Mbinu 6 za kukusogeza karibu na mafanikio ya malengo yako
Jitihada zako binafsi zitakuwezesha kusonga mbele kufikia malengo yako, vilevile kukosa kwako maarifa sahihi kwaweza kuwa sababu ya wewe kutopiga hatua na kurudi nyuma mbali na malengo yako. Soma mbinu zifuatazo zikusaidie kusogea karibu na mafanikio.1. Tafakari kwa makini malengo yako na tambua nini unataka kufanikiwa.
Huwezi songa mbele kama hujui wapi unataka kufika. Pata ramani halisi ya malengo yako yani wapi utaanza na wapi utaishia, kufanya hivyo utajua vizuri njia gani upitie na nini ufanye ili kutimiza malengo yako.
2. Pata picha ya kile unachotaka kufanikisha.
Vuta taswira ya malengo yako, ni kwa namna gani utapitia njia sahihi itakayokufikisha kwenye kilele cha mafanikio. Usiruhusu mtu au watu kukukatisha tamaa, unapoambiwa utashindwa usikasirike bali jipe moyo utafanikiwa tu.
3. Husisha furaha na mafanikio ya malengo yako.
Kusudio la kuhusisha furaha na malengo yako ni kujipa motisha na nguvu ya kuendelea na msimamo wako wa kutaka kufanikiwa. (Consider how you will feel when succeed)
Jiulize, je utakapofanikiwa utajisikiaje? Utakapofanikiwa utasherekeaje? Kwa kuendelea kujisikia furaha utaongeza bidii ya kutafuta unachokusudia kufanikiwa na hatimaye kusogea karibu na mlango wa mafanikio.
4. Husisha maumivu na wazo la kufeli.
Kuwaza je kama nitafeli wakati mwingine husaidia watu wengi kuongeza bidii na mkazo wa kutaka kufanikiwa. Mfano mwanafunzi anapoogopa kufeli atakazana kusoma kwa bidii ili afikie malengo yake ya kielimu. Hii ni sawa pia kwa mtu mwingine yeyote anayetaka kufanikwa katika jambo lolote lile.
Unapotaka kufanikiwa ni muhimu ujiulize maswali yafuatayo.
Je utakaposhindwa kutimiza malengo yako utajisikiaje?
Je watu wanaokuzunguka watakuchukuliaje watakapokuona umeshindwa kwa bahati mbaya? Labda watakuchukulia kama mzembe, mvivu au mtu usiye na dira.
Ukiwa na mawazo haya wakati mwingine hayakubomoi bali yatakukomaza kifikra kwa lengo la kukukumbusha umuhimu wa wewe kufanikisha malengo yako.
5. Jiwekee msimamo wa kufanya mambo ambayo yatakusogeza karibu na mafanikio ya malengo yako.
Anza kwa kutambua maswala muhimu kwanza ambayo utakapokuwa ukiyafanya kila siku yatakusogeza mahali unapotaka kuwa kimafanikio. Hata kama malengo uliyojiwekea ni madogo kiasi gani ni vyema kuyatimiza kwani yatakujengea nidhamu ya kufanya vizuri katika malengo mengine makubwa. Muhimu kwako ni kupiga hatua zitakazokuelekeza kwenye mlango wa mafanikio.
6. Weka msisitizo wa kufanikiwa katika akili yako.
Kuwa na ufahamu wa kile unachofanya kutakusaidia uishi kila siku kwa kuamini ipo siku utatimiza ndoto zako kwakuwa unajishughulisha ipasavyo ili ufanikiwe. Hakuna jasho litakalopotea bure hata kama hutopata kile kitu halisi ulichotegemea kupata kwani ni lazima utakuwa umejifunza kitu kutokana na ulichokitolea jasho na kwa namna moja au nyingine hutokuwa sawa kama zamani kwani utakuwa umepata uzoefu wa kutatua changamoto na kujua nini unafanya.
Kama una chochote cha kuongeza kuhusiana na makala hapo juu, tafadhali usisite kutoa maoni yako!
No comments:
Post a Comment