayo ndiyo iliyomlea kabla ya kutua Yanga.
Mwaikimba Vs Ashanti
Straika wa Azam FC, Gaudence Mwaikimba aliifungia timu yake mabao mawili ilipoiangamiza Ashanti United kwa mabao 4-0 msimu uliopita. Mwaikimba amewahi kuichezea Ashanti miaka ya nyuma kabla ya kusajiliwa Yanga, Kagera Sugar na kisha Azam anayoichezea kwa sasa. Mabao hayo mawili yanamweka kwenye rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi alipokutana na timu yake ya zamani.
Ngassa Vs Simba, Kagera
Mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa aliifungia timu yake bao moja ilipotoka sare ya mabao 3-3 na Simba msimu uliopita. Bao hilo la Ngassa linamweka kwenye orodha ya wachezaji waliozifunga timu zao za zamani ndani ya miaka miwili iliyopita. Ngassa alicheza Simba msimu wa 2012/2013 kabla ya kukamilisha dili lake la kuhamia Yanga.
Ngassa pia aliifungia Yanga bao moja ilipoifunga Kagera Sugar mabao 2-1 msimu uliopita na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyezifunga timu mbili tofauti alizozichezea miaka ya nyuma. Awali Ngassa alikuwa akiichezea Kagera kabla ya kuhamia Yanga iliyomuuza kwenda Azam mwaka 2010.
Nonga Vs Oljoro
Mshambuliaji wa Mbeya City, Paul Nonga naye ni miongoni mwa wachezaji waliowahi kuzifunga timu zao za awali baada ya kuifungia timu yake bao moja ilipoifunga JKT Oljoro mabao 2-1 msimu uliopita. Nonga alisajiliwa na Mbeya City akitokea Oljoro ambayo ilishuka daraja msimu uliopita.
Javu, Bahanuzi Vs Mtibwa
Mastraika Hussein Javu na Said Bahanuzi wao waliweka rekodi hiyo kwenye mechi ya kirafiki wakati Yanga ilipoifunga Mtibwa Sugar mabao 3-1 Agosti mwaka jana. Bahanuzi na Javu waliwahi kucheza Mtibwa miaka ya nyuma kabla ya kusajiliwa Yanga wanayoichezea mpaka sasa.
No comments:
Post a Comment