Tanzania
na Jamhuri ya Watu wa China, Alhamisi, Oktoba 23, 2014, zimetiliana
saini Hati za Makubaliano (Memorandum of Undestanding) ambako taasisi za
China zitawekeza mabilioni ya dola za Marekani katika uchumi wa
Tanzania.
Shughuli hiyo ya utiaji saini imekuwa sehemu ya Mkutano wa Tatu wa
Uwekezaji Kati ya Tanzania na China uliofanyika kwenye Ukumbi wa
Mikutano wa Nyumba ya Kufikia Wageni wa Serikali ya Diaoyutai mjini
Beijing, China.
Aidha, utiaji saini huo ambao utaziwezesha taasisi kadhaa za Tanzania
kunufaika na mitaji na uwekezaji kutoka China ulikuwa sehemu ya ziara
rasmi ya Kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika China kwa mwaliko wa Rais Xi
Jinping. Rais Kikwete ameshuhudia shughuli hiyo ya utiaji saini.
Miongoni mwa Makubaliano yaliyotiwa saini ni pamoja na Makubaliano ya
Ushirikiano wa Kimkakati kati ya Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) na
Kampuni ya China Railway Jianchang Engineering (CRJE) ambako kiasi cha
dola bilioni moja unusu zitawekezwa katika uchumi wa Tanzania.
Kiasi cha dola bilioni moja zitawekezwa katika ujenzi wa mji mpya wa
Salama Creek Satellite, eneo la Uvumba, Wilaya yaTemeke, Dar es Salaam
na kiasi cha dola milioni 500 zitawekezwa katika ujenzi wa Financial
Square, eneo la Upanga.
Aidha, NHC itapata kiasi cha dola za Marekani milioni 200 kutoka
Kampuni ya Poly Technologies kwa ajili ya ujenzi wa Mradi wa Valhalla,
eneo la Masaki, Dar es Salaam.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pia limetiliana saini Makubaliano
na Kampuni ya Hengyang Transformer ambako Kampuni hiyo ya Tanzania
itapata mamilioni ya dola za Marekani kwa ajili ta mradi wa kusambaza
umeme vijijini.
Aidha, Shirika hilo la TANESCO limetiliana saini Makubaliano ya ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Kinyerezi IV.
Halmashauri ya Manispaaa ya Temeke, Dar es Salaam imetiliana saini
Makubaliano na Kampuni ya Jiangyin Tianhe Gasses Group ya ujenzi wa
barabara ya lami ya Kikwete Friendship Highway katika Wilaya ya Temeke.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Saidi Mecky Sadiq na Mkuu wa
Wilaya ya Temeke, Mheshimiwa Sofia Mjema wameshuhudia utiaji saini
Makubaliano hayo.
Vile vile, Mkoa wa Pwani, umetiliana saini Makubaliano na Kampuni ya
Jiansu Shenli Plastics Gropu Limited ya China kwa ajili ya kugharimia na
kuendeleza Mradi wa Viwanda na Uchumi katika eneo la Mlandizi. Mkuu wa
Mkoa wa Pwani, Mama Mwantumu Bakari Mahiza ametia saini kwa niaba ya
Mkoa wake.
No comments:
Post a Comment